Uchambuzi Wa Mixtape: Jandoni
Emcee: Testa Tungo Tata
Tarehe iliyotoka: 24.08.2020
Nyimbo: 15
Watayarishaji: Mandellah
Studio: J. M. Music

Nyimbo nilizozipenda: Acha Achepuke, Afrika, Mpe Talaka, X, Adam Mchovu, Husband Material

Testa Tungo Tata

“Wazo la kufanya Jandoni Mixtape lilikuja baada ya kupata wazo la kutoa mixtape itakayobeba elimu na burudani itakayolenga zaidi watoto wa kiume hasa vijana na hapo ndipo nikapata wazo la kufanya mixtape nitakayoiita Jandoni”, anasema Testa Tungo Tata.

Na kusema kweli mradi umesimama kwenye mada hii mwanzo mwisho. Mradi unaanza na utangulizi mzuri uitwao Karibu Jandoni ambao unaonesha moja kwa moja nia ya Testa ni kutumia kinasa chake, mashairi na midundo kuongea na kijana wa kiume na kumpa ushauri kuhusu, ujana, changamoto za marafiki, mahusiano pamoja na umuhimu wa kuangalia tunachokula.

Ngoma ya kwanza toka kwa mradi huu ni Acha Achepuke ambapo emcee huyu anamkejeli bwana mmoja ambae japokua kaoa kashindwa kwenye mautundu ya mahaba kwa mpenzi wake ambae kwa kushindwa kuhimili hili anageukia vi Ben Ten ili kuweza kukosha haja zake. Ni wimbo flani wenye nia ya kuonesha kuwa mapenzi ni zaidi ya mali unazoweza kumpa umpendae, unatakiwa uwe vizuri kwenye show pia.

Changamoto za ndoa kwa kijana wa kiume kwenye ndoa zinazidi kumulikwa zaidi kwenye Mpe Talaka kwenye wimbo wenye mdundo mzuka sana unaomuhimiza kijana kumuacha mke aliemuoa kama hampendi tena kwani kama anavyosema Testa,

”Muache, wanaume tupo, umemuona kimeo/
Ulichokiona kwa mchepuko, tumekiona kwa mkeo”

Madini kibao unayapata pia kwenye wimbo kama Badilika unaomkashifu kijana wa kileo anaependa ‘kitonga’ badala ya kujituma ili aweze kujitegemea kimaisha. Ucheshi kibao ndani ya madini.

Nyimbo nyingine zilizosimama ni kama Adam Mchovu, Afrika, Kivuli pamoja na Husband Material ambazo zinazidi kuonesha wigo wa mawazo ya Testa kupitia mashairi yake. Na usiongelee uchaguzi wa midundo ambao ni mzuri pia hata kama hii ni Kanda Mseto.

Pia nilichokipenda ambacho kwenye mradi huu ni mashairi aliyoyakariri emcee huyu kwenye mradi huu ambayo yalikuwa ya kina sana. Mashairi yenyewe ni Nguvu Za Kiume – Rudia Asili

inayomhamsisha mtoto wa kiume kuwa halisi na kujikubali na kukubali vya mababu zetu vilivyo tupa afya nzuri kama vile kula mihogo badala ya burger.

Shairi jingine ni Porojo Za Mwanaharamu inayohoji hizi imani/dini zetu pamoja na Mshamba. Kwenye shairi Mshamba Testa anatukejeli kwa kujiita mshamba kwani haendi na wakati na kukumbatia mambo ya mitandao ya kijamii, mambo ya kumwagiana maji wakati wa birthday, ama kweli sisi ni washamba, sorry Testa ni Mshamba.

Kupitia mradi huu emcee huyu ameweka msingi mzuri unaomtambulisha vizuri kwa mashabiki na kuwaacha na kiu ya kusubiria kwa hamu miradi yake mingine. Testa Tungo Tata kupitia mradi huu keshapita Jando(ni) la Hip Hop.

Kupata nakala yako wa Kanda Mseto ya Jandoni kwa Tshs 3000.00 pekee. Wasiliana na Testa Tungo Tata kupitia;

Facebook: Testa Tungo Tata
Instagram: testatungotata