Fivara - Emcee Of The Month February 2024

Tuzo Ya Ishirini Na Saba ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (March, 2024) Tumemkabidhi Jay MauMau (Back To The Source, Sons Of Dogons)

Ukitaka kujua Jay Mau Mau ni nani inapokuja kwenye mchango wake kama emcee kwenye tasnia ya Hip Hop hebu pata mda ucheki YouTube channel yake ambayo ndo CV yake ya kazi. Jamaa amedondosha ma ngoma kibao kwa miaka zaidi ya mitano zikiambatanishwa na video nzuri za hali ya juu.

Jay kwenye hii safari yake ya muziki amefanya kazi na watu tofauti wakiwemo Mzee Peter O’neal (wa Black Panthers), Anna Maria, Vique Ofula, Kenny Smith, Tobias Tillian, Jot Kosmos, Makostamina Masta Kimbo na Nyota Ndogo.

Mwaka huu Jay ameendelea na utaratibu ule ule wa kudondosha ngoma na video nzuri pia. Mwana alitufungulia mwaka na ngoma mzuka sana kwa jina ‘Back To The Source’. Ngoma hii ambayo inatuhimiza turudi tulipoanzia au tusisahau tulipoanzia imesimamiwa na mtayarishaji HR The Messenger kutoka Kenya.

Jay Mau Mau ameishi mamtoni mda mrefu ila jamaa anajivunia chimbuko lake na kupitia kinasa sauti na sanaa yake anaonesha haachi mila kwani hawakukosea wazee waliposema “Muacha mila ni mtumwa. Nilichokipenda pia kwenye video ya ngoma hii ni vile elements kibao za Hip Hop zimewakilishwa freshi kwenye video hii; ushairi (emcee), graffiti (machata), break dancing, Dee Jay na mavazi (street fashion).

Kwenye ‘Sons Of Dogon’ Jay Mau Mau aliungana na HR The Messenger tena kutupatia ngoma chanya sana. Dogon ni kabila flani linalopatikana kule Mali ambao walibobea kutokana na uwezo wao kujulikana kwa hadithi zao kuhusu asili yao na ujuzi kuhusu nafasi na viumbe vya nje. Kwenye ngoma hii Jay kwa kutumia jina la Dogon ameendelea kutuhamasisha kupenda na kutambua historia ya kwetu kwani mtu akitaka kukupoteza huanza kwa kukuibia historia yako. Hivyo Jay amejitwika jukumu la kuelimisha jamii ambayo ni nguzo muhimu ya Hip Hop kwenye kipengele cha Each One Teach One. Kichupa kama kawa ni mzuka na utakipenda.

Hongera sana kwa Jay Mau Mau kwa kujinyakulia tuzo ya ishirini na saba ya mwezi wa March 2024 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.