Shazzy B - Emcee Of The Month September 2023

Tuzo ya ishirini na moja ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (September, 2023) tumemkabidhi Shazzy B (Just Facts, Thoughts)

Wachanaji wa kike kwenye game la Hip Hop duniani sio Africa Mashariki tu ni wachache mno. Hii ni kutokana na sababu kibao ambazo zilishatajwa na waandishi na mashabiki wa Hip Hop kwa hiyo mimi sitozitaja hapa.

Ila kitu nitakachokitaja hapa ni kuhusu almasi flani ambayo iligundulika kule machimbo ya handaki ya Hip Hop ya Kenya, emcee dada Shazzy B. Shazzy B tulianza kumskia taratibu alipokua akijijengea jina kwenye cyphers za Hip Hop, The Mic Gym na Door Knockers.

Shazzy amejituma na amezidi kunoa penseli yake ili kuweza kutupatia muziki mzuri unaotuburudisha na kutuelimisha. Kutoka kwenye EP yake inayodondoka hivi karibuni ndio tumepata vibao viwili vilivyo mtunuku emcee huyu tuzo yake ya kwanza ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards akiwa ni mwanadada wa pili baada ya Kanambo Dede ambaye naye alijinyakulia tuzo hii mnamo mwaka jana.

Shazzy B yupo kwenye harakati za kudondosha EP yake The Boss Lady EP aliachia kichupa kwa ajili ya singo yake ya kwanza Just Facts akimshirikisha Trabolee. Ngoma hii ambayo imetayarishwa na Kunta Official Beats kutoka Truce Label, ni mdundo wa Boom Bap ambao unawawezesha ma emcee hawa wawili wanaowakilisha vizazi tofauti kutema ukweli tu.

Kwenye ngoma hii emcee huyu anatema nondo kuhusu maisha yake ya muziki, changamoto zake na malengo yake ambayo anatarajia ayafanikishe maishani mwake ilhali Trabolee anampa shavu mdogo wake na kumshika mkono kwa kutema mashairi yaliyokwenda shule.

Mwezi September dada huyu akaamua kuonesha ana uwezo wa kusimama mwenyewe tena na kutupatia madini kwenye mdundo wa Boom Bap kwenye ngoma ya Thoughts. Ngoma hii pia imesimamiwa na Kunta Official Beats na inaongelea vita vya kimawazo anavyo kabiliana navyo Shazzy B katika hali ya kujitafuta, msongo wa mawazo na afya ya akili.

Ni jambo jema kuona kuwa kuna akina dada hawajautosa utamaduni wa Hip Hop na wanaenda freshi kwenye midundo ya Boom Bap. Ni mda tu unahitajika ili tuone kama Shazzy B atafanikiwa kuwa The Boss Lady kupitia sio tu hii EP yake bali hata miradi ya baadae.

Hongera sana kwa Shazzy B kwa kujinyakulia tuzo ya ishirini na moja ya mwezi wa September 2023 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.