Msanii: Tin Kais
Kanda Mseto: Ndoto Za Boy Wa Mtaa
Tarehe iliyotoka: 09.12.2019
Nyimbo: 6
Producer: Adabia
Studio: Afdope Records
Binadamu huwa anapata misukumo tofauti tofauti maishani mwake inayomuwezesha kufikia malengo yake. Moja ya misukumo hii ni ndoto; ndoto juu ya jinsi atakavyofanikiwa maisha yake, ndoto kuhusu familia yake, ndoto za kifedha, ndoto za mapenzi na pia ndoto za kukuza vipaji vyake.
Ndoto hazina umri, mtoto ana ndoto ya kila anachotaka kuwa, kijana anaweza kuwa na ndoto ya kupata mchumba wa kuoa ilhali wazazi wana ndoto kuwa watoto wao watafanikiwa ki maisha.
Tin Kais pia ana ndoto zake ambazo aliamua kuziandika ndani ya daftari kwanza kabla ya kuamua kutushirikisha kwa kutumia kinasa. Matokeo yake ni mradi aliouita Ndoto Za Boy Wa Mtaa.
Martin Ng’ang’a Kiiru ni emcee aliyezaliwa Thika, Kenya, miaka ya tisini. Jina la Tin Kais ni ufupisho wa majina yake; Tin likiwa herufi tatu za mwisho wa jina lake rasmi Martin ilhali Kais limetoka kwenye jina lake la ukoo, Kairu linavyoitwa kwenye lugha ya Nairobi ya ‘sheng’.
Tin Kais ni emcee anayepatikana mahandaki ya Thika kule Kenya alipokuwa akikuza kipaji chake cha uandishi na uchanaji hadi 2017 alipoanza kuonekana kwa mashabiki baada ya kurekodi ngoma yake ya kwanza ijulikanayo kama “Ndoto Za Boy Wa Mtaa”. Ndoto yake iliyoanza akiwa shule ya upili ilianza kutimia.Kilichompa msukumo Kais kuchana ni changamoto zetu za Kila siku mambo yanayotokea kwenye bara letu la Africa na jamii inayomzunguka.
Single ya Ndoto Za Boy Wa Mtaa ndio iliyozaa Mixtape hii ya kwanza toka kwa Kais na ndio iliyompa ari ya kufanya mradi wake uliozidi kumtambulisha zaidi kwa mashabiki wa hip hop. Tin kazaliwa mtaani, kaishi mtaani, kajifunza mambo mengi mitaani, kakulia mtaani, anaishi mtaani na bado anaiwakilisha mitaa. Album imebeba changamoto na ndoto za msanii yoyote anayechipuka.
Mradi unaanza na singo iliyobeba jina la kanda mseto; Ndoto Za Boy Wa Mtaa, Kais anaeleza kinaga ubaga ndoto zake kama kijana na mchanaji chipukizi kwenye hili game. Vinanda vilivyoundwa ki ustadi vinampa Kais uhuru na motisha ya kujiachia kwenye kinasa. Kama chipukizi yoyote, Kais anaweka msimamo kuonesha yeye ni nani,
“Kaa ni class, basi mi ndio teacher/
Kama nambari ni one, basi mi ndio kichwa/
Najiamini zaidi ya kujisifu, vifua mbele na kiburi/
{Najitahidi kila time tena kwa bidii, kua oriji}/
Elevate Me (B.O.A.T) ni track mzuka sana inayoonesha chimbuko la Tin Kais, toka nyumbani alipozaliwa, maisha yake mtaani na kilichompa motisha ya kuandika na hadi sasa. Kwa chipukizi yoyote anayetaka kuanza akiskia wimbo huu atajua Roma haikujengwa kwa siku moja. Kais anaongelea changamoto zake hivi,
“I was bright at school, kila mtu alijua/
Mama hope yake kubwa kwangu nita make it hadi campus/
But if only she knew nimepate new area of interest/
Sometimes baada ya kusoma naandika tu mistari/
Akiuliza, na mshow hizi ni poems/”
Kwenye wimbo huu Tin anajionesha vile yeye anajua kuandika na kusimulia hadithi. Kaomba mashabiki wamuinue- “Elevate me”.
Dream Chaser ni nyimbo nzuri sana kwenye kanda mseto ya Ndoto Za Boy Wa Mtaa. Vinanda ni vya hali ya juu ki Cold Play pamoja na kiitikio cha wimbo. Dream Chaser ukiiskia ni kama uko ndotoni. Mdundo wa producer Adabia umepigwa ki ustadi utadhani jamaa la mamtoni umesimama sana na unamsaidia Kais kueleza ndoto Zake vilivyo.
Samples za mkongwe wa Hip Hop Redman toka kwenye nyimbo ya iitwayo "I'll Bee Dat" zimetumika kwenye single iitwayo Fool inayosema ukisimama kumlenga mbwa yoyote njiani anayekubwekea utapoteza muda. Na mbwa wanabweka kweli kwenye wimbo huu. Usibishane na mjinga anasema Kais, wacha wabaya wako wabweke kama mbwa. Redman anaafiki akisema, “That’s True”. Sampling nzuri.
“Failure Sitambui” single nyingine ndani ya album inaonesha jinsi Tin Kais alivyoamua kuwa hakuna kitakachomzuia kutimiza ndoto zake. Ukijaribu kuwa kizuizi cha ndoto zake utajua haujui.
“Don’t Come Close” ndio wimbo unaotufungia kanda mseto ya dogo huyu mwenye kipaji. Huu ndio wimbo pekee aliowashikirikisha ma emcee wengine kama Star 1(ambaye yuko kule Kenya ki masomo) na Kay K. Ni track ya mapenzi ambayo anasisitiza kuwa akiingia kwenye sakafu la kucheza ngoma akiwa na mpenzi Wake, asimkaribie mtu.
Tin Kais akizidi kuandika ana uwezo wa kuzidi kufanikisha ndoto zake kwani bado kuna maeneo tofauti tofauti anaweza kuboresha ki unandishi na kiuchaniji ili aweze kuwa mtunzi mzuri zaidi . Safari ya kufikia ndoto zake ndio imeanza.Hatuna budi kumtakia Safari njema kaka Kais.
Tin Kais – Failure Sitambui (Video) - https://www.youtube.com/watch?v=zryBXsiKdhQ