GNL Zamba- Emcee Of The Month June 2023

Tuzo ya kumi na nane ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (June 2023) tumemkabidhi GNL Zamba (Hustle & Motivate)

Ni mwezi sasa tangu tuanze kuangazia ngoma za kutoka nchi ya jirani ya Uganda kila jumapili kwenye kipindi kipya “Uganda Ulingoni”. Hatua hii imetusaidia sisi wana Africa Mashariki kuweza kutega maskio ili kuweza kunasa na kinachojiri kutoka kwa wenzetu inapokuja kwa maswala ya utamaduni wa Hip Hop na sanaa.

Uganda ndio tulipo mpata mshindi wetu wa tuzo ya Micshariki Africa Emcee Of The Month ambayo tunaitoa kila mwezi kama njia ya kuenzi wachanaji kutoka kanda letu ambao wanatuburudisha na kutuelimisha pia.

Kutana na GNL Zamba ambae ni emcee wetu wa kwanza kutoka Uganda alie jinyakulia tuzo ya mwezi Juni 2023 kutokana na wimbo na video yake mzuka sana Hustle & Motivate. Binafsi GNL Zamba ndio nimemfahamu hivi majuzi tu ila nilichogundua kutokana na tafiti zangu nilizofanya kuhusu mwana Hip Hop huyu ni kua ana uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja.

GNL ambae anachana kwa lugha za Kingereza, Kiswahili na pia Luganda au ukipenda Lugaflow alitudondoshea kibao chake kipya Hustle & Motivate ambacho kinatutia moyo inapokuja kwenye maswala ya kusaka mikwanja kwa ajili ya kujikimu. Ngoma hii ambayo inapiga juu ya mdundo flani mzuka sana unatuhamasisha tujiamini kwa chochote kile tunachokifanya kwani tutafanikiwa tu! Hili ni somo zuri kutoka kwa Zamba ambae jGNL linamaanisha Greatness with No Limits (Ukuu Usiokua na Mipaka.)

Huu mgoma ni kwa ajili ya yoyote yule anaeparangana, pambana kwenye Utamaduni wa Hip Hop ukibweteka itakula kwako.

Hongera sana kwa GNL Zamba kwa kujinyakulia tuzo yetu ya kumi na nane ya mwezi Juni 2023 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.