One The Incredible - Emcee Of The Month March 2023
Tuzo ya kumi na tano ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (March 2023) tumemkabidhi One The Incredible (Msaada Kwao, Vitendo Dhidi Ya Maneno, In My Heart)
Mwaka huu ni Jubilee Year ya Utamaduni wa Hip Hop. Utamaduni wa Hip Hop umepiga hatua nzuri kutoka ile tarehe 11 Agosti mwaka 1973 Hip Hop Kulture ilipozaliwa kule Bronx. Mtu mmoja ambae ameuvaa utamaduni huu nchini Tanzania ni emcee One The Incredible, ndio, yule wa Culture Movement.
Mapema mwaka huu nae pengine kwa kujua umuhimu wa mwaka 2023 na mchango wake kwenye utamaduni huu hapa Tanzania na East Africa pia, alikuja na album yake mpya Achieving Greatness. Ni kutoka kwa kazi hii ndio tumepata vibao vitatu ambavyo vimemuwezesha emcee huyu kujinyakulia tuzo ya Micshariki Africa Emcee Of The Month, March 2023.
Cha kufurahisha ni kwamba kwenye vibao hivi vyote Uno amemshirikisha TK Nendeze ambae binafsi naona mchango wake kwenye sanaa ya uimbaji na kwenye chorus za wana Hip Hop bado haujatambulika vilivyo. Kwenye ngoma hizi ndio unaona nguvu ya sauti ya mwanadada huyu anapo bariki ngoma hizi za One na sauti yake nzito ila yenye utulivu.
Msaada Kwao ndio kibao cha kwanza kwenye orodha yetu ambayo kimepikwa freshi na mtayarishaji Wizard. Juu ya mdundo wenye vinanda vizuri sana, One anaongelea changamoto za kuishi na watu na kwakua moyo wa mtu kichaka na ni vigumu kujua hila na nia zao kuja kwako basi anakushauru ukae na wana kwa makini, kwani wengine wanaweza kua karibu nawe kwasababu ya vitu wanavyovipata kutoka kwako ila vikikata ndio utawajua freshi. Huu mgoma ukitaka kuuelewa upige kwenye kwa sauti ya juu, hahaha. Bomba sana.
Mtayarisha John Mahundi nae anashika doria pale studio za MV09 kwa Ommy Pah na kutupatia mdundo wa Vitendo Dhidi Ya Maneno ambapo One akiwa na TK Nendeze wanaongelea umuhimu wa watu kuwa watendaji zaidi ya kua waongeaji na ndio maana unaskia msisitizo huu kwenye kibwagizo cha kila beti ya mashairi ya One akisema, “Lakini huu utamaduni, Vitendo Dhidi Ya Maneno”. Tuwacheni blah blah na kabobo nyingi, tupigeni kazi, tuwe zaidi watu wa matendo.
Umahiri wa mtayarishaji Wizard unauona tena kwenye In My Heart akiwemo TK Nendeze tena. Hapa unaona team work ya watatu hawa, mtayarishaji, mchanaji, muimbaji (m3). Kwenye ngoma hii emcee One anakuonesha uwezo wake wakua bilingual, anachana freshi tu kwa Kingereza na Kiswahili na unamskia poa. Utatu huu wa O-W-T unatuandalia ngoma yakututia moyo na kutuinua ili tuweze kujiamini, kuwa wajasiri na kufanya tunachofanya, bila kutetereka na kuamini kua tutafanikiwa.
Hongera sana kwa One The Incredible kwa kujinyakulia tuzo ya kumi na tano ya mwezi wa March 2023 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.