Wasanii: Tingu na Tofa Tofali
Tarehe iliyotoka: 25/03/2021
Nyimbo: 17
Wapiga midundo na ma producer: AP Made It, Miracle Noma, Binara, Tony Elshabaz,
Mixing & Mastering: Nebo J, AP Made It,
Studio: Rockside Music
Kwa watu ambao awali walikuwa hawafahamiani Tingu na Tofa Tofali walikutana kama zali. Kule Singida kwenye studio anayo patikana producer AP Made It, vijana hawa walikuwa wakienda kila mtu kwa muda wake kufanya kitu anachokipenda, kuchana. Baada ya AP Made It kuwasikilizisha wawili hawa kazi za mwingine bila ya wao kufahamiana ilionekana kuwa kuna ulazima wakutane.

Tingu
Wawili hao ni Tingu akifahamika rasmi kama Newton Ntandu Kitundu na Tofa Tofali akijulikana rasmi kama Christopher Anyambi Robert. Jina la Tofa Tofali limetokana na kufupishwa jina la Christopher kuwa Tofa.

Tofa Tofali
Kilichotokea ni vijana wawili wenye mapenzi ya dhati na Hip Hop kuamua kufanya kazi bila kuwa kundi na matokeo yake ni mradi wao makini sana Naishi Na Hip Hop.
Wimbo Uwezo ndio zao la kwanza walipofanikiwa kuingia booth pamoja kwa mara ya kwanza. AP Made It alihakikisha amewapatia mdundo flani soulful sana na ma emcee wote walitamba vilivyo. Wimbo umejaa madini ya majigambo kama zilivyo asilimia themanini ya nyimbo kwenye mradi huu.
Kwenye Intro ma emcee hawa wanatupa utangulizi mzuri unaotuonesha maana halisi ya Naishi Na Hip Hop huendana vile wanavyovaa, vile wanavyotembea, vile wanavyoongea, wanavyo chana, wanavyofikiri na wanavyo waza hadi watakapofukiwa ardhini. Hivyo basi mradi huu mwanzo mwisho maudhui ni maisha na Hip Hop.
Baada ya kuwakumbuka waliotutangulia mbele ya haki kwenye wimbo wa R.I.P ambao unachanwa na Tingu, Tofa anatufungulia mradi rasmi akitusimulia story kuhusu maisha ya yanki flani kwa jina Konoradi kwenye mdundo unaotumia sampuli nzuri, vinanda na violin inayopiga kwa kusikitisha tunapopata simulizi.
Uwezo wa kusimulia hadithi toka kwa Tofa Tofali unazidi kuonekana tena kwenye wimbo unaoitwa Kibaoni ambao unatupa taswira ya kuogofya kuhusu kitaa hiki na beat iliyotumika ni ya Smash Bong wimbo ukiwa ni Modus Vivendi.
“Daily doria mapoti wanazunguka/
Na asubuhi utaskia flani amekutwa amekufa/
Juu ya mawe amefia na mwili ukatupwa/
Majambazi wamevizia mapoti hawajustuka/
Na maisha yanaendelea vigodoro kila siku/
Huku tushazoea migogoro kila usiku/
Ndio maana mpaka leo bao zinapigwa/
Na ukijifanya Commando kipondo kitahusika/”
Tingu pia kama vile Tofa pia anapata fursa ya kutuonesha uwezo wake wa story telling anapochukua kinasa na kutusimulia kuhusu chimbuko lake kwenye Natokea Singida. Tingu ana bless track yenye beat mzuka sana toka kwa wimbo wa Big Drastic unaoitwa Family First (Saul Goodman).
Katika hali ya kuonesha umoja na upendo kwa ajili ya Hip Hop na kati ya wana Hip Hop ma emcee hawa na walitupa nyimbo kama Tuko Happy na Naishi Na Hip Hop. Hizi nyimbo zinakupa matumaini bila kujali unachokipitia kwa sasa. Kwenye nyimbo zote mbili ma emcee wote wanachana pamoja na mashairi yao yamesimama vilivyo. Kiitikio cha Tuko happy kinasema hivi,
“Tuko happy/
Japo hatupati kila kitu/
Tuko wapi hatupati kila usiku/
Tuko hapa/
Tuna tungo takatifu/
Very happy kama tutaishi kila siku/”
Naishi Na Hip Hop ni wimbo mzuka sana ambao ndio uliobeba jina la Kanda Mseto hii na ma emcee hawa wanabadilishana mic wakionesha mapenzi yao ya dhati kwa mpenzi wao Hip Hop. Wimbo huu kama vile wa Common I used to love H.E.R pia utakukumbushia wewe mwana Hip Hop siku ile ulipokutana na binti Hip Hop na kumpenda kiukweli. Speaker zinapiga taratibu mistari ikitoka hivi,
Tofa Tofali:
“Nilikupenda ukaniteka tangu niko vidudu/
Radioni ulipochezwa niliweka sauti juu/
Ili usikike vizuri nilitoboa madumu/
Nilitoroka skuli na kisa ni wewe tu/
Tingu:
“Sasa wapi nikakae/
Yupi anifae/
Kwako nishazama acha niwatoe nishai/
Ulinipa nilipokwama ili nitoke gizani/
Toka enzi napigana umenijenga Imani/”
Hii one –two inaendelea hadi pale kiitikio kinaposema,
“Nikikusikia huwa napata mizuka/
Nitakusifia mpaka siku utayokufa/
Acha wachonge sana/
Wabonge bonge sana/
Milele, mimi naishi na Hip Hop/
Mimi ntaishi na Hip Hop/
Na nachoishi ndio Hip Hop/”
Shabiki yoyote wa kweli wa Hip Hop ataelewa wanachokichana ma emcee hawa kwenye wimbo huu.
Mistari pia ni wimbo unaoendeleza maudhui ya Hip Hop pale Tingu anaposhika kinasa solo na kumuuliza kinasa anataka nini na microphone nayo inamjibu kuwa anachokitarajia ni yeye achane mistari mizuri. Mdundo uliotumika na ulioundwa ki Battle Cat au Dj Quik ni Summer Time wa Solja Sick.
Majigambo kwenye tasnia ya Hip Hop ni kawaida na nyimbo kadhaa kwenye albam hii zimejaa mashairi ya kujipiga kifua kama King Kong kama vile Tingu, Kibaoni Cypher, Kibonge mimi, Uzamivu na B-54(Bars). Nyimbo hizi zina ma punchline kibao zenye ucheshi kama vile,
“Hali mchele/
Ndio sababu hatemi pumba/”.
Yuda ipo tofauti kidogo na unamkuta Tingu akiwa solo akiongelea usaliti wa kila aina unaopatikana kwenye jamii zetu. Baada ya kutukumbushia usaliti wa Yesu Kristo, Tingu anaendelea kwa kutuonesha usaliti unaopatikana ndani ya maisha yetu ya kila siku; kwenye makundi yetu, kwenye ndoa zetu na kathalika. Tingu hapa anabwaga manyanga na kuweka bayana kuwa wasaliti wetu huwa ni watu wetu wa karibu.
Mixtape hii ni introduction nzuri toka kwa Tingu na Tofa Tofali. Uwezo wao umeonekana bayana na mie sasa naweza sema nasubiria kwa hamu na ghamu albam zao aidha wakiwa pamoja au ya mmoja mmoja
Mradi huu nimeukubali sana na kama anavyosema Tofa Tofali kwenye B-54(54 Bars) wao ni “(Wa)stahiki meya wa jiji la mistari/(Wa)Nastahili kupewa heshima na nishani/”. Hivyo basi kazi kwao sasa kuhakikisha viwango hivi vya juu walivyo viweka kwenye mradi huu vinahifadhiwa au sisi kama madiwani wa Hip Hop hatutakuwa na budi kuwapiga chini kwenye uchaguzi mkuu wa Hip Hop utakapotokea pindi watakapotupatia miradi iliyo chini ya viwango.
Kazi kwenu Meya Tingu na Meya Tofa Tofali.
Kupata nakala yako wa mradi huu wasiliana na Tingu na Tofali kupitia mitandao ya kijamii :
Instagram: tofa_emcee
Facebook: Tingu Boy Newton
Naishi Na Hip Hop Mixtape

