Rojo Fojo & Dark Master - Emcee Of The Month October 2023

Dambwe La Hip Hop mwaka 2016 walitukumbusha wajibu wetu sisi wana Hip Hop kua kwa chochote tunachofanya tuhakikishe kua tunaangalia “Jamii Kwanza”. Ngoma hii ilitoka kwenye mradi wao wakudumu “Macho Ni Ngumu Kuona”. Kauli mbiu hii ya “Jami Kwanza” ndio kigezo cha kujipima na kupima kama ma emcee wetu wana elimisha jamii wakati wakiwaburudishi.

Emcee Rojo Fojo kwa majina rasmi Ali Shabaan ambae ni daktari wa afya ya akili kitaaluma anae patikana pale Hospitali ya Milembe, Dar Es Salaam, aliungana na Dark Master majina rasmi Athuman Jumanne ambae kando na kua emcee ni muigizaji mzuri tu (cheki filamu za BongoHoodz pale YouTube) pamoja na kua balozi wa afya ya akili anaetumia muziki wa Hip Hop pale Milembe. waliungana pamoja na kutupatia wimbo wakuelimisha jamii “Afya Ya Akili”.

Rojo Fojo

Wimbo huu ambao ulizinduliwa rasmi mbele ya Naibu Waziri Wa Afya kwenye shehere iliyo adhimisha siku ya Afya Ya Akili tarehe 10 mwezi Oktoba 2023 pale Nyerere Square, ulikuja mda mwafaka kwani tatizo la afya ya akili limekua changamoto sana miaka hii ya karibuni.

Kwenye mdundo flani mzuka sana uliyo tayarishwa na J Drama (On The Beat)  wawili hawa wanaungana kutupatia elimu kuhusu gonjwa hili. Wimbo unafunguliwa na beti kutoka kwa Mwanachemba, Uncle Digital, Doctor Wa Hisia anaetuambia vile gonjwa hili linavyo athiri jamii wengine wakadhania ni maswala ya ushirikina. Hii inaonesha vile ni muhimu sana kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu janga hili linalowasibu.

Dr. Rojo Fojo nae anatupatia elimu zaidi kuhusu nini husababisha matatizo haya na nini kifanyike ilikuweza kupata suluhu. Kiitikio pia kinasisitiza kua maswala ya afya ya akili, “Ni tatizo kama mengine/Na ukiziona dalili za mwanzo njoo upime/…” Tusichukulie poa maswala ya Afya Ya Akili.

Dark Master

Ni jambo jema kuona wasanii wakifanya wajibu wao kama vioo vya jamii kwa kutuletea elimu ya mambo magumu kwa njia nyepesi ya kueleweka na kuburudisha. Ngoma hii ni nzuri sana kwa kutoa elimu mashuleni, vyuoni, magengeni, kwenye dala dala kwani mtu akiuskia anagusika na kufarajiki kua wana Hip Hop wanajali jamii.

Hongera sana kwa Rojo Fojo na Dark Master kwa kujinyakulia tuzo ya ishirini na mbili ya mwezi wa Oktoba 2023 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.