Mitaa Na Sanaa

Mitaa Na Sanaa ni moja kati ya majukwaa ambayo yanaendeleza harakati za hip hop (handaki) kwa mkoa wa Mwanza. Leo tumepata nafasi ya kuzungumza na mmoja wa waanzilishi wake anayefahamika kwa jina la Yona Poppa Mwandenuka. Tutapata nafasi ya kumfahamu yeye ni nani na jukwaa la Mitaa Na Sanaa linafanya nini kwenye harakati za huu utamaduni.

Karibu katika jukwaa la Micshariki Africa, ingekuwa vyema kama ungeanza kwa kutuambia jina lako halisi na ni lini ulianza kupenda utamaduni wa Hip Hop?

Jina langu halisi najulikana kama Yona Ally Mwandenuka. Utamaduni wa Hip Hop nilianza kuupenda zamani kidogo miaka ya 2001. Nilikua napenda kusikiliza na kuimba nyimbo za Mr 2 (Sugu) kiasi  mtaani watu wakaanza kuniita Sugu .Ila miaka ya 2006 ndio nikatokea kuupenda zaidi huu utamaduni wa Hip Hop.

Mbona waitwa au wajiita Big Poppa?

Hii ni a.k.a tu ambayo nilianza kuitumia mwaka 2010 baada ya kuwa namsikiliza na kumpenda msanii wa Hip Hop Notorious B.I.G, Biggie Smalls.

Yona Ally Mwandenuka

Tukiachana na Sugu (Mr 2), je ni emcee gani wa ndani au wa nje ya nchi aliyefanya ukazidi kuona Hip Hop kwako ni kitu sahihi kukiendeleza?

Hapo alikuepo emcee Raff G a.k.a Father Nelly(R.I.P). Wimbo wake wa Nini Dhambi pia alinifanya nipende Hip Hop.

Asili yako ni wapi na unawakilisha mkoa gani? Na katika utamaduni wa Hip Hop unasimama upande gani? Emcee, dj, graffiti au nguzo ipi?

Asili yangu mimi ni kusini mkoa wa Mbeya wilaya ya Rungwe…ila kwa sasa naishi Mwanza nikiwa huku nawakilisha kundi la Wasadikaya. Ila pia kwa Mwanza ni muongozaj na muhamasishaji wa kundi la mitaa na sanaa . Pia nasimama katika nguzo ya knowledge (noleji) naweza sema hivyo maana kazi yangu katika jukwaa la mitaa na sanaa ni host wa jukwaa.

Toka 2006 mpaka sasa je kuna wimbo au album ambayo usharekodi hata moja ili mitaa ipate kile ambacho unaamini kitaweza kuwapa elimu?

Hapana ila kwa kitu ambacho naweza sema nimekifanya kwa kipindi hicho chote ni kuwashawishi na kuwavuta watu kutoka kwenye fikra zao na kuanza rasmi kuijua na kuipenda Hip Hop. Pia nimeweza kuwalipia baadhi ya ma emcee studio na kuweza kurekodi nyimbo zao na kutoa elimu kwa jamii inayotuzunguka na ile ya mbali na tulipo maana mziki ni sauti kubwa na nyepesi kusikika kwa kila mtu.

Kitu gani kwa Mwanza kilikusukuma ukaamua kuanzisha Mitaa Na Sanaa na kutoendeleza Wasadikaya harakati za kundi lenu?

Wasadikaya ipo na inaendelea pia ni kundi ambalo linapatikana kusini na limezaliwa huko. Na sisi ni wawakilishi wake tulioko mikoa mingine hapa Tanzania. Kilicho nifanya nikae na crew yangu kuanzisha kitu kama Mitaa na Sanaa ni upendo wa kuupenda utamaduni wa Hip Hop. Pia  nilipoona Mwanza kuna vipaji ila mziki wa Hip Hop ulikua umelala ndio nikafanya hivyo ili kuwakumbusha na kuwastua watu kua Mwanza Hip Hop ipo na inaweza kuwepo kila wakati.

Kwanini uliamua ku support sanaa ya utamaduni wa Hip Hop na sio kitu kingine? Kwako Hip Hop ni nini kuliko sanaa zingine?

Niliamua ku support sanaa ya utamaduni wa Hip Hop sababu naupenda na sioni kama napoteza mda ku support Hip Hop.

Malengo ya Mitaa, Sanaa na Kilinge ni yapi? Je mnayafanikisha kila mara kunapokuwepo tukio?

Lengo kuu ni kuinua vipaji vya vijana kama katiba yetu inavyo sema, pia ni kutoa elimu juu ya utumiaji wa madawa ya kulevya, upotoshaji wa jamii na mambo mengi ambayo katika jamii hayafai ni lengo letu sisi kuyakemea na kuyafuta kabisa katika jamii. Pia hatuwasahau watoto wa mitaani kwani wao pia wana vipaji, ambao tukikaa nao toka saa nane hadi saa moja, kwa masaa matano au sita hayo basi kama alikua ni mwizi basi mtaa unapona. Lengo letu ni kukomesha vitendo vya kihalifu

Kuna utofauti upi ambao unaona upo kwa sasa kati ya kundi lako la kwanza Wasadikaya na ili la sasa Mitaa Na Sanaa?

Hakuna tofauti sana maana wote tunafanya kitu kimoja, Hip Hop . Tofauti ni mikoa na majina tu.

Kabla ya Mitaa na Sanaa, Mwanza kulikuwepo na movement zingine za Hip Hop kama Gogo Vinu na kadhalika. je umejipanga vipi kulinda hii movement yako idumu mda mrefu tofauti na zilizotangulia?

Yah ni kweli zilikuwepo na zikafa. Mipango yangu ya kulinda Mitaa Na Sanaa isife ni mipango mikakati ya kamati yangu. Pia najitahidi kujifunza na kufikiria wenzangu walianguka wapi ili mimi nisije kuanguka pia.

Support yako juu ya kuwalipia ma emcee studio na kuandaa onesho la Mitaa Na Sanaa je kuna faida ya kipato unayopata au ndio una support sababu unapenda huu utamaduni?

Kwa sasa bado sijapata faida yoyote maana tunatakiwa kuonesha kipaji kwanza ndio tuwaze mchongo. Lakini lengo kamili ni kufaidika pia. Kwa sasa tunaweka nguvu katika ku support ila pale watu na wadau wakielewa najua faida zitaanza kuja zenyewe.

Mpaka sasa ushasaidia emcee wangapi kuingia studio na wangapi wameshatoa Ep au albam?

Mpka sasa nimesaidia emcees wawili na nyimbo ambazo ni singo zipo. Pia kuna cypher kama mbili ambazo hazijaachiwa. Kwa sasa kuna uandaaji wa Ep ulianza mwisho wa mwezi wa 9 mpaka sasa ngoma kama tatu zipo tayari na tunaendelea kufanya zingine.

Unaweza kutusaidia EP zitakamilika baada ya mda gani ili mtu anayetaka kununua ajiandae na malipo(gharama) yake ipoje kama itatoka?

Kukamilika itakua ni mwezi wa 12 mpaka wa 1 mwakani. Na kuhusu bei siwezi elezea maana mara nying huwa naweza panga kutokana na ugumu wa ufanyaji kazi.

Tukitoa kuwasaidia emcees kuingia studio ni kitu gani kingine ambacho Mitaa Na Sanaa mnafanya?

Mitaa na sanaa tunafanya miradi  ya ndani kama biashara za t-shirt na uchoraj wa picha(graffiti).

Chata la Mitaa Na Sanaa

Kwanini ulichagua kufanya unachokifanya sasa na sio kuwa mchanaji au Dj?

Katika maisha si wote tufanane au sio wote tufanye kitu kimoja lazima tugawane majukumu ili tusonge. Ndio maana mimi nikawa muhamasishaji ili wengine wasonge kwa hamasa zangu. Na wao ni ma emcee ila hawawezi kwenda bila kuhamasishwa. Kwa hiyo  naona hiki kitengo Mungu kanipatia kina maana sana kwangu na huu utamaduni.

Unaitazama wapi underground Hip Hop ya Mwanza, Tanzania na Afrika mashariki baada ya miaka mitano kupita?

Baada ya miaka mitano underground Hip Hop itakuwa mbali sana kwa sababu Hip Hop ya handaki  imekua wazi na imetengeneza ufamilia tofauti na zamani. Kulikua na kujitenga sana pia ukanda mwingi; wa huku ni huku wa huko ni huko ila sasa familia imekua moja kwa ushikamano wa hivi. Ndani ya miaka hiyo isemwayo tutakua mahali pa juu.

Taswira ya jamii ya watu wa Mwanza wanaichukuliaje movement yako ya mitaa na sanaa?

Wameipokea kwa mikono miwili. Kuanzia wananchi mpaka viongozi wanatoa pongezi kwa vijana. Maana muitikio kutoka sehem mbal mbali unaonekana.

Je akitokea mtu mwingine akataka kuanzisha movement kama yako utampa ushauri gani kabla ya kuanzisha?

Yah nipo tayari maana sisi ni watu tunaosafiri kwenye mtumbwi mmoja iweje tuanze kugawana mbao saa hizi. Kwa hiyo nipo tayari kumshauri na kumpa miongozo itakapobidi.

Vikwazo gani unavyokutana navyo katika harakati zako za Mitaa Na Sanaa kwa hapo Mwanza?

Vikwazo ni pesa tu.

Tutegemee nini cha tofauti kutoka kwako na Mitaa Na Sanaa?

Kitu cha tofauti mnachotakiwa kutegemea ni ngoma kali na back to back za ngoma. Pia na online Tv ambayo itakuwa na vipindi vya kupiga story na ma emcee wa mitaa yote ya Mwanza na nje ya Mwanza ikibidi mpaka Afrika Mashariki.

Mbona umeamua kufanya tukio hili mtaani na sio pengine ukumbini?

 Mitaa ndio inahitaji elimu hii. Ukumbini watakaoweza kufika ni wenye kipato tu . Hii ndio sababu ya kufanya onesho la wazi  ii mwenye nacho na asiye nacho aweze kufaidika.

 Tukio la Mitaa Na Sanaa lilianza mwaka gani?

 Tukio hili lilianza rasmi mwaka 2019 mwishoni tukaenda nayo vyema hadi 2020 ambapo kuna mchanganyiko ukatokea tuka stop tukio. Baadae tukatafuta watu ambao tuna real love na Hip Hop ikabidi tuinuke tena. Kama unavyojua katika maisha kuna kugombana na kufanya nini na kuna watu hawaelewi wanachokifanya. Mwaka 2021 mwezi wa kwanza tukaanza na tukio tena na kukimbizana nayo mpaka sasa. Kwa hiyo tunaweza sema tukio mpaka sasa lina miaka miwili na nusu.

Hua linafanyika wapi na kila baada ya mda gani? Pia tukio linafanyika sana ngapi hadi saa ngapi?

Hua linafanyika mitaa ya Kirumba, Mwanza karibu na kituo cha polisi kushoto kuna shule ya msingi kuna eneo la wazi tunalo liita Shock Absorber na hua linaanza saa nane hadi saa moja jioni.

Unahamasishaje watu kujua kuhusu tukio hili na kuhakikisha mahudhurio ni mazuri?
Je kuna wafadhili wanao wa support?

Tunahamasisha watu kwa kuhudhuria kilingeni kwetu kwa njia ya posters zinazotoka siku 5 an 4 kabla ya tukio. Pia tuna share kwa ma group ya WhatsApp ili watu wajue kinachoendelea kuhusu tukio letu.

Kwa upande wa ufadhili hatuna anayetufadhili kwa sasa ila tushawahi kuwa nao kitambo ila hawakuwa stable kwani wao kwa wakati ule walikuwa wanajaribu pia.

Ni nini kifanyike ili wana Hip Hop waweze kuwa na matamasha makubwa ya kujitegemea au hata ya pamoja?

Kitu cha kufanya ili tuweze kufanya matamasha makubwa ya Hip Hop mimi nadhani ni kupata wafadhili waliotulia na walio simama katika misingi. Mfadhili akielewa ni nini tunachokifanya nina imani tunaweza tukafanya matamasha makubwa na kwenye kumbi kubwa na hivyo basi hata kulipa mlangoni watu watalipa.

Pili mimi ninavyoona ni kuweka juhudi na kutoa kitu kizuri ili tutakapoweza kushawishi watu kuja sehemu wakiamini kwa kile tunachokifanya na waje kwa moyo mmoja.

Mwisho kabisa unauzungumziaje uimara wa handaki ya bongo na mapungufu yake? Je nini kifanyike kuweza kuyapunguza hayo mapungufu au kuyamaliza kabisa?

Kwa uimara wa handaki uzidi kuimarika tu na kushikilia kwa nguvu zote maana ndio tunaelekea nchi ya ahadi yenye matunda na kuheshimika... mapungufu ni machache sana  na yanamalizwa kwa kuwekana sawa kuambiana ukweli.

Shukran sana Yona kwa kutuhabarisha kwa kina kuhusu tukio la Hip Hop Mitaa, Sanaa na Kilinge. Tupe tovuti unazo/mnazotumia kwa ajili ya mawasiliano ya shughuli hii

Mitandaoni mimi napatikana hapa;

Facebook: Yona Poppa Mwandenuka(Big Poppa)
Instagram: yonamwandenuka 

Ihali kwa upande wa shughuli za Mitaa Sanaa na Kilinge ni;

Facebook: Mitaa sanaa na kilinge
Instagram: Mitaa Na Sanaa
YouTube: Mitaa Na Sanaa

Shukran!