Plate MdaiJasho - Emcee Of The Month Mwezi Novemba 2022

Tuzo ya kumi na moja ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (November 2022) tumemkabidhi Plate MdaiJasho (Kichwani, Taswira Halisi 1, Mpwa, Mapinduzi Yako, Kichwani, Mpwa, Yoo, Nani Hajui?, Kamari )

Mwaka huu umekuwa busy sana kwa Plate MdaiJasho. Emcee huyu ambaye anapatikana Ushirombo, Geita, Tanzania alitubariki mwaka huu wote na sio tu ngoma mpya bali pia video pia. Baada ya kuachia msururu wa EP yake ya tatu chini ya mradi wake unaokwenda kwa jina TuTaLeTa (Tujenge Taifa Letu Tanzania) Desemba mwaka jana, emcee huyu aliendelea kwa kasi hiyo hiyo kwa kuachia video yake Kichwani mwezi Februari.

Kichwani ilikuwa singo ya kwanza kuachiwa kutoka kwenye mradi wa TuTaLeTa Vol. 3 ulisimamiwa na Kunta Official Beats kutoka Nairobi Kenya akisaidiwa na Stim Master kwenye maswala ya mixing and mastering. Wimbo huu ambao ulidonyoa sampuli kutoka wimbo wa Big Syke aliomshirikisha 50 Cent, My Money On My Mind ulikuwa unatuhimiza tuchakarike kihalali ilikuweza kupata senti za kujikimu.

Wakati bado tunajaribu kuwa wabunifu na kutafakari kuhusu wosia wa Kichwani, Plate akarudi shaa shaa studio kutuandalia jiwe jingine. Raundi hii aliomba msaada kule BBC kwa Black Ninja na baada ya kupewa mdundo uliotumia sampuli mzuka sana toka kwa Dolly Parton alikwenda hadi O_Lock Studio zilizopo Kahama na kutuandalia kibao flani chenye hisia Taswira Halisi Vol. 1. Wimbo huu unafafanua zile ahadi wanazotamka wanandoa wakati wa harusi wanaposema watakua na wapenzi wao “wakati wa uzuri, wakati wa ubaya, wakati wa utajri, wakati wa umaskini, kwenye hali ya ugonjwa na afya, kupenda na kutunza, hadi kifo kitakapotutenganisha” kwani shemeji yetu anaumwa ila Plate anaapa kuwa naye bega kwa bega hadi pale atakapoachia pumzi yake ya mwisho. Elimu tosha kwa wanandoa.

Mwezi wa 5 kijana aliamua kusafisha hali ya hewa ya Hip Hop ya Tanzania alipoachia diss Track yake MV Bukoba ambayo ilizua gumzo sana kitaa kabla ya kurejea katika ratiba yake ya kutulisha madini. Mwezi wa 6 MdaiJasho akaamua aongee na wadogo zake kwenye kibao chake kilichotoka rasmi mwaka jana 2021 mwezi Februari kwenye TuTaLeTa Vol 1. kiitwacho Mpwa. Akisaidiwa na Jaheem Masaki kwenye mdundo wa Mwamba Mgumu (Sima On Da Map) na Young Ghost, emcee Plate anawasihi wapwa (nephew) zake kuhakikisha wanaishi vizuri na jamii na pia wawe chonjo na vishawishi vinavyokuja na shinikizo la rika. Je mpwa ataskia? Ushauri sio ombi.

Mwezi wa nane Plate MdaiJasho alipata mshawasha wa kuongea na Hip Hop kama mtu na basi akaomba mdundo tena toka kwa Mwamba Mgumu wakishirikiana na Stim Master wakatubariki na jiwe jingine tena Mapinduzi Yako. Kwenye wimbo huu Plate anaongelea historia ya Hip Hop Tanzania na matokeo chanya aliyoleta kijamii na kiharakati. Hip Hop Hurray.

Kwenye Yoo wimbo uliodondoka mwezi September uliosimamiwa na mtayarishaji Evano wa 64 Hip Hop kule Eldoret, Kenya emcee huyu alitupatia wimbo simple  juu ya mdundo simple sana ila kama kawaida ya Plate MdaiJasho edutainment lazima ihusike kwani hapa unaburudika na kupata shule kwa mkupuo.

Baada ya hapa emcee huyu anaenda kisiasa zaidi kwani nyimbo mbili zinazofuata baada ya hapa zinagusa mada hii. Kwenye Nani Hajui, Plate bado anabaki kule Kenya na pamoja na Evano tena wanatuangushia wimbo na video mzuka sana. Tarumbeta linapiga taratibu juu ya mdundo wakati Plate MdaiJasho akitupatia masomo juu ya siasa za bongo.

Masomo ya siasa yanaendelezwa tena kwenye darasa la Simple Versity wakati Plate anaamua kumuenzi hayati rais John Joseph Pombe Magufuli kwenye wimbo Alisema JPM akishirikiana na Ormie 29 kwenye chorus ilhali Mwamba Mgumu alisimama kwenye mdundo na Stim Master akimalizia mixing and mastering. Japokua ngoma hii iliachiwa mara ya kwanza mwaka jana mwezi April 2021 baada ya Magufuli kuaga dunia kwenye TuTaLeTa Vol 2 #Magufulification, Plate MdaiJasho aliamua kumkumbuka shujaa huyu kwenye siku yake ya kuzaliwa tarehe 29 October kwa kuachia kichupa kipya ya kumuenzi. Kazi nzuri.

Katikati ya mwezi Novemba emcee huyu alirudi studio tena ila wakati huu alitimba kule Baobab Studios, Pwani kwa mtayarishaji OneJast na kutupatia somo jingine tena Kamari. Wimbo huu ni shule tosha kwa yoyote ambaye ana bisha kuhusu athari za kamari ukiangalia vile kila unapowasha data, radio au tv kila mahali matangazo sasa yamekuwa kuhusu kamari/betting aka mkeka! Natumai vijana wameskia onyo la Plate MdaiJasho anapowaambia kua,

“Kamari mchezo wa hatari/
Kamari humaliza mali/
Kamari haina hodari/
Kamari kaa nayo mbali/
Kamari ni shari/
Kamari ni zari/
Kamari ni ghali/
Kamari ajali!/”

Aisee Plate MdaiJasho kajituma sana mwaka huu na ametupatia video 9 za nguvu zinazozingatia vigezo muhimu vya utamaduni wa Hip Hop, elimu na burudani bila ya kuhesabu singo zake binafsi pamoja na zile alizoshirikishwa na ma emcee wenzake. Pia tusisahau emcee huyu kutokana na ubunifu, uthubutu na utendaji kazi wake ameweza kushiriki kwenye cyphers mbili za kanda; Door Knockers Cyphers Episode 3 pamoja na All African Cypher 2 ya Truce Label. Tutakua hatujamtendea haki emcee huyu kama hatutotambua mchango wake kwenye tasnia ya Hip Hop sio tu nchini Tanzania bali kwa kanda yetu ya Africa Mashariki ki ujumla. Hip Hop ya Geita, Tanzania na Africa Mashariki ipo pahala pazuri kwenye kalamu ya huyu bwana.

Hongera sana kwa Plate MdaiJasho kwa kujinyakulia tuzo yetu ya kumi na moja ya mwezi November 2022 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.