Uchambuzi Wa Album: Ma Li Za Ro Ho (1NE)
Emcee: Trabolee x Akili Blaq
Tarehe iliyotoka: 04.03.2022
Nyimbo: 12
Mtayarishaji, Mixing & Mastering: Akili Blaq
Studio: DextRaw Africa

Nyimbo Nilizozipenda: We 1Ne, Rangi Zingine, Ma Li Za Ro Ho, Radiate, Sahau Shida, Hertz, Si Kioo La Tatu, Rafiki Pesa, The Healing, My Time, Born 2 Fight, Hii Spark

Trabolee ambaye jina lake kwa urefu ni “Truth Reigns Above But Only Love Exists Eternally” ambayo kwa tafsiri ya Kiswahili ni “Ukweli Unatawala Juu Lakini Upendo Pekee Upo Milele”. Trabolee mwenyewe hupenda kufupisha jina lake na kujiita “Tra” hajioni kama mchanaji tu bali anajiona kama sanaa (Art). Hivyo basi Tra ni Art.

Emcee huyu anayetokea kule Nakuru Kenya ni mpiga kazi na hili unaliona wazi kwani amefanikiwa kuachia albums kadhaa; THC (2013), Occult Lore (2013), All Roads Lead Home (2015), Telos, Preaching To The Converted (2018). Pia ameachia EP kadhaa kama vile SADFA (2020), Safari (2021) pamoja na singles kibao. Pia Trabolee amebobea inapokuja kwa maswala ya mtindo huru na amewahi kuwa mshindi wa Aarban Cypher.

Trabolee

Akili Blaq naye ni mtayarishaji mbunifu aliyebobea kwenye upande wa uandaaji sauti zenye midundo mingi, ambaye ana ustadi wa maumbo, hila na mipangilio ya kitanzi isiyotarajiwa. Mbinu yake isiyo ya mstari (minimalist) imeingizwa kwa uzuri katika msururu wa Snappylilbits, sampuli ya haraka-haraka mkusanyiko wa midundo na nyimbo zilizotawanyika na vipengele vya muziki kutoka kwa washirika wa karibu na marafiki. Kwa kuongezea, DNE yake inachanganyika kudokeza wasanii wengine wa muziki ambao yeye huchota, anafurahia au anachochewa nao. Hivyo basi midundo yake inatokea tofauti na midundo uliyozoea kuiskia.

Akili Blaq

Mapema mwaka huu wawili hawa ambao walishawahi kufanya kazi pamoja (SADFA) waliungana tena na kutupatia album yao Ma Li Za Ro Ho (1NE).

Kama utangulizi ulivyosema juu ya wawili hawa kila mtu anafanya kitu chake tofauti na tulivyozoea. Hivyo basi Ma Li Za Ro Ho (1NE) ipo kitofauti mwanzo mwisho sio tu kwa upande wa midundo bali hata kwa uchanaji.

Nilisoma sehemu flani shabiki wa Trabolee alithubutu kulinganisha ubunifu wa kitofauti wa Trabolee ni kama ule wa marehemu MF DOOM na kuwa usipochunga maana ya mashairi yake yatakupita. Mimi naongezea pia kuwa Trabolee kama vile Aesop Rock sio kikombe cha chai cha kila mtu (nimetafsiri moja kwa moja toka kingereza “not everybody’s cup of tea”).

Wimbo wa kwanza toka kwa mradi huu ambao uliachiwa rasmi kama single ya kwanza Hii Spark unakuonesha moja kwa moja nini utarajie toka kwa mradi huu. Kwenye mdundo unaskia filimbi zinapiga na ndege wakiitana taratibu kabla ya emcee Trabolee kuanza kuchana. Wimbo huu ndio cheche(spark) inayowasha moto unaohakikisha mradi wote ni moto.

Mradi unaingia taratibu sana kwenye ngoma ya pili We 1ne akiwa na Xylo ambapo unaona vile wawili hawa wanavyochanganya ubunifu wao, kimistari na pia pale Akili Blaq anawakilisha vyema kwenye midundo. Xylo nae anampa support Trabolee kama backup singer.

Single ya pili toka kwa mradi huu ambayo imepikwa ikapikika ni Rangi Zingine. Trabolee anachana kuhusu umuhimu wa kuthamini ngozi yetu nyeusi na Akili nae anakupatia mdundo unaokufanya ujihisi fahari kuwa mtu mweusi. Nondo zinatemwa hapa si mchezo akisema,

“What now?/
Black in heaven/
Black is God/
Black is Rhythm/
Black is Power/
Blacker than where I came from/
Blacker than where I’m going/
Black in not the absence of light/
Black is all the light combined/

Hizo Rangi Zingine wacha…

Mradi unaendelea na wimbo mzuka pia Radiate ambao umeundwa ki design flani unaweza chezesha mwili wako mzima na sio kichwa tu kabla ya speed kushuka kidogo kwenye wimbo chanya sana pia ambao umebeba jina la album Ma Li Za Ro Ho. Wimbo huu una double entendre flani unaonuia kuonesha mali ziwe za roho ila mali hizi pia zina uwezo wa kumaliza(ua) roho yako. Akili Blaq kaanda mdundo flani mzuka sana.

Sahau Shida unaendeleza ubunifu na utukutu wa uthubutu wa hawa jamaa wakimshirikisha emcee Leo Coltrane kutoka Brooklyn, America ambaye kaja na nondo zake pia. Ngoma chanya ambapo Tra anachana mistari ya kiujanja akisema, “Patieni Tra kazi/Lisheni bar addicts/” kama anavyo kuambia pia kwenye My Time akiwa na TLS,

“Hizi bars zinaweza amsha kesha/
Mkini gas manze mnanichekesha/
Juu mi ni bash na natafuta pesa/
Nipe ma bars zile Bobs za Nesta/”

Pia kwenye Hertz unaona jinsi Trabolee anaweza kuchukua vitu vidogo na kufanya uone impact yake kama vile akisema,

“Still I tip them over with pivotal facts/
You tweeted umeomoka/
Now you got to pay digital tax/”

Kwa wale wenye tabia za kuweka hadharani maisha yao KRA wanawaona na watajia cha kaisari. Ngoma yote ni madini kwenye mdundo unaopiga taratibu; vinanda, na ngoma pia. Safi sana.

Ngoma nyingine ambayo niliyoipenda ni Si Kioo La Taa Tu akiwa na dada Ach13ng’ ambapo anacheza na maneno kama kawa kutupatia kitu cha maana na kitamu. Kisha tunaenda Born 2 Fight ambapo sasa mtayarishaji Akili Blaq anaamua kuingia booth na kuchana pia. Baraka sana.

Rafiki Pesa ni wimbo chanya pia unaongelea pesa, uzuri wake, jinsi ya kuzitumia vizuri , jinsi zinaweza kukuharibu, jinsi unaweza zikuza na vile huwa tunaweza hangaika wakati tunazihitaji ila hazipatikani. Wimbo mzuri sana juu ya mdundo mzuri pia.

The Healing ndio wimbo ambao unatamatisha mradi huu mzuka sana. Kusema kweli jamaa wanatuacha tukiwa matawi ya juu na wimbo huu ambao unaongelea maswala ya kujitibu sio tu kiafya bali kiakili, kimwili, kimawazo, ki dini, kimaamuzi…

“Healing ya ma sufferer/
Na healing ya mblein/”

Trabolee na Akili Blaq ni vichwa viwili makini sana inapokuja kwenye maswala ya uchanaji (TRA) na uandaaji midundo (AB) na hapa wameshirikiana na kutupatia mradi wa kudumu sana Ma Li Za Ro Ho (1NE). Hip Hop ipo kwenye mikono mizuri na tumebahatika kuwaona wawili hawa wakiwajibika kuiweka Hip Hop ya Africa kwenye ramani ya dunia.

Wafuate wawili hawa kwenye mitandao ya kijamii;

Instagram: trabolee
Instagram: akiliblaq