The Funk Brothers Trio

Micshariki Africa leo tumetimba Digg Down Records ili kuweza kupiga gumzo na mmoja wa watayarishaji na wamiliki wa studio hii, Troo Funkmonk. The Funk Brothers Trio ni ndugu watatu wa damu wanaofanya kazi kubwa kwenye tasnia ya Hip Hop ya Tanzania. Wamefanya kazi na ma emcee tofauti kama Nash MC, Dambwe La Hip Hop, Mantiki Barz, Abby MP, Watunza Misingi, Nikki Mbishi, Lugombo MaKaNTa, The MC 255 n.k. Karibuni ili muweze kuwafahamu  "Wachimbaji" hawa.

Karibu sana kaka Troo Funkmonk au ukipenda Funk Brother Number One...Kwani kuna Funk Brothers wangapi na je ninyi ni ndugu wa damu?.

The Funk brothers tupo watatu na tunajulikana kama “The Funk Brothers Trio” na wote ni ndugu wa damu yaani ndugu wa baba na mama mmoja.

Japokua hii interview nafanya na wewe ningependa uwawakilishe vyema wale Funk Brothers wengine kwani hapa ni fursa ya kupiga three in One. Jitambulishe majina yako rasmi pamoja na wale funk brothers kisha unieleze mnapatikana wapi na mnajihusisha na nini?

Kwa majina ya utayarishaji wa muziki nafahamika kama “Troo Funk Monk” aka Funkbrother Number 1, majina yangu rasmi kiserikali na katika kitambulisho cha NIDA ni Lingajoune George Lingajoune. Pia katika kundi la The Funk brother Trio kuna ndugu yangu anayenifuatia ni “ILL Funk” anafahamika zaidi kwa utayarishaji wa mdundo wa wimbo wa Tunapotea wa Dambwe La Hip Hop.

ILL Funk ni mtayarishaji wa muziki na muongozaji wa video. ILL Funk kwa uchache sana na mara chache hufanya kazi za utayarishaji wa muziki lakini yeye zaidi amejikita katika uandaaji wa filamu, sinema na video za muziki.

Na wa mwisho ni “De La Funk aka “Astro Funk” yeye amebobea katika utayarishaji wa muziki, kuingiza na kurekodi sauti na uchangayaji wa sauti na kukamilisha nyimbo zote za Digg Down (Mixing and Mastering Wizard wa Digg Down Records).

Hivyo kukamilisha idadi ya ndugu watatu ndani ya kundi moja la utayarishaji wa muziki na video. Kwa sasa The Funk Brother Trio tunapatikana katika Studio za Digg Down Records zinazopatikana Sinza Kwa Remy. The Funk brothers Trio tunajihusisha na utayarishaji wa muziki kwa zaidi ya miaka 12 toka mwaka 2012 mpaka sasa. Tumekuwa tukijihusisha na uandaaji wa miradi mbalimbali ya Hip Hop kama album, mixtape, EP na nyimbo mbalimbali.

Pia zaidi ya kufanya kazi ya utayarishaji wa muziki, tunajihusisha na usimamizi wa vipaji vya muziki vya wasanii ambao wapo chini ya label ya Digg Down kama kundi la Waandamizi na wengine ambao hivi karibuni watatambulishwa kazi zao.

Haya majina yenu yalikujaje na yana maanisha nini?

Troo ni slang ya neno “TRUE” kumaanisha kitu cha kweli, halisia, pekee na bora ilhali neno Monk lina maana ni Mtawa na muunganiko wake unapata Troo Funkmonk.

ILL pia linamaanisha kitu Noma Sana na Astro linahusisha mambo ya anga na nje ya sayari yetu kwa hiyo kama ni kazi za kisanaa maana yake lazima ziwe kubwa sio za nchi hii, sio poa, yaani ziwe kama zimetayarishwa kutoka ulimwengu mwengine. Na kwa kujumuisha jina la mwisho ambalo ni jina la ukoo wa Funk unapata Troo Funkmonk, iLL Funk na Astro Funk kwa pamoja unapata The Funk Brother Trio.

Majina yetu yana ufanano katika jina la mwisho kama ilivyo kawaida kila familia huwa na jina la ukoo na kwetu jina lililoonekana linafaa na lenye maana kubwa sana katika sanaa ni neno FUNK. Kwa hiyo FUNK likaja kuwa jina letu la ukoo katika sanaa na kututambulisha kazi zetu. Hiyo ilipelekea pia hata watu kusema ahhh wale jamaa wa Funk, ndio ikawa imenoga katika kujitofautisha katika kiwanda.

Hii ilianzaje? Neno Funk lina maana ya kitu bora, pekee na kizuri sanaa na baada ya kufatilia sana miziki ya jazz, soul na gospel inapoishia ndio Funk inapoanzia kama muziki yaani muunganiko wa miziki hiyo tajwa unatokeza aina nyingine ya muziki ambao ni FUNK. Muziki unaotawaliwa na baseline kali na ngoma zenye groove hivyo basi hapohapo tukaona ni wasaa wa kuhakikisha bidhaa zetu nazo lazima ziwe za pekee na bora kwa kulitumia kama utambulisho na kulitendea haki neno FUNK kama ukoo wetu kisanaa.

Troo Funk

Hebu tupatie historia yako yenu/yenu kimaisha; uli (mli) zaliwa wapi, masomo shule ya msingi, upili na pengine baada ya hapo?

Kihistoria Troo Funkmonk ni mwenyeji wa Tukuyu, Mbeya. Nimezaliwa mkoa wa Dodoma wilaya ya Kondoa na nilisoma elimu yangu ya awali Shule ya Msingi Miningani, Sekondari nimesoma Tosamaganga High School 2002 na Pia Jitegemee High School kwa kidato cha 5 na 6 mwaka 2006.

Stashahada ya kwanza nimesomea Usimamizi wa Biashara ya Chuo kikuu cha Dodoma mwaka 2008 na Stashahada ya pili ya uzamili nimesomea Sayansi ya Usimamizi wa Masoko, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tawi la Dar es salaam mwaka 2012.

Kwa ufupi, kihistoria na kimaisha The Funk Brothers Trio tunatokea katika familia ya Hip Hop kuanzia baba, mama mpaka watoto ambao ni wanne wote wa kiume, familia yetu ilikuwa ni ya wapenda na wasikilizaji wazuri wa muziki. Nakumbuka miaka ya 1980 mdingi alikuwa ana tabia ya kununua album za tape cassete za pops, house, jazz, na funk kwa wingi sana tulikuwa na box hilo lilikuwa na tape kama 300 hivi.

Baadae taratibu miaka ya 1990 kaka yetu mkubwa naye akaanza kununua tape cassete za album za kina Nas, Onyx, Busta Rhymes, Tupac, Notirious BIG, Coolio, Wu Tang Clan, Timbaland na Magoo kuongeza idadi ya tape kama 500 hivi katika boksi. Baada ya manunuzi ya album hizo za Hip Hop miaka hiyo kaka yetu yeye akawa msikilizaji mzuri sana wa hizo tapes akaangukia katika uchanaji lakini hakufanikiwa kurekodi, zaidi ya kurap katika majukwaa ya kitaa.

Baadae miaka ilivyosonga kwa upande wetu The Funkbrothers mijadala ikajikita katika hizo tapes namna ya uaandaji wa midundo ulivyofanyika, bassline zilivyofumuliwa, gitaa zilivyocharazwa na vinanda vilivyopigwa kwa umaridadi. Mijadala na ubishi juu ya album gani au watayarishaji gani ni noma sana kwa kipindi hicho ikapelekea tutamani kutumbukia ktk utayarishaji wa midundo, huo ndio ukawa mwanzo wa kuanza kujifunza utayarisha kwenye miaka ya 2008.

Mlijikutaje kwenye huu ulimwengu wa muziki na utayarishaji, tupeleke nyuma mlipoanzia, safari ilivyokua hadi hapa mlipofikia.

Kama nilivyodokeza hapo nyuma katika ulimwengu wa muziki kihistoria maisha ya usikilizaji sana muziki nyumbani na ufuatiliaji wa wasanii wa muziki kiundani ulipelekea kuweka misingi ya kutamani kufanya kitu katika muziki. Wanasema ukipenda sana muziki unaweza kufikiria namna gani muimbaji ameimba au mchanaji amechana ukienda ndani zaidi lazima utajikuta umeangukia kuwa mchanaji au muimbaji na ikiwa kama utasikiliza sana muziki na ukakazia fikra namna gani vifaa vimepigwa kwa umaridadi lazima utatokea kutamani kutengeneza hatimaye utakuwa mtayarishaji wa muziki.

Hivyo hivyo mijadala ya muziki tukiwa nyumbani ilikuwa imejikita zaidi katika namna gani vinanda vimepigwa, magitaa yamecharazwa au ngoma zimepigwa na namna gani wimbo mmoja au mwingine umeandaliwa vizuri katika utayarishaji. Taratibu mijadala ilivyozidi baina yetu ndio kiu na hamu ya kutengeneza muziki ilizidi, namna gani na vipi?

Hilo lilipata majibu yake baada ya kuanza chuo na kuwa na laptop hapo safari ya utayarishaji ikaanza mwaka 2008 hii ni kipindi nipo chuo na hapo ndio nikaanza kujifunza kupitia vitabu vya mitandaoni na video za YouTube zinazotoa mafunzo ya utayarishaji wa muziki. Taratibu nikaanza kujifunza software mbalimbali na nakumbuka kipindi hicho nilianza kutumia FL Studio 5 kipindi cha mwaka 2008 baadae nikaendelea kujifunza softaware mbalimbali za utayarishaji mpaka leo hii kujifunza hakujakoma.

Tuongee kuhusu Digg Down...Hii studio ilianzishwa lini, nani wamiliki na nini mnafanya kule?

Studio za Digg Down Records jina lake, mawazo na mpaka logo ya studio, ubunifu wake na jina hili ulifanyika miaka ya 2012. Mwaka huo na kazi mbalimbali za miradi kama mixtape, EP na album zilianza kerekodiwa mapema kabisa katika studio tofauti tofauti jijini Dar Es Salaam lakini chini ya mwamvuli wa Digg Down Records.

Miaka 5 baadae, baada ya kufanya kazi na miradi mbalimbali hatimaye mwaka 2017 basement za Digg Down Records zilizifunguliwa rasmi Sinza Kwa Remy. Studio za Digg Down zinamilikiwa na The Funk Brothers Trio, kundi ambalo linaundwa na wana familia ndugu wa damu. Kundi hilo lina watayarishaji wa video na muziki.

Watayarishaji katika kundi hilo ni Troo Funkmonk, iLL Funk na De la Funk (aka Astro Funk). Studio za Digg Down zinajihusisha na shughuli za utayarishaji wa muziki na video wa genre za aina zote, kurekodi matangazo ya biashara na uingizaji wa sauti kwa ajili ya sinema na filamu. Pia Studio zinajishughulisha na usimamizi wa vipaji vya wasanii ambao wamepata kandarasi ya kupata huduma za wachimbaji katika usimamizi wa kazi zao za sanaa. Miongoni mwa wasanii hao ni kundi la Waandamizi.

Kando na nyie Funk Brothers je kuna watayarishaji wengine mnaofanya kazi pamoja hapo Digg Down Records?

Kwa sasa hatuna watayarishaji wengine wa muda wote wanaofanya kazi katika studio za Digg Down records zaidi ya The Funk brothers Trio. Tumekuwa tukifanya kazi na watayarishaji mbalimbali wa kujitegemea ambao wanafanya kazi pamoja nasi kwa zile kazi za muda mfupi ambazo ni miradi ya nyimbo au album zinazofanyika kwa muda maalumu au mfupi wa mradi husika.

Hii imekuwa kawaida kwetu ikiwa msanii amependelea kuja na mtayarishaji wake katika studio zetu huwa anakaribishwa sana kulingana na aina ya muziki anaoutaka msanii mwenye mradi wake na siku zote milango ipo wazi kwa msanii na mtayarishaji wake anayemtaka yoyote yule anakaribishwa kuja kufanya kazi zake.

Nembo Ya Digg Down Records

Kwa yoyote yule anayetaka kufanya kazi nyie, gharama zenu zipoje?

Gharama za kufanya kazi nasi huwa tunatoza kwa kuzingatia makundi matatu kulingana na bei zetu elekezi katika makundi hayo matatu; kundi la kwanza ni gharama za kuingiza sauti pekee, kundi la pili ni gharama za mdundo pekee, na Kundi la tatu ni gharama za uchanganyaji na urekebishaji sauti na ukamilishaji wa wimbo pekee.

Tunakaribisha wasanii kujipatia bidhaa na huduma kutoka katika makundi hayo tajwa. Kwa Msanii atakayehitaji wimbo uliokamilika huwa ni mjumuisho wa makundi yote hayo matatu na punguzo la bei hutolewa kwa kazi za album, EP na Mixtape kwa bei ya jumla na idadi ya nyimbo.

Bei za kila kundi zinatofautiana na kundi moja hadi jingine na pia hizi hubadilikabadilika kutokana na kuanzia thamani ya mdundo na makundi mengine ya kiutayarishaji. Bei hupangwa kwa kuzingatia bei elekezi na pia uwezo wa msanii na bajeti aliyokuja nayo kwa ajili ya mradi husika vitaamua gharama ya kazi husika kwa hiyo hatuna bei moja. Kwa yeyote yule anayetaka kufanya kazi nasi anaweza kutuona ofisini au kutupigia simu tukajadili biashara na namna gani tunaweza kufanya kazi nae.

Je nyie mmejikita kwa midundo ya Boom Bap pekee au wana Singeli pia wana karibishwa?

The funk Brothers Trio ni wabobezi wa midundo ya Boom Bap lakini sio watu waliojikita katika midundo ya boom Bap pekee. Studio za Digg Down Records sio studio za Hip Hop tu, ni studio za muziki. Hii inamaanisha ni music recording Studio. Wasanii wa Singeli na aina nyingine ya muziki wanakaribishwa sana. Digg Down haibagui aina ya muziki au kuogopa ujio wa aina fulani ya muziki.

Mie nilianza kuwaskia freshi kwenye album ya Mantiki Barz, Shahada Ya Mtaa, kisha Macho Ni Ngumu Kuona ya Dambwe La Hip Hop (na miradi yao mingine) pamoja na Refraction ya The MC 255. Hebu niongezee kazi nyingine ambazo mmezisimamia nyie wana Digg Down iwe ni EP, Mixtapes au hata albums (naomba majina ya mradi na msanii husika)?

Miradi iliyofanyika Digg Down Records/ifuatayo ni productuction catalog toka 2012 mpaka sasa.

Mwaka 2012

Mwaka wa 2012 Studio za Digg Down zilianza utayarishaji  kwa kutegemea kwenda kurekodi na emcee katika studio mbalimbali mitaa ya Mbagala, Gongo La Mboto, Ubungo, Kijitonyama na Sinza kwa kushirikiana na wachanaji wa awali kabisa kufanya nao kazi walikuwa ni Kuga na Mwangalizi. Wimbo wa Maisha ya Kitaa ya “Mwangalizi” na wimbo wa Komando Kuga alifanya Dakika 10 Za Kuga One Take. Kuga alikuwa anajipima uwezo wa kuchana dakika 10 pasipo kusimama au kuungaunga beti.

Mwaka 2013

Nash Emcee - Chizi Mixtape - 2013.

Katika mixtape hii kuna wimbo wa Kuishi au Kuishia, Wanaonijua, Nilivyompata, Nash Da Gama, Chizi(Utangulizi) na Maswali ya Kiwaki zote zimetayarishwa na Troo Funkmonk.

Mwaka 2014

Nash Emcee - Mchochezi EP - 2014.

Katika EP hii kuna wimbo wa Mshairi na Maisha Baada ya Chuo zote zimetayarishwa na Troo Funkmonk

Mwaka 2016

Dambwe La Hip Hop - Macho Ni Ngumu Kuona - 2016

Album ya Macho Ni Ngumu Kuona ya Dambwe La Hip Hop ilifanyika chini ya usimamizi wa Digg Down na pia nyimbo kama Macho Ni Ngumu Kuona, Akili Na Maarifa,Tunakemea, Baraka LA Wakongwe, Nafsi Na Mwili, Hujafa Hujasifiwa, Kichaa Kafanya Mambo na Jamii Kwanza, zote zilitayarishwa na Troo Funkmonk.

Dambwe La Hip Hop

Mwaka 2017

Mwaka 2017 Studio zilifunguliwa rasmi na mradi wa kwanza kuanza kufanyia kazi ulikwa wa Next Level Mixtape ambayo ilirekodiwa takribani nyimbo 15 lakini ulibakia kuwa unreleased project.

Mwaka 2018

Abby MP – Heshima - 2018

Album ya Heshima pia ilifanyika Digg Down na katika utayarishaji wa midundo amefanya Abby Mp na Troo Funkmonk. Nilitayarisha nyimbo mbili ya Pande Mbili Wa RADO na wimbo wa Kitabu amechana Abby MP.

Watunza Misingi – Alkebulan - 2018

Pia Album ya Alkebulan ilifanyika Digg Down Records, nyimbo zote kwa kushirikiana na watayarishaji mbalimbali na nyimbo tatu ambazo katika album hii Ninachokijua, Wapo Uchi, Amsha Unganisha Tekeleza zote zimetayarishwa na Troo Funkmonk.

Mwaka 2019

Dambwe la Hip Hop - Usingizi-Kulala-Kifo EP

Moja ya EP kali katika Hip Hop kwa mwaka 2019 ilirekodiwa Digg Down. Katika EP hii kuna wimbo wa Before Death alitayarisha Abby Mp pia Troo Funkmonk alitayarisha nyimbo kama Itabaki Misingi na Wapokee. De La Funk alitayarisha nyimbo kama Wasinge Kufa na Tutakufa Macho.

Mantiki-Bars - Shahada Ya Mtaa - 2019

Album ya Mantiki Bars nyimbo zote zimefanyika Digg Down Records. Kwa upande wa The Funk Brother TrioILL Funk ametayarisha wimbo wa Galacha, Kabla Hujalala na Dada Yake Baba.  De La Funk nyimbo alizotayarisha ni Nyota Tano, Nje Ya Muziki, Wasalaam, Kibati. Mungu Wangu, zimetayarishwa na De La Funk na mwisho wimbo wa Siku Moja umetayarishwa na Troo Funkmonk.

Mwaka 2019

Nash emcee  Diwani Ya Maalim - 2019

Album ya Diwani ya Maalim pia nyimbo zote zilirekodiwa Digg Down Records kwa kushirikiana na watayarishaji wa muziki wengine ila kwa upande wa Funk brothers Trio, De La Funk alitayarisha wimbo wa Dirisha Dogo na Troo Funkmonk alitayarisha nyimbo zifuatazo Beti, Mwalimu Mashaka, Mpiganaji, Wavuja Jasho, Barua Kutoka Bangui na Mwanaharakati.

Mwaka 2023

Kwa Miaka sasa 12 Digg Down records imetoa na kutayarisha kazi nyingi sana album, single na EP na kwa uchache kazi nilizokutajia hapo juu ni sehemu tu ya baadhi ya kazi zilizofanyika kwa miaka hiyo na kwa ufupi. Mwaka 2023 ni mwaka ambao miradi mingi ilisimama kwa sababu ya kupisha ujenzi na upanuzi wa studio ya kisasa ya audio na video kukamilika. Zipo kazi ambazo zimesharekodiwa tayari hivi karibuni tutazichia kazi hizo za kutosha za wasanii ambao wapo chini ya label ya Digg Down.

Pia watu ambao wamefanya kazi Digg Down kuna emcee mmoja dahhh ni mtu hatari sana nilikua narekodi nae album 💿 tulifika nyimbo 4 tuliplan nyimbo 12 ila nikasafiri 2018 nikaenda bukoba 2019. Emcee mwenyewe ni Big Solo. Bado sijajua kama data bado zipo maana tulikua tukihamia kutoka old Digg Down kwenda New Digg Down Basement. Sijajua kama DATA ZIPO ila mradi huo ni unreleased 🙏🏾

Astro Funk- ana mradi wake binafsi upo YouTube unaitwa

1) Slice X Beat Tape 

2) Ukanda Wa Radi EP (humo ndani Bokonya, The MC 255(Mukimala & Catalyst), DLH, Mantiki, Fivara)

Na pia Astro Funk alishiriki katika mradi wa Boyca wa FUTURE NI LEO kuna wimbo unaitwa Furaha Ni Sasa (Fivara, TK Nendeze, Mantiki Bars)

Troo Funkmonk nilishakuwa na beat tapes tatu

1) Two Hand Full Of Funk (2017).

2) Funk By Nature (2016) –

3) Mchizi Wa Hood Beat Tape (2011).

Pia De La Funky ana mradi wake na Swahili Son - Emotional Pill (2023)

Pia ningependa kupata orodha ya wasanii ambao mmeshafanya kazi ambao hamkufanya full projects ila kazi zao zilipita mikononi mwenu...

Sir Lu, Saigon, Lugombo MaKaNTa, Bokonya, Boshoo Ninja, Mteganda, Rado Kiraka, Kiraka Tosh, Dizasta Vina, Stereo, One The incredible, Lady Jaydee, Nikki Mbishi, Kafeel, Mkemia Wa Rap na Adam Shule Kongwe.

Nieleze kuhusu hii chemistry yenu na DLH ilikujaje maana mkikutana miradi yenu huwa mzuka sana?

Yes, na DLH chemistry ilikuwa mzuka sana, na hata kazi nyingine toka 2012-2023. Hii inatokana na Dira za studio ya kutoa huduma ambazo ni zaidi ya utayarishaji na kurekodi muziki. Kwa sababu kila mtu anaweza kutengeneza mdundo na kila mtu anaweza kumrekodi mtu lakini linapokuja suala la UBORA na UPEKEE wa kazi ni lazima uwe MCHIMBAJI yaani uwe mbunifu na mbobevu katika sanaa yako na hapo ndipo tunapojitofautisha katika kutoa huduma zetu.

Siku zote chochote ambacho kitapitia MCHAKATO WA UCHIMBAJI mara zote kikiinuliwa juu ni lazima kiwe MADINI. Hii ni kutokana na ubora wa kazi zetu sio wa kuungaunga tu bali huhusisha maandalizi ya kujifua katika UBUNIFU na utayarishaji wa MIDUNDO na mada au mawazo ya nyimbo husika huwa yanahusisha UTULIVU wetu katika kazi zetu.

Pia historia yetu ya kuufuatilia muziki kiundani zaidi na sikio letu la muziki ambalo lilijengwa kwa misingi thabiti huwa linafanya yeyote ambaye tutafanya naye kazi lazima iwe muunganiko wenye chemistry na mzuka sana kwa sababu ya michakato ya kichimbaji.

Mbona huwa mnajiita "Wachimbaji"...kwani mna mgodi sehemu na mnachimba nini?

Wazo la kujiita Wachimbaji lilikuja pia sambamba na wazo la jina la studio na katika kulipata jina hilo vitu vilivyoangaliwa ni Dira, Dhamira, Maudhui na aina ya muziki tunaofanya-Hip Hop. Dira na malengo ya studio ilikuwa ni kuhakikisha studio inajikita katika kufanya kazi na wasanii wasio na majina na studio isiyo na jina wote wapate majina kwa pamoja kazi za sanaa zisikike.

Lengo kuu lilikuwa ni KUIBUA VIPAJI kutoka CHINI na kuvifikisha JUU. Tofauti na studio nyingine, studio inapoanzishwa huwa wanatafuta wasanii maarufu ambao wame HIT warekodi nao ili studio ipate jina au pia wasanii wanaotaka kusikika nao hutafuta studio inayosikika iliyo HIT wakiamini wakirekodi katika studio hiyo nao watasikika.

Digg Down Records tuliamua kupita njia nyembamba na kuiacha ile njia pana wanayopita watu wengi, kwa hiyo wazo likawa ni studio isiyo na jina ifanye kazi na watu wasio na majina na hawa wasanii tunawapata wapi? Watu hawa wapo underground unawapataje? Lazima uchimbe, lazima uwatafute katika vilinge, mitaani, na katika mitandao ya kijamii wanapatikana ila hawajapewa sikio japo ni MADINI.

Tukirudi katika aina ya muziki tunaofanya ambao ni Hip Hop ili uunde midundo yake hatua ya kwanza inahusisha mchakato wa KUTAFUTA records za zamani na msamiati unaotumika kwa kitendo hicho ni “DIGGIN”- ohh kumbe DIGG basi tu DIGG, kitendo hicho kilituvutia sana. Dhamira ya kuwasaidia underground ikakazia fikra CHINI YA ARDHI - DOWN hasa tabaka lile ambalo halijapewa umuhimu. IMANI yetu CHINI kule underground ndipo yalipo madini, yaani vipaji vya wasanii halisi ambavyo havijasikika kwa sababu watu hawajachimba kufikia HAZINA hizo.

Pia tuliamua kujikita katika kusimamia MAUDHUI ya nyimbo tunazotayarisha yaani tusipige midundo pekee tu au kurekodi rekodi kiholela bali tuhakikishe tunasimamia mchakato mzima wa kutoa kazi zetu, uwe kama ule wa KUCHIMBA MADINI yaani sio mchakato wa kumuuzia mtu mdundo tu au kumrekodi tu kisha tuchukue hela tumemalizana naye, hapana, tuwe na mchakato, mfanano na wachimbaji wa madini.

Tukaamua tusimamie kazi ikitoka iwe kama madini, pia mchakato wake wa kuanzia wazo la nyimbo, mashairi na mpaka jina la wimbo tuwe tumeupitisha katika MOTO WA WACHIMBAJI. Kimsingi tunahakikisha tunapata wasanii ambao sio tunarekodi nao tu bali shughuli inaanzia kuandaa mada na maudhui ya nyimbo, kutoa mafunzo ya uchanaji, nini wachane, kipi wasichane, nini waandike na nini wasiandike. Hapo sasa ndio maana ya UCHIMBAJI ikaja na tokea hapo UBORA wa kazi zetu ukajidhihirisha kwa kutoa miradi yenye MADINI na kupelekea Digg Down Records kujulikana zaidi kwa aka ya MGODI WA HIP HOP, sehemu ambayo kila siku uchimbaji unaendelea!

De La Funky

Pale studio ni vifaa gani vya kazi mnavyotumia ili kuweza kufanya kazi zenu; hapa naongelea software pamoja na hardware...Je mnapiga vyombo vya muziki pia?

Yes, tunapiga vyombo vya muziki pia. Vifaa na vyombo vya muziki tunavyotumia na kupiga kwa upande wa vifaa analogia ni vinanda kama Korg K49 na AKAI MPK Min, na pia tunatumia Drum Mashine na Sampler kama AKAI MPC Studio na Maschine. Kwa Upande wa vifaa vya kidigitali na program zake ni Studio One, Pro Tools, Cubase na FL studio.

Watayarisha gani waliwapatia motisha ya kuzama kwenye maswala ya utayarishaji?

Watayarishaji waliotupatia motisha katika utayarishaji ni DJ Toomp, RZA wa Wu Tang Clan, Havoc wa Mobb Deep, P Funk, Lindu, Roy(RIP), Timbaland, Dr Dre, DJ Premier, Pete Rock na J Dilla

Changamoto mnazopata wana Digg Down ni zipi na mnakabiliana nazo kwa njia ipi?

Kwa sasa studio haina changamoto inazokabili zaidi tunaona njia nyingi za kuchangamkia fursa ambazo zipo mbele yetu na ni nyingi kweli kweli na hazijastukiwa zipo chini zinahitaji uchimbaji lakini ambazo kwa wengine ni changamoto ila kwetu tunaziona ni fursa kuanzia masoko, mitazamo ya watanzania, vyombo vya habari, na hata vikwazo ndani ya kiwanda cha muziki na kimaisha.

Siku zote tunaamini changamoto au vikwazo vyovyote vile ukiviona kama ni vikwazo vitakuwa kweli vikwazo kwako, ila ukiona matatizo kwa mtazamo wa kuziona njia za kutatulia hivyo vikwazo kwako itakuwa rahisi kukabiliana nazo na kuibuka mshindi.

Bro huu mziki unawalipa nyie the “The Funk Brothers Trio” au pia mnapiga mbanga zingine ili kuweza kuongeza kipato?

Waswahili wanasema usiweke samaki wote katika kapu moja, Akioza mmoja wameoza wote. Kama Digg Down Records hatuna kapu moja la chanzo cha kipato, tuna makapu mbalimbali ya vyanzo vya kipato yanayosaidia kusukuma gurudumu la harakati lisonge mbele.

Hii inasaidia pia kufanya kazi zetu kwa uhuru pasipo kurogeka na Mchawi Tumbo. Pia kwa upande mwingine hii imekuwa msaada sana kwa wasanii chipukizi na kwa wale ambao wanashindwa kumudu gharama elekezi za studio, hii sasa imewapa fursa waweze kusaidika na kupata msaada wetu hata kama malipo yao hayalipi kulingana na thamani ya huduma na uwekezaji tuliofanya. Kiukweli muziki kama muziki unalipa vizuri kabisa taratibu kwa kiasi chake kulingana na muda uliojiwekea na lini unataka uone malipo yake na hapo ndio uvumilivu unapoingia kwa kufanya kazi kwa kufuata miiko ya biashara na sio ushkaji au usela katika biashara. Ukifanya hivyo lazima muziki ukulipe mengineyo ukitarajia kulala maskini na kuamka tajiri huo hautakuwa muziki labda biashara nyingine au betting uweke buku upige milioni kwa dakika 90 hahaha.

ILL Funk

Vipi hali ya Hip Hop Kwa sasa, je ipo sehemu nzuri au twende na mitindo mipya inayoibuka hivi karibuni?

Hali ya Hip Hop kwa sasa ipo vizuri sana tofauti na inavyoongelewa huko mitandaoni. Mambo hayapo kihalisi waongeaji wengi na wachambuzi wengi ni watu walioujua utamaduni kwa ku-u-google au kuusoma katika Wikipedia. Ni vyema na ni sawa kujifunza kwa platform hizo ila upotoshaji sio kitu kizuri hasa kwa wale waliojivika ni wafanyaji wa Hip Hop.

Hip Hop hufanyi, bali unaishi na ni maisha. Tumeona hata wale ambao ni conscious ndio wapo unconscious kabisa na movement nyingini zimekuwa ni movement za kusambaza chuki na unafiki. Hiyo pia ni fursa sana ikiwa movement nyingi zinakuwa ni magenge ya wahuni na walevi ambao ni unconscious, basi kwa watu wale ambao hawana movement wanaweza kuanzisha harakati za kweli zinazosambaza upendo na kuhubiri umoja na sio makundi na watafanikiwa sana wakatengeneza historia kubwa na kuifanya Hip Hop kwa ukanda huu mashariki ikafika mbali kama South Africa Hip Hop ilivyostawika.

Hali ya Hip Hop ni nzuri sana tunaona kumekuwa na movement mbalimbali za Hip Hop na tumeona muunganiko wa wasanii wa Afrika Mashariki na hii pia imewezeshwa na movement ya Micshariki Africa. Ni movement kubwa sana tunaifuatilia kwa ukaribu sana kwani tunaona kazi mpya zinazotolewa iwe Kenya, Uganda au Tanzania hiyo inaonesha activeness ya emcees kwa ukanda huu.

Ni jambo jema sana kuona wasanii wa kanda hizi za afrika ya mashariki wakishirikiana katika miradi mbalimbali hii ni sababu tosha ya ushahidi kwamba hali ni bora kwa sasa na inaendelea kuwa nzuri kadri siku zinavyosonga.

Mitindo mipya inayoibuka hivi karibuni ni jambo jema sana hata Hip Hop iliibuka kama mtindo mpya wa vijana. Kuhusu mitindo mipya hatuna noma nayo na hii ni sawa na KIFO na KUZALIWA kila dakika au sekunde yupo MTOTO anazaliwa na kila sekunde au dakika yupo mtu anakufa hilo halizuiliki na halipingiki. MCEE anazaliwa na pia MCEE  ana KUFA tuwaache WAFU wawazike WAFU wenzao, kikubwa kaidi ni kutoa support kwa emcees wanaozaliwa kulikoni kuwa na hofu na emcees wanaokufa kisanii au kuogopa aina ya mitindo mipya inayoibuka au kuwa na chuki nayo.

Tuna kila sababu ya kujivunia kwa sababu Hip Hop ilianza kama muziki na baadaye ukawa UTAMADUNI kwa zaidi ya miaka 50 sasa mpaka leo. Kama unavyoelewa UTAMADUNI haufutiki au kutoweka kirahisi kama watu wanavyofikiria sio jambo dogo kabisa. Mtindo wa muziki unaweza kupotea lakini siyo UTAMADUNI.

Kuhusu Hali ya Hip Hop, Digg Down hatunaga wasiwasi nayo hata Tanzania asipokuwepo mtu hata mmoja anayewakilisha Hip Hop bado hatutokuwa na Hofu, tutasikiliza Hip Hop toka Tunisia au India hahahaha. Huu ni utamaduni wa DUNIA sio wa south Africa au Nijeria pekee. Mitindo mipya itaibuka itaenda na itapita lakini Hip Hop kama Utamaduni utaendelea milele na milele.

Tukimalizia ungependa kutuambia kitu gani ambacho pengine sisi hatukukuuliza?

Kila kitu naona umelimaliza maswali yote yamegusa kila taarifa au mambo ambayo watu wangetamani kuyajua kuhusiana na Digg Down Records na Wachimbaji. Maswali mazuri sana shukrani mpaka next time tuchekiane tupige story kuhusiana na USTAWI WA HIP HOP na UIBUKUKAJI WA MITINDO MIPYA YA MUZIKI naona hii itabidi tuchimbe zaidi na kuwa na marejeo ya kina.

Troo Funk na Abby MP

Wapi mnapatikana nyie The Funk Brothers Trio pamoja na Studio yenu ya Digg Down Records kwenye mitandao ya kijamii? Pia wapeni wasomaji wetu mawasiliano yenu ya simu pamoja na email kama ipo ili waweze kuwasiliana nanyi.

Studio za Digg Down Records zinapatikana Sinza Kwa Remy, Sinza B-Barabara ya Zinga.

Namba za simu kwa ajili ya mawasiano ni

Tel No: +255-679-531-530

Kwa Mawasiliano ya

WhatsApp: ni +255-753-530-531

Mitandao ya kijamii instagram tunapatikana kwa kurasa hizi

Instagram:@diggdownrecords
Instagram@troofunkmonk
Instagram:@de_la_funky
Instagram: @illfunkmonk

    Shukran sana wanafamilia wa Digg Down kwa kutupatia fursa kuongea nanyi na kuweza kuwafahamu #Wachimbaji...kila la heri!

    Aksante sana. Shukrani sana kwa nafasi hii adhimu.