Daz Nundaz - Kamanda

Mwaka 2002 ndio mwaka ambao kundi la Daz Nundaz refusha Dangerous Zone of Nundaz walipata kuachia album yao ya kwanza kama kundi inayofahamika kwa jina la Kamanda.

Kabla ya kutoa album yao ya Kamanda walianza na wimbo unaoitwa Maji Ya Shingo wimbo mmoja mkali sana wenye simulizi nzuri sana kusikia hasa ukizisikia sauti za Daz Baba na Feruzi wanavyoimba.

Daz Nundaz ni kundi linaloundwa na memba watano ambao ni Daz Baba, Feruzi, Lusajo, Larumba bila kumsahau Critic. Daz Nundaz ni miongoni mwa makundi yaliyofanya vizuri sana kwa mwaka huo.

Baadae kundi lilipotea kwenye ramani ya muziki baada ya memba wawili kuamua kila mmoja kufanya kazi ya peke ake(solo project) memba hao ni Daz Baba na Feruzi kila mmoja alitoka na album yake.

Albam ya Kamanda ilitoka chini ya Bongo Records kwa mkali P Funk, Majani.

Album ilibeba mawe tisa mazito sana na kutoa shavu kwa wasanii wa tano tu. Nyimbo zilizobeba album ya Kamanda.

  1. Barua
  2. Maji ya Shingo (remix)
  3. Kioo (feat. Scout Jentiaz & Sewa Side)
  4. Matatizo rmx (feat. Lady JD & Juma Nature)
  5. Kamanda
  6. Shuka Rhyme
  7. Kiama (feat. Computer)
  8. Nitafanya nini?

Huku wimbo original wa Maji Ya Shingo ukiwekwa kapuni inasemekana chorus yake ilizua kizaizai kidogo kwa wenye mamlaka. Wakaweka remix ambayo ilibadilishwa chorus na mdundo beti zikibaki vile vile.

Maji ya shingo ya kwanza chorus yake ilisimama mtindo huu, au tuanze na utangulizi wake kwanza wa wimbo.

Yooh!
Daz Nundaz family
Sakafu ya majukumu yafuka moshi
Nguvu ya mkiwa duniani haitoshi

Kiitikio

Maji ya shingo yamenifika mwana mkiwa Sisikii siambiwi la kutamkiwa
Jela ni kitu gani nitakwenda nitaachiwa Kama vikesi mbuzi vingi nishasingiziwa
Mbele kiza kimetanda sioni njia Mbele kiza kimetanda sioni njia

Wadadisi wa mambo wanasema wakuda walimaindi mstari unaosema "jela ni kitu gani nitakwenda nitaachiwa" bwana weh! Wazee wa ng'ombe wakaona madogo wanawachukulia poa yani jela ni kitu gani kweli?

Nakupa na kionjo cha beti ya kwanza ambayo alipita Feruzi.

Misukosuko ilianza tu pale nilipofiwa, wazazi waliponitoka nikabaki mwana mkiwa/
Sijuhi ni wapi mimi nitakimbilia, nabaki najikunyata kama kinda la njiwa/
Wazazi waliniachia urithi ila ndugu wakanidhulumu, wakanifanyia na njama nikapewa na hukumu/
Maisha yangu hivi sasa jama ni magumu, sina kitu alosto mimi yani sina usawa, siwezi kuruka tena mimi sina ubawa/

Maji ya shingo yamenifika mwana mkiwa, nipo katikati ya bahari sioni hata kisiwa/
Naangaza pande zote sioni hata wa kuniokoa, kina sasa ni kirefu naelekea kuzama/
Hii si wema tena ni kama unyama yote hii sababu ya kifo cha baba na mama/
Mwili umechakaa kwa ajili ya kusota na jela, kila mtu anithamini sababu wazazi wangu wapo ahera/
Sioni hata wa kunitetea sina hata nguzo ya kuegemea, ninavyoteseka maadui wanachekelea/

Maji ya shingo, maji ya shingo
Maji ya shingo, maji ya shingo

Ukisoma beti unapata picha ni jinsi gani mali zinaleta tatizo pindi aliyezisaka akiwa katangulia mbele ya haki kitu gani kinabaki kwa familia yake.

Ukiachana na Maji Ya Shingo manundaz na ununda wao wote wakaja kulia kwenye Barua humu walilia sana yani ingekuwa zama hizi za Mtalaze wangeupa jina "mapenzi yalaniwe". Barua ni wimbo ambao unazungumzia mtu aliyeachwa na mpenzi wake na kwenda kuolewa na mtu mwingine.

Machungu yote yalimalizwa kwenye wimbo. Beti alianza Daz Baba ndipo Feruzi akampokea japo kuna watu wengi zamani walishindwa kutofautisha sauti kutokana na mtindo wa kuimba wa Daz Baba na Feruzi.

Oya namna gani mzee,
Ah, mbona leo uko hivi mzee, (basi tuuu).

Vipi mchizi wangu mbona naona umesizi, Unaonekana kama moyoni una majonzi/
Au dili zako leo haziendi sawa, jinsi unavyoonekana kama umepagawa/
Niambie ili nielewe, ili na mie nisipagawe/
Kwani tangu nimefika nakuona umepooza, hebu niambie kitu gani unachowaza/
Sema basi, nini kinachokusumbua nafsi
Niambie basii au kuna kitu kimekugasi/

Aah we bora acha tuu wangu mkachaa, ni story ndefu nikianza kukupa/
Ubongo wangu nahisi kama unazafilika, kwa haya matatizo makubwa yaliyonifika/
Shemeji yako nadhani unamjuaa, ambaye kichwa changu alikichenguaa/
Baada ya kuishi muda mrefu na wangu lazizii,Ikabidi niende kuwataarifu wazazii/
kwamba nimeshampata mwenzanguu, ambaye nitafunga naye pingu za maisha/
Na nilikuwa na hakika hakuna ambaye atatutenganishaa, Basi bwana baada ya kurudi yangu safari/
Nikakuta mlango wa gheto umepigwa kufulii, Nauliza watu wote sipati jibu/
Ni mkasa mkubwa mwenzako ulionisibu, nikaanza kusaka tunda langu kwa sanaa/
lakini jitihada mwisho zikashindikana, Nikaamua basi tu mi kutulizana/
nikawasitoki nje nipo ndani tu nalalaa, Huku mawazo mengi kichwani yamenitawalaa/

Ndipo linafata moja kati ya chorus la kusikitisha la kwenye album hii …

Katika mahaba tulishazama dimbwini, lakini barua niliopokea nashindwa hata kuamini/
Ua langu moyo wangu halipo tena na mimi, barua hii jamani inanihuzunishaa/
kila nisomapo moyo unasononekaa, na ufukara ndio uliotutenganishaaaa/

Apo ndipo unapopata picha kilichowaliza manunda ni ukosefu wa hela na sio uno au vumbi. Beti ya pili inaendelea

Subiri basi story nikumalizie enhe! mkasa huu ulionifika mie enhe!/
Hususani baada ya wiki kadhaa, ndipo hapo nikapokea baruaa/
Kilichokuwa ndani sikukitambuaa, nikaja kuelewa baada ya kuifunguaaa/
Nikakuta barua yenye ujumbe mzito, ikiwa imeambatana na kadi ya mwaliko/
Ndege wangu ameruka hayupo tena namii, sasa hivi sijui mwenzangu mimi nanii/
Hali yangu duni imenifanya kuelemewa, na hivi karibuni demu wangu anaolewa/
Barua inanisisitiza Harusini niuzuriee, sijui siku hiyo hata wapi mi nianziee/
Mpenzi umeniacha kwenye nyavu nimenasa, nimebaki kama kipofu sioni pa kupapasa/
Nikisoma barua hii kumalizia huwa nashindwaa, kwani nahisi kama ulivyonishadundaa/
Shika mwenyewe usome barua hii, soma mwenyewe uone barua hii/
Shika mwenyewe usome barua hii, soma mwenyewe uone barua hii/

Ikufikie wangu wa enzi mpenzi, mi kiafya mzima, natumai na we kiafya uhai/
Dhumuni la barua ni kukutaka na wewe kujua, mimi ni Assa na kipi kisa na mkasa/
Kilichonishawishi bali nawe mpenda kuishi, sio siri mimi binafsi kupenda kuishi maisha duni ya chini sana/
Kumbuka ufukara umasikini kututenga vimechangia, ila usipinge bwana, sasa nani alaumiwe unadhani/
Hivi punde tu nataraji kufunga pingu maishani ili niishi maisha ya thamani/
Yaliyogharama tena adimu na tena adimu kama almasi, fanya hima usikose harusini ukipata nafasii/ Katika barua hii nimeambatanisha kadi hii ya mwalikoo ni yakoo.../

Basiii usimalizie kusoma, basiii usimalizie kusoma, kwani ukiendelea moyo wangu unauchomaa/
Kwa kuondoka wangu huyu mpenzii, moyo wangu umejawa na simanzi/
Niliamini tutatenganishwa na umauti, sasa nimekubali fukara hana sauti/
Mola ndiye anayegawa umasikini na utajirii, naye hali yangu mpenzi ameshindwa kuhimili/
Na ndio maana unaniona leo nimeshika tama, utadhani kifaranga aliyekosa mama/
Aliyemgaia yeye ndie aliyenipa mimi ufukaraa, lakini naamini ipo siku nyota yangu itang'araa/

Yani mpenzi wako anakukimbia kisha anakupa barua ya mwaliko sasa kwa mwendo huo kwanini usiseme "mapenzi yapewe utamalizia mwenyewe au utaomba mtalaze akusaidie kumaliza.

Barua ni wimbo ambao ulitengenezwa na Mika Mwamba ni mmoja kati ya producer wakali wa kitambo kile ambacho mziki uliku mziki sio sasa mziki umekua kiki.

Kamanda ni wimbo mwingine ambao ulipotoka tu wale wagonjwa wengi kusikiliza kwao waliona kama ndio wanakufa vile yani ukimuwekea anaona kama umemuekea mtoa roho.

Siku mapigo yangu ya moyo wangu ya mwisho yatakapovuta/
Nuru itazima mfano wa nyota inapodondoka/
Sitoweza kuamka tena macho yangu yatapofumba/
Safari imewadia nenda kwa baba muumba/
Maasela nawaachia usia/
Wambie ndugu na jamaa wapunguze kulia/
Sote takwenda bali mi natangulia/
Duniani siyo makazi yangu tena/
Niombeeni kwa mola nilazwe peponi pema/
Hamtaniona tena milele/
Nawaachieni majonzi tele/
Buliani naaga na natakata kauli/
Roho yangu inatolewa na izraeli/
Yowe la uchungu litasikika/
Pale roho yangu itakopokuwa inatokaa/
Vazi langu sanda nitakuwa nimevikwa/
Niko kwenye jeneza tayari kwenda kuzikwa/
Mauti pindi yataponikabili/
Ni nani atakayeliziba pengo hili/
Uhai utabaki mzunguko wa damu umesimama/
Kama jahazi kinani linazama/
Buriani naaga masala/
Kwaherini ndugu jamaa na masala/
Suicide masala/
Scout Jenta masala/
Kz camp masala/
Bad Memory Squad masala/
Buriani nakuaga Mika Mwamba/
Ninakutoka kamanda/
Alazwe pema peponi kamanda/

Huu ndio wimbo ambao ulibeba jina la album na ukasumbua kweli kweli miaka yake na mpaka sasa bado unasumbua unapotekea msiba.

Kiitikio

Itakuwa huzuni kwa ndugu na madela safari yangu itapofika kwenda ahera/
Mtabaki mnaniombea alazwe pema peponi kamanda/
Alazwe pema peponi kamanda/
Mtabaki mnaniombea alazwe pema peponi kamanda/
Alazwe pema peponi kamanda/
Itakuwa huzuni kwa ndugu na masela safari yangu itapofika kwenda ahela/
Mtabaki mnaniombea alazwe pema peponi kamanda/
Alazwe pema peponi kamanda/

Nyimbo zingine zilizopatikana na simulizi zake.

Matatizo

Wimbo ulizungumzia matatizo ambayo kila sehemu mtu unapojaribu kufanya jambo unakutana na tatizo. Humu Juma Nature anakwambia ukienda kucheki maiti yako ni kasheshe yani kile utakachokutana nacho utajuta labda utoe hela. Yani ni matatizo juu ya matatizo.

Shuka Rhymes

Huu kwangu ni wimbo pendwa sana yani huu wimbo masela walishuka sana mistari yani ni kama wimbo flani wa ku party hivi walivyokichafua humu utasema sio Daz Nundaz wenyewe wa kusikitika.

Nitafanya nini?

Humu pia walizungumzia watafanya nini ikiwa mikasa na matukio kwao bado yapo kila siku na maisha bado yale yale mpaka anawaza afanye nini ili apunguze matatizo. Anakwambia usione akinungunika ukajua anapenda lakini inabidi tu kwani kila mkeka unachanika.

Kioo

Huu ulizungumzia kua wao ni kioo cha mtu kujitazama na utende yale ambayo wanayatenda. Kuna jamaa anakwambia kama bado ujaelewa kuhusu kioo anakuita kuja kumtazama yani yeye ndio kioo chako wewe mtazamaji.

Kiama

Naweza kusema ukitaka kujua balaa la Computer aliepewa shavu humu ndani nenda kasikilize Muda Mrefu ya Sugu ndio utajua Computer ni nani kwenye mashairi.

Kamanda ni album ambayo naweza sema ni kama tamthilia ya kusikiliza na ukajenga picha na matukio ukaelewa kabisa. Daz Nundaz Family ni miongoni mwa makundi bora kutokea Tanzania na katika huo ubora ndio wakatupa baraka ya Kamanda tubaki nayo tuishi nayo