TK Nendeze sio mwanamuziki wako wa kawaida. Japokua yupo kwenye tasnia ya muziki kwa muongo mmoja sasa, binafsi naweza kusema kua bado hajathaminiwa kama vile anavyo stahili. Inapokuja kwa uimbaji dada huyu ametubariki na sauti yake kupitia ngoma zake binafsi pamoja na kuingiza vocali zake kwenye ngoma za ma emcee kibao kama vile Nikki Mbishi, One The Incredible, Dizasta Vina, Veryl Mkali Wao, Joh Makini, Stereo Singa Singa, P Mawenge, D Maujanja na kadhalika.
Leo tunapiga gumzo na malkia wa RnB kutoka bongo mwenye maisha mia moja…
Karibu sana Micshariki Africa dada TK Nendeze. Tuanze kwa kukufahamu majina yako rasmi, unatokea wapi na unajishughulisha na nini?
Naitwa Tecla Kituli, ninatokea Dar es Salaam na ni mwanamuziki wa RnB.
Tueleze historia yako, ulizaliwa wapi, ulisomea wapi, mpo wangapi kwenu na umefikia wapi kimasomo? Utoto wako ulikuaje?
Nilizaliwa Dar, nimesoma Mbezi Beach High School na Tumaini University, Dar. Tupo watoto wa nne kwetu. Utoto wangu ulikuwa poa sana ukizingatia pia ni binti pekee so wazazi na kaka zangu walinipa good time sana.
Nimekua nikiona picha zako za TBT na video zako ulipokua ndio unaanza muziki wako. Tueleze kuhusu historia yako ya muziki, ulianzaje hizi shughuli za muziki?
Nilianza muziki mwaka 2003 chini ya label ya Backyard baada ya kushiriki mashindano ya kuimba, Pop Idol na kushika nafasi ya nne.

Ngoma yako ya kwanza ulifanikiwa kuirekodi lini, inaitwaje na je ulijiandikia mashairi yako au uliandikiwa? Wimbo huu ulipotoka mashabiki zako waliupokeaje?
Wimbo wa kwanza kuimba uliitwa Nipe Love nilimshirikisha Noorah. Haukufanya vizuri na honestly sijuagi kwa nini 🤣
Kwa wana Hip Hop wa handaki Tanzania, sauti yako inafahamika na kusifiwa na wengi sana, ila kwa maoni yangu kule mkondo mkuu naona kidogo kama hujapenya kihivyo. Tatizo ni nini, mbona iko hivi na je wewe mwenyewe hua unawaza kuhusu hili?
Nadhani mimi nina aina ya kipekee sana ya mashabiki zangu, na hao hao napenda sana nisiwaangushe. Endapo na kule wakinielewa itakuwa blessing sana ila sina mpango wa kubadilika.
Mapenzi yako na Utamaduni wa Hip Hop ulianzaje na umeathiri vipi muziki wako? Kwa wale wasiokufahamu waeleze vile wee ni mnona pia inapokuja kwa uchanaji na tupe baadhi ya ngoma ambazo umechana tu iwe ni mwanzo mwisho au hata beti moja?
Mimi nimelelewa kwenye mazingira ya Hip Hop nimesikilizishwa sana Hip Hop na kaka zangu. Childhood yangu ilikuwa fun sana. Na unoma wangu unatokana na Hip Hop! RnB Hip Hop na Soul ni mapacha watatu na huu muziki ni real sana.
Dada umefanya kazi kibao na ma emcee wengi Tanzania; Nikki Mbishi, Dizasta Vina, One The Incredible, P Mawenge, Mansu Li, Stereo Singa Singa, Joh Makini, Mex Cortez, D Maujanja na kadhalika...hebu tuongezee orodha kwani hatuwezi choka kujua mchango wako kwenye miradi ya wana Hip Hop. Je hii fursa na barka ya kufanya kazi na hawa wasanii unaizungumziaje?
Okay ... AY, FA, Inspector Haroun, Songa dah! Wako wengi sana! Ni blessing sana kufanya kazi na wana Hip Hop I consider them family.
Mbona hukuamua kua mchanaji moja kwa moja na kuwaachia wengine kuimba ili tuongeze idadi ya wachanaji wa kike kwenye game? Unahisi ni kwanini game la Hip Hop sio tu Tanzanai bali hata Africa Mashariki akina dada ni wachache? Nini kifanyike ili tuongeze akina dada zaidi sio tu kwenye nguzo ya uchanaji bali hata kwenye nguzo kama za DJ, Graffiti, Breakdance na kadhalika?
Mimi kuchana niliamini naweza na ni kweli naweza ila kuimba ndio hatari! Hahaha so kuna baadhi ya projects nimechana mfano cypher ya Valentines na wimbo wangu wa Kichochezi, A Letter To A Son And Daughter pia.Kuhusu DJ, Graffiti na vitu kama breackdance nadhani ni wengi wetu hatujaamua tu Ila ni fani poa sana coz wapo wadada nchi za wenzetu wanafanya poa, ni ushawishi tu na sisi kufanya maamuzi au kuthubutu coz huwezi kujua kama unaweza jambo fulani bila kujaribu kufanya.
Najua mpaka sasa una miradi kibao iwe ni singles, EP na album. Tueleze kuhusu kazi zako kuu, zinaitwaje, zilitoka lini na zinapatikana wapi?
Nina kazi kama The Playlist ilitoka mwaka jana. Ep ya Stimu mwaka juzi 2021 na sasa nina album ya A Hundred Lives. Nimetoa nyingine kama New Era ilifanya poa sana pia.
Pia umeachia album yako mpya A Hundred Lives. Mbona Miaka Mia? Pia album hii imesimamiwa na watayarishi gani na wasanii gani waalikwa wameshirikishwa kwenye mradi huu?
Album yangu imeshirikisha watu wengi sana nikiwa na maana sio wanamuziki tu mpaka producers. Pallah, Sigga, Cjamoker, Blaq Beats, Ommy Pah, Dj Super Fly ambaye ni kaka yangu kabisa wa kwanza ndio ma producer waliofanya album hii. Kaka yangu nayefuatana nae kuzaliwa ameandika almost 50 percent ya nyimbo. P Mawenge, One (The Incredible), Motra (The Future), Rosie M, The City, Elihekima, Nikki Wa Pili, na kaka yangu Ghannied ni baadhi ya walioshiriki humu kama artists.
Album hii pia uliizindua na kuifanyia Listening Party, mmoja wa wachache kuenda njia hii, kwanini? Sherehe yenyewe ilikuaje?
Idea ilikuwa ni ya Dotto Wa Maujanja kufanya hiyo event na kitu kizuri sana watu wakaipokea vizuri sana. Asante sana kwa Nyeke wa Watunza Misingi kwa kuendesha event nzima, the guy is a genius. Watu walistream Wimbo mmoja mmoja kwa madau yao. Na nikapata pesa nzuri tu.

Siku hizi tuko kidigitali, wee unaongeleaje usambazaji wa muziki kwa kupitia njia hii kwani naona pia hua unauza nakala zako kwa wateja wako moja kwa moja bado?
I find it easy tu. Sitaki kuongelea sana maana dah!
Umuhimu wa mradi huu kwako ni upi na je mashabiki watarajie nini kutoka kwa kazi hii?
Huu mradi pia uko very personal. Hii album nimeiita A Hundred Lives na sio a hundred years kwa sababu nataka iishi maisha au kwa vizazi na vizazi na sio kwa miaka tu kadhaa. Album ni kaliiiii sana, wanicheki tu kuipata.


Baada ya hapa mashabiki watarijie pengine matamasha na media tour kutoka kwako?
Yes nitafanya live events, videos na media tours…
Muziki wako hupata ushawishi kutokwa wapi ndio uanze kuandika ngoma? Na je mchakato wako wakuanda muziki ni upi?
Mimi naimba yale yanayotokea tu maishani. Ni mara chache sana naimba kuhusu maisha yangu. Nimekuwa influenced na watu kama Aaliyah, TLC, SWV na Lauryn Hill. Huwa naandikiwa maana saa zingine akili inaganda 😅.

Mwaka jana nilifurahi kuskia wana handaki wawili kutoka Kenya na Tanzania, tena akina dada wakifanya ngoma pamoja. Hapa nazungumzia ngoma yako na Veryl Mkali wao kwenye ngoma This Game inayopatikana kwenye album ya Black Ninja, Ilolo Confirmed. Hii collabo ilikujaje, mapokezi yalikuaje na jee mathara ya kazi hii kwenu nyie kama akina dada mlioweza kufanya kazi hii ni ipi?
Nilitambulishwa Veryl na Black Ninja. Nilifurahi sana maana nilikuwa nawish sana nipate collabo nyingi na wadada. Na vile Veryl ni Mkali nikaona safi sana.
Tutarajie nini kutoka kwako baada ya A Hundred Lives, music videos, more songs, collabos?
Yeah video tatu, more collabos na album nyingine August (2023). Hamna kupoa.
Shukran zako zinaenda kwa akina nani?
Sifa na utukufu kwa mwenyezi Mungu. Napenda kuwashukuru sana familia yangu, yaani wazazi wangu na kaka zangu kwa kunilea kimisingi sana. Napenda kuwashukuru my diehard fans sana. Lastly but not least Dotto wa Maujanja kwa kila namna anayo ni encourage niweze kusonga mbele.
Wapi unapatikana kwenye mitandao ya kijamii?
Facebook: TK Nendeze
Instagram: TK Nendeze
TikTok: TK Nendeze
Audiomack: TK Nendeze
YouTube: TK Nendeze
Neno la mwisho?
Neno la mwisho, "Acha upendo utuongoze daima!"
Shukran sana kwa mda wako dada TK Nendeze, nakuita Mary J. Blige wa Tanzania!
It is Maaaaary! 🤣🤣 Asante sana kaka kwa muda wako pia. Endelea kubarikiwa. Umekuwa ukipush sana kazi zetu. Asante sana kwa upendo.