Uchambuzi Wa Mixtape: Nipo Njiani The Mixtape
Emcee: Trickson Knowledge
Tarehe iliyotoka:  08.08.2021
Nyimbo: 10
Mtayarishaji, Mixing & Mastering: Black Ninja
Studio: Boom Bap Clinic

Nyimbo Nilizozipenda: Sema Nao, Usiondoke, Asante, Nipo Njiani, Juu, Mitambao, Ndotoni, I Am A Professional, Tofauti,

Trickson Knowledge - Mwanaupeo

Mwana wa Geita aliyejikita Mbeya Trickson Knowledge (Mwanaupeo) mwaka jana alikuja na mradi wake Nipo Njiani The Mixtape. Nimekuwa nikisema nitakuja andika kuhusu hii kazi kwa muda sasa kumpa shavu mwana na leo muda umewadia.

Mixtape hii, uzuri wake ni kuwa unaweza tafuta midundo mizuri ya ma emcee wengi na ukachana juu yake ila bado ukijitoa asilimia mia kama kwa mradi huu na penseli yako ikatulia basi mtu anaweza dhania anaskia album. Na hili ndilo unaliona kwenye kazi hii ya ngosha.

Mradi unaanza na wimbo Sema Nao ambapo emcee huyu anaanza kwa kujitambulisha,

"Kila chenye mwanzo kina mwisho ndio maana penye uhai pana kifo/
Jema na baya kuna malipo/
Sio simple kuwa juu hapa kuna na nafuu naongozwa na Mungu Mkuu still rap Bishop/
Trickson na flow bila wasi/
maridadi ka mwili kadogo sauti hii ni soo kama radi/
Kasirika mbogo niku shoot kwa risasi/
Mwanaupeo logo ipeni muda ipande chati/”

Mdundo uliotumika hapa ni wa Bishop Lamont, First They Love You ulioundwa na 9th Wonder.

Baada ya hapa emcee huyu anagusa mada ya mahusiano kwenye Usiondoke anapomsihi mrembo wake asimuache na ninachokipenda kwenye wimbo huu kama kwenye nyimbo zote kwenye mradi huu ni mashairi yalivyoandikwa kwa urahisi na kuchanwa freshi neno kwa neno pamoja na unataji wa mdundo.

Asante pia inagusia freshi mada ya mahusiano akiendelea pale alipoachia kwenye usiondoke akisema,

“Nilikwambia usiondoke baby ulinisikiliza/
Ikabidi niokoke nipinge nguvu za giza/
Nimwamini Allah pia nimwamini Jesus/
Nakupenda mpaka nimepitiliza/”

Nyimbo hizi mbili zimeendana freshi kabisa na mdundo uliotumika safari hii ulikuwa wa MC David J, NewLove.

Nipo Njiani ndio wimbo uliobeba jina la album na uligonga vi noma sana kwenye speaker zangu. Kwa kupitia ubeti mmoja emcee huyu bado anaendelea kuongea na mrembo akimwambia amsubiri kwani yupo njiani kutoka anapotoka lakini hataki tena mahusiano naye kwani taarifa zilizomfikia ni kuwa ashakuwa mdangaji.

Kwenye mdundo wa Young Roddy, Russian Roulette emcee Mwanaupeo anarudi tena Juu akisema,

“Mi napanda juu we ningoje chini utasanda tu/
Unangoja nashuka lini huku nimepanga rumu/
Juu ni raha ndio maana walio hawashuki/
Hata shida zenu hawakumbuki/
Hawashtuki hawainuki walio juu huwa hawajuti/
Wanahisi kuwa chini ni umauti madhubuti tubutu/
Hao chini huwakuti ndio sababu wakishuka juu wanarudi nduki/”

Ubeti mmoja nondo tupu mwanzo mwisho.

Mitambao ndio ya pili iliyowahi kutoka kwenye mradi ambapo emcee huyu kashirikisha ma emcee Nicksome Mo, Rabi James na Black Fire ambapo kila emcee amewakilisha freshi. Mdundo huu uliundwa na Black Ninja. Kwenye wimbo huu Trickson Knowledge anatoa shout out kwa alipotokea akisema, “Nyumbani Geita so usiulize where this rapper from? /” Katupa shavu wana Geita na sisi tumempa shavu Micshariki Africa.

Ndotoni wimbo unaofuatia ni wimbo unaosimulia hadithi flani ya yanki flani ambaye aliona kapata ngekewa pale alipo tongozwa na shangingi flani kumbe kwa bahati mbaya au nzuri jamaa alikuwa anaota, aisee, jamaa hakupiga kama Mheshimiwa Temba kwenye Nampenda Yeye!

Baada ya hapa emcee anadandia mdundo wa The Alchemist – Genesis & Omega kwenye Deep Flow kabla ya kuchana kwenye mdundo classic wa Duke Tachez kwenye wimbo wa Fid Q ambao pia kama huu wa emcee Trickson Knowledge unaitwa I Am Professional. Trickson anajitahidi kuua na kwenda toe to toe na Fid Q na kusema kweli anajitahidi akisema,

“Huwezi compare na mimi sipo fair mi nasogea juu nawashusha chini/
Ngoma ilipigwa na Duke ndani vesi za Fid sasa vesi zangu mimi/
Wote wa Mwanza Mwanza kabla Geita haijawa mkoa sasa Geita ndio nyumbani and/
Najipanga kwa hi stanza marida Geita kwenye ramani /”

Tofauti akiwa na X Ray Vina ndio ngoma inayotufungia mradi. Ngoma mzuka sana mdundo wa Black Ninja ambapo wawili hawa wanatupatia madini kuhusu vile watu wawili kila siku wapo tofauti.

Emcee Trickson Knowledge kupitia kandamseto hii Nipo Njiani Mixtape ametuaminisha kwamba siku ile akiwasili na album yake rasmi tutamkubali na kumlaki vyema. Tunakusubiria Trickson Knowledge, Mwanaupeo.

Mfuate Trickson Knowledge kwenye mitandao ya kijamii;

Facebook: Trickson Knowledge
Instagram: trickson_knowledge
Twitter: trick_knowledge