Uchambuzi wa EP: Ndumbuli
Emcee: Trump Mc (Teacher wa Rap Ushairi Midondoko na Punch)
Tarehe iliyotoka: 27.02.2022
Nyimbo; 7
Watayarishaji: Black Ninja, Kise P, Kingu Master, Wise Genius
Studio:BBC, AMG Records, Kinasa Records

Nyimbo Nilizozipenda: Mapambano, Tambo

Tarehe 27 mwezi wa pili mwaka 2022 ndio mradi wa Ndumbuli umeingia sokoni rasmi.

Ndumbuli EP ni jina lililobeba mradi toka kwa Teacher wa Rap Ushairi Midondoko na Punch fupisha muite Trump Mc. Mwezi huu wa pili wengi hujua ni mwezi wa wapendanao ila Teacher wa Rap Ushairi Midondoko na Punch anakukumbusha kuwa huu ni mwezi wenye maana kubwa kwenye Hip Hop ndio maana kakupatia Ndumbuli EP kama zawadi kwako shabiki, mfuasi na kila mwanautamaduni wa Hip Hop.

Mradi huu wa Ndumbuli umewashirikisha emcees watano (5) Mbize Mc, Kay wa Mapacha, Nikki Mbishi, Rabi James pamoja na Al Beez. Ndumbuli Ep ina jumla ya nyimbo 7.

  1. Intro Beberu la Mbegu
  2. Sitabiriki ft Mbize Mc
  3. Ngebe ft Kay wa Mapacha
  4. Inbox ft Nikki Mbishi
  5. Mapambano ft Rabi James
  6. Makasiriko ft Albeez
  7. Tambo
  8. Ndumbuli ft Nikki Mbishi 

Watayarishaji waliotengeneza huu mradi ni watatu, Black Ninja(BBC), Kise P, Kingu Master bila kumsahau Wise Genius.

Kwenye hii Ep ya Ndumbuli nimepata nafasi ya kuzungumza na Trump kuhusu nyimbo za hii Ep na kufahamu lengo kuu la mradi huu ni nini kwa jamii nzima inayomzunguka na kumpa thamani ya juu ya Teacher wa Rap Ushairi Midondoko na Punch.

Trump MC

Trump hebu tuzungumzie kuhusu hii Ndumbuli EP kabla ya kupitia wimbo mmoja baada ya mmoja, hebu tuambie Ndumbuli ni EP ya namna gani na kuna nini ambacho kinaweza kumshawishi mtu kuinunua na kusikiliza kilichomo?

Ndumbuli ni EP inayozungumzia mambo mbalimbali yanayoizunguka jamii. Ndumbuli ni nyumbani Ifakara ninapotokea mimi. So katika Ep hii nimejaribu kuzungumzia maisha ya jamii inayoishi kijijini na mjini. Kinachoweza kumshawishi mtu kununua EP yangu ni kwamba nimejitahidi kuandika ujumbe tu kwenye nyimbo zote. Kwa hiyo kila wimbo atakaosikiliza mtu atakuwa anatoka na kitu kikubwa sana. Nimejitahidi kuelimisha jamii kupitia EP hii,sio ya kukosa.

Tutegemee kupata kitu gani kwenye hii EP yako ambayo umeingiza sokoni kwa sasa? Na hii ni EP yako ya ngapi toka umeingia kwenye utamaduni wa Hip Hop?

Mtegemee kupata vitu vingi sana ambavyo hamjawahi kukutana navyo kwenye nyimbo nyingine za watu wengine. Ndumbuli ni EP yangu ya kwanza. Sikuwa katika mipango ya kuachia EP ila baada ya mashabiki na producers kuona uwezo wangu wakanishawishi kuandaa EP. Ni watu wengi ila mtu kama Palla Midundo, Maujanja Saplayaz, Beberu la Mbegu, Iddy Mwanaharamu, Logic (Mantiki) ni baadhi tu ya watu walionishawishi, ila ni wengi sana kutaja wote hapa ni ngumu.

Naomba kuwafahamu watengenezaji wa huu mradi na emcees ambao umeshirikiana nao katika nyimbo zako na kwa nini uliwachagua hao kuandaa hii kazi yako ya kwanza ambayo unaingiza sokoni?

Waandaji wa mradi huu ni Blackninja,Wise G, Kise P na Kingu Master. Ma emcee nilioshirikiana nao kwenye EP hii ni Nikki Mbishi, Rabi James, Kay wa Mapacha, Mbize MC na Albeez. Nimechagua wachache sababu ngoma ni chache, kwenye Album watakuwa wengi zaidi.

Ndumbuli imebeba nyimbo 7 naomba tuanze na huu wimbo wa Makasiriko, kitu gani kilikusukuma kuandika huu wimbo na pia unahisi jamii itapata elimu gani kupitia mashairi yako kwenye huu wimbo?

Yeah, Jamii itapata elimu kubwa sana. Sababu nimeelezea sio kila atakayekuudhi umlipe kisasi, na pia katika huo wimbo nimemshirikisha Albeez naye ameelezea makasiriko ya kijijini. So kuna kitu kikubwa jamii itajifunza. Kitu kilichonisukuma ni kutaka jamii ijue kuwa kila kasiriko lina suluhisho lake.

Tuzungumzie pia wimbo wa Sitabiriki kwa nini umeandika huu wimbo au kuna watu unawaonesha jinsi gani ulivyo upande wa kushika Mic na uwezo wako ulivyo kwenye handaki au ni wazo lilikuja tu ukachorea mistari?

Niliandika wimbo huu kuonesha watu kwamba mimi huwezi kunitabiri, kila pande nipo. Unaweza kuniwazia huku kumbe mimi nipo kule.

Mapambano naona ni moja ya wimbo mkali kwa upande wangu, wazo la huu wimbo limetokana na nini? Naona mashairi yanasisitiza vijana kujivunia kwao na kuwapa sifa viongozi waliopo kwa mazuri wanayotenda.

Wimbo huu unazungumzia zaidi kukumbuka tulipotoka, tusaidie mapambano ya maendeleo ya tulipotoka. So nimesisitiza viongozi wapambane kuleta maendeleo na wananchi tunawaunge mkono na kushiriki nao shughuli mbalimbali.

Wimbo wa Tambo nao ni moto sana umejitamba na kuyapa sifa machata yetu. Ndani ya wimbo wa tambo umezungumza mengi sana je jamii inapata elimu gani kwa huu wimbo?

Nimezungumzia mengi, unaweza kujitamba kisha ukaishia pabaya, kama nilivyosema

 "Tambo za kuku zinafichwa na mwewe".

Kwahiyo nimetamba kona zote.

Ngebe inafanya nione hii Ep ni kama tamthilia inayohusu Ndumbuli, ilikuaje ukaandika huu wimbo au kuna tukio ulikutana nalo chaka ulipoenda au ni raia wa mjini walijua ukienda chaka unapotea kimaisha?

Nimekutana na matukio mjini na kijijini, watu wana ngebe(Kebehi) sana. Nimejaribu kuwaelekeza kuwa taarifa zao nimepata na waache ngebe.

Wimbo Inbox jina la wimbo linaweza kufanya watu wakajua unazungumzia inbox za mitandao ya kijamii lakini mwisho wa beti unasema inbox ni wewe. Kwa nini wewe ukawa inbox?

Nimezungumzia Inbox ni mimi sababu inbox yako unaimiliki wewe mwenyewe. So taarifa zinabaki kwako tu.

Tunamaliza na wimbo uliobeba jina la mradi huu Ndumbuli, Ndumbuli ni wapi au ni nini? Kitu gani cha kipekee kinapatikana Ndumbuli ambacho mtu akiona anajua hii ni Ndumbuli chata?

Ndumbuli ni kijijjini ninapotokea. Mimi ni mwenyeji wa Ifakara-Lipangalala Ndumbuli. Huu wimbo nimezungumzia mazingira ya Ndumbuli ambapo ni nyumbani. Hata meya wa mji wa Ifakara anatokea Ndumbuli, vipaji vingi vya mpira wa miguu, uongozi na vipaji vingine vimejaa, wachezaji kama vile Aziz Hunter, Monja Liseki, Tom Karume, Casto Liseki, kuna dogo anaitwa Lupekenya anacheza sasa ligi ya Zanzibar na wengine wengi wanatokea Ifakara. Kuna vipaji vingi sana. Huyo dogo Bright naye anatokea Ndumbuli tena ni jirani. So Ndumbuli ni noma. Alama ya Ndumbuli ukiona mwana anapenda sana samaki, maji baridi na wali ujue anatokea Ndumbuli.

Tutegemee kitu gani kitafuatia toka kwako baada ya hii EP kuingia sokoni?

Album ambayo itakuwa na ngoma nyingi sana na nitashirikisha wasanii wengi sana sababu napenda ushirikiano sana na ndo maana hata jina langu linaakisi hiyo kitu. Ukiacha ile Teacher wa Rap Ushairi Midondoko na Punch pia TRUMP=Tengeneza Raia Upate Maisha Popote. Naomba support yenu kwenye Ep yangu na Album inayokuja.

Note: Mameneja wangu ni Beberu la Mbegu(Don Dee Dion) na Iddy Mwanaharamu.

Je mtu akitaka kupata hii EP na kazi zako zingine zilizotangulia anazipata kwa njia gani?

Hii Ep bei yake ni Tsh.5000/= ila unaruhusiwa kulipia zaidi ya kiasi hicho. Ngoma zangu zingine zipo Audiomack, Mdundo na YouTube. Ukiandika Trump Mc(Mfalanyombo) utapata ngoma zangu zote.

Mtu akitaka kukupata mtandaoni anakupata kwa njia gani (majina gani)?

Facebook: Moses Mfalanyombo
Instagram: mfalamoses
Twitter: mfalamoses1

Asante kwa mda wako Teacher wa Rap Ushairi Midondoko na Punch.