Ulrykah Benard

Kama mwanaharakati wa Hip-Hop, jambo moja ambalo nimeona ni mwaka huu wa 2022 utakuwa wa kufurahisha kwa sababu tu ninakutana na wasanii wapya ambao wanafanya kazi nzuri.

Sasa mfahamu Ulrykah Benard . Yeye ni femcee ambaye nimekuwa nikimsikiliza kwa mwezi mmoja sasa, na ninakubali mtindo wake, haiba yake na nondo zinaonesha kuwa ana mengi ya kutoa kwa ajili ya utamaduni wa hip hop. Shukran zangu ziende kwa DJ Cuts Dread wa Sherehe Sheria kwa ajili ya kunikutanisha nae.

Japo bado hajatoa mradi mkubwa kando na ngoma chache alizoachia ila kuna taarifa kwamba mradi wake tutaupata mwaka wa huu 2022.

Ulrykah ni rapper wa Kenya, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo anayeishi Washington DC, Amerika. Alizaliwa na kukulia nchini Kenya alipofanya elimu yake ya A-level katika shule ya Moi Girls Isinya na baadaye kuhamia Marekani.

Mbali na kufanya muziki, pia ana ujuzi katika masuala ya teknolojia.

Nilipata fursa ya kufanya mahojiano naye ili wewe kama shabiki wa hip-hop/rap upate taarifa kumhusu.

NYIMBO MUHIMU:

  • Black Lives Matter
  • Deep Reverence
  • Breakfast In Bed
  • It’s The Way

Karibu sana Micshariki Africa dada Ulryhah. Jina lako la kisanii, Ulryka Benard lilikujaje na lina maanisha nini?

Jina Ulrykah Benard limetoka kwa mchanganyiko wa jina la mwisho la baba yangu na jina ambalo nilipata kwenye gazeti maarufu wakati huo.

Safari yako ya muziki imekuwaje, nini kilikufanya uingie kwenye muziki wa rap?

Upendo wangu kwa muziki ulizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 80 na nilikua nikisikiliza muziki wa Taarabu, R&B, Old School na aina zingine nyingi kwa hivyo nilikulia kwenye mazingira yenye sauti ya muziki ambayo ni tofauti.

Nilipata msukumo kutoka kwa vyanzo tofauti kwa hiyo nilianza hivi karibuni kufurahia beats kutoka kwa wadundishaji midundo kisha nikaanza kupima uwezo wangu hadi  hapa  nilipo.

Muziki umekuwa sehemu ya maisha yako kwa muda gani?

Muziki umekuwa sehemu kubwa sana ya maisha yangu… Maisha yangu yote. Mimi huamka kila wakati kwa muziki na kwenda kulala kwenye muziki.

Ulitambuaje kwamba muziki ulikuwa njia ya kusonga mbele kwako?

Wakati fulani katika maisha yangu, nilijiwazia, je nina chochote cha kupoteza? Acha nishiriki nilichoandika na nione ulimwengu unafikiria nini.

Je, unalenga kuleta mabadiliko kwa njia gani?

Ninataka kubarikiwa na fursa ya kuwa msukumo kwa wengine na kubadilisha ulimwengu kupitia muziki.

Ninanuia kuhamasisha ulimwengu kupitia muziki wangu na kuwa katika nafasi nzuri ya kufanya hisani.

Je kazi yako ya muziki inaelekea wapi, nini maono?

Maono kwangu yangekuwa ni kuweza kushiriki jukwaa na wakubwa.

Je, ni mradi gani unaoupenda zaidi kufikia sasa?

Mradi wangu ninaoupenda hadi sasa umekuwa mabadiliko yangu mwenyewe kutoka kuwa mtu ambaye angeogopa kusimama mbele ya watu hadi mtu ambaye hawezi kungoja onesho linalofuata. Kujibadilisha ni mradi.

Ni akina nani walio na ushawishi mkubwa zaidi wa muziki wako haswa hapa Kenya?

Walioathiri muziki  wangu ni pamoja na Femi One, Mejja , Khaligraph Jones, Naiboi , Nadia Mukami , ArrowBoy na wengine wengi.

Nini kinakufanya uwe tofauti na wasanii wengine wa rap?

Ninathamini vipaji na vipawa vya kipekee vya kila mtu, nina mfanano fulani na msanii mwingine lakini uzoefu wangu wa maisha ambao unaunda muziki wangu ndio unanifanya kuwa wa kipekee.

Nani ni shujaa wako mkuu unaemuangalia na kwa nini?

Ninajaribu kujiepusha kujifananisha na mtu zaidi ya kuvutiwa, kwa hivyo kwa wakati huu sidhani kama nina shujaa mkuu.

Je una tabia zozote za kijinga ambazo tunapaswa kujua?

Sina hakika kama kuna tabia nilizo nazo ambazo ni za kijinga…akicheka. Labda kutazama simu inapoita kwa sababu sipendi kuongea na simu.

Je, unadhani mustakabali wa tasnia ya muziki uko wapi?

Mustakabali wa muziki upo mikononi mwa wasikilizaji, wao ndio watumizi wakubwa wa bidhaa yetu. Kama wasanii ni jukumu letu kuunda mitindo na aina mpya lakini mwishowe ni wasikilizaji ambao wana usemi wa mwisho juu ya kile wanachotaka kusikia.

Je, unapanga kufanikiwa vipi katika soko la Kenya?

Ninapanga kupenya katika anga ya muziki wa Kenya kwa kufanya kazi na wasanii wengine na kuwafanya mashabiki wao kunifahamu pia.

Wewe ni rapper wa Kenya mwenye makazi yake kule Marekani, unadhani nini kinafanya muziki wa Marekani na Kenya kuwa tofauti?

Kuishi Amerika kunatoa matukio ya kipekee ambayo watu wanaoishi Kenya wanaweza wasijihusishe nayo. Ninataka kuziba pengo kati ya haya mataifa wawili na ninatumai kwamba wasikilizaji wa Kenya watafurahia mtindo ninaowasilisha… pamoja na aina mbalimbali za muziki nchini Kenya hatuhitaji kuwa na mtindo sawa wa muziki.

Nini kinafuata kwa Ulrykah ?

Nina nyimbo na video chache za muziki ninazofanyia kazi na nitatafuta ubia mwingine pia.

Neno la ushauri kwa chipukizi ambao wanajaribu sana kufikia hatua fulani na wanataka tu kukata tamaa?

Kama unawaza kukata tamaa… usikate tamaa! Watu wengi hupata msukumo kutoka kwako hata kama hawaoneshi kwenye mitandao ya kijamii… usikate tamaa!

Mitandao yako rasmi ya muziki/mitandao ya kijamii?

Facebook: Ulrykah Benard
Instagram: ulrykahbenard

Je, ungependa kumshuruku nani?

Ningependa kuwashukuru na kuwapa hongera wasichana wote wachanga wanaokuja … Tunashindana katika ulimwengu wa wanaume na hilo ni jambo la kupongezwa.

Asante. Kingine chochote cha kutuacha nacho ukimalizia mahojiano?

Unapoteza 100% ya risasi zako ambazo hukupiga (kujaribu jambo) ! Kwa hivyo ikiwa utapata nafasi ya kupiga risasi, piga risasi!! Huna cha kupoteza.