Veryl Mkali Wao

Veryl Akinyi anayejulikana kitaalamu au kikazi kama Veryl Mkali Wao ni mwanamuziki toka Kenya emcee/msanii wa Hip Hop/msanii wa kurekodi na kuigiza na Deejay pia Alizaliwa Januari 30, 1994 nchini Kenya na kando na kuachia singo kadhaa zikiwemo Acha Waseme, Mkali Wao, I Have A Dream ,No Gimmicks na moja ya kolabo Triggers, mwaka huu mwishoni alifanikisha kutuletea albam yake ya kwanza Shadow Of Death.

Tulipata fursa ya kupiga naye gumzo kwa njia ya WhatsApp ili kuweza kumfahamu yeye kama msanii pamoja shughuli zake za Hip Hop pamoja na kutaka kuelewa maana ya mradi waka mkubwa wa kwanza Shadow Of Death.

Karibuni sana.

Karibu sana Micshariki Africa dada Veryl. Kwanza kabisa tuanze kwa kufahamu unaitwaje na unatokea wapi.

Naitwa Veryl Mkali Wao kutoka Nakuru 1183, Kenya.

Kwa nini unaitwa Verly Mkali Wao, jina lilitokea wapi au majigambo tu? Sio kujiamini kupitiliza unapodai wewe ni "Mkali Wao"?

Nilipokua naanza kuchana miaka ya nyuma nilikua najulikana kama Veryl Sweezy, kuna ngoma nilifanya mwaka wa 2017 inaitwa Mkali Wao na ni ngoma ambayo mashabiki walipenda sana mpaka Queen Nerfertiti ambaye ni mmiliki wa Crown alifadhili video ya wimbo huo.

Mnamo mwaka 2019 katikati niliweza ku perform Churchill Show na kupitia majaribio ya tukio hili watu walianza kuniita Mkali Wao so hata wakati ulipowadia wa kuonesha kipaji changu kwenye hiyo tamasha hili Churchill aliponiita jukwani alinitambulisha kama Mkali Wao na toka hapo jina likageuka toka kwa Veryl Sheezy hadi Veryl Mkali Wao.

Tueleze kidogo kuhusu historia yako ya nyuma ya mziki

Historia yangu ya mziki imekua ya milima na mabonde. Kitambo nikianza kwa upande wa uwasilishaji na uchanaji naweza sema nilijaribu na pia nilikua mchanga sana na sikujua utamaduni huu kiundani ila niliweza kuchana kwenye matamasha kibao sana kama vile Mseto Campus Tour, Churchill Show, UnKut The Cypher, E Squared Battle Rap, matukio ya Sauti Za Mabinti pamoja na Hip Hop Garage. Majukwaa haya yalinisaidia sana na yalinisogeza hadi mahali nipo kwa sasa.

Kupitia Sauti Za Mabinti(ya Nimo Futuristic) niliweza kujuana na kundi la 1183 ambao ndio walininoa sana kwa hili game. Ndio maana utaskia kua Veryl wa sasa hivi ni tofauti sana na yule wa kitambo.

Verly Mkali Wao anawakilisha Nakuru. Tueleze kidogo kuhusu hali ya Hip Hop Nakuru. Nini kinachomtofautisha emcee wa Nakuru na emcee anayetokea kokote pale nchini Kenya?

Kitu kinachomtofautisha emcee wa Nakuru na emcee anayetoka sehemu tofauti na Nakuru ni uwasilishaji, uchanaji pamoja na punchlines. Pia Nakuru tuko na njaa sana ya game na ndio maana tunatoa na kuwapatia mradi baada ya mradi. Yani hakuna kulala na ni kazi tu mpaka milango ifunguke.

Wimbo wako ambao ulinivutia sana ni Triggers. Nieleze kidogo kuhusu kibao hichi maana kilinigusa sana.

Triggers ni wimbo ambao umetokana na matukio ya kweli. Nilikua na rafiki yangu alitaka kuchukua uhai wake sababu alihisi kama hapendwi na hapewi fursa ya kuonesha kipaji chake. Alikua akijaribu sana kufanya watu wamskie ila alianza kuchoka na kuanza kuhisi amefika mwisho.

Na kila mda alikua akijaribu kutoa uhai wake kuna mtu alikua anajitokeza anamuokoa. Hili jambo lilinigusa na kuniskuma niongee na producer wangu Level Next akasema tunaweza msaidia kama tutachana kuhusu hilo jambo. Hapo ndipo wazo la kuunda wimbo Triggers lilipo zaliwa.

Hip Hop duniani ina mashabiki na wachanaji wengi wa kiume kuliko wa kike. Je hii ni changamoto kwako wewe kama mchanaji wa kike? Je ni changamoto gani ambazo wewe binafsi umepitia hadi kufika ulipo sasa?

Hip Hop ni tasnia inayotawaliwa na wanaume na ni wakati muafaka wa kusimama ili tukubalike kwenye game la hip-hop. Ninachokiona ni kama sisi kama wanawake tunatakiwa kupigana zaidi na kuwa na ujasiri wa kutosha ili tuweze kuchukua nafasi yetu kwenye utamaduni huu. Naweza kusema kwa sasa naweza simama jukwaa moja na emcee wa kiume kwa kutumia ujuzi wangu wa kughani na nipo tayari kuchukua nafasi yangu kati yao.

Changamoto ambazo nimepitia ni kama watu kutonithamini, watu kunitaka kimapenzi ili waniwezeshe kwa namna moja au nyingine au kupata nafasi ya kufanya show katika majukwaa makubwa yatakayoniwezesha kuonesha kipaji changu, wakati mwingine nilikua nasafiri kutoka Nakuru hadi Nairobi(Kilomita 170) kwa ajili ya kupiga show ambazo wakati mwingine sikua nalipwa ilhali nilikua na majukumu kibao ambayo yanahitaji hela.

Pia kwa upande wa waunda midundo, ma producer wa kike ni wachache au hata hamna Africa Mashariki nzima kama sijakosea au ni wachache mno. Tatizo ni nini na kipi kifanyike ili kuweza kutatua hii ishu?

Ma producers wa kike wapo, nawafahamu baadhi na kama nilivyosema hapo awali madem huwa hatuweki juhudi zote kwa hili na hatuna ujasiri sana wa ku sukuma vipaji vyetu tunataka kufuata njia rahisi na hatupendi vitu vinavyofanya tufikiri sana au vinavyofanya tuwe wabunifu zaidi. Nadhani ndio maana ma producer wa kike ni wachache kwa sababu kuandaa wimbo unahitaji kuwekeza vitu kibao kufanikisha na sio rahisi hivyo.

Kando na mziki emcee Verly Mkali Wao anajihusisha na nini kingine ile aweze kuongeza msosi mezani?

Kando na kuchana mimi ni DJ. Nadhani nimejikita sana kwenye tasnia ya burudani na hapo ndipo nimewekeza nguvu zangu zote kwa sasa.

Veryl nimekuona kwenye vilinge (rap battles and cyphers). Umuhimu wa hizi battles kwenye Hip Hop game ni nini ?

Umuhimu wa battles ni kuwa zinasaidia kufanya msanii aonekane zaidi na pia inamuwezesha yeye kuonesha uwezo wake wa kuunda mashairi na kuchana pamoja na uwasilishaji. Matukio haya huonesha dunia unyama wako kama emcee ili wazidi kukuogopa!

Hayawi hayawi huwa! Hatimae ukatubariki na albam yako ya kwanza. Tueleze kidogo kuhusu mradi huu na je kabla ya mradi huu umeshatoa kazi gani hapo awali?

Ngoma ambazo nimeachia na zinazopatikana pale YouTube ni Triggers, No Gimmicks, Da Underground na Hormonal Imbalance.

Album inaitwa Shadow Of Death.  Death au Kifo hapa kinaashiria changamoto nilizopitia toka nianze mziki kama vile kutokujiamini,uoga, unyanyasaji wa kijinsia na kudharauliwa au kuonekana sina thamani.

Album ya Shadow Of Death inatokana na hadithi ya kweli na imechambuliwa kwa jinsi safari yangu imekuwa na ninahisi ulimwengu unahitaji kuisikiliza kwa sababu wengine wataona vile inahusiana na maisha yao pia watakapo usikiliza mradi huo.

Naona uliamua kutumia technologia ya tovuti kusambaza mradi wako. Technologia inamsaidia vipi emcee wa handakini(underground)? Tupe tovuti inapopatikana album. yako.

Mimi na timu yangu tuliamua kuunda tovuti ile kuweza kuwa tofauti na kuonekana tofauti na  pia kuonesha wasanii wengine kua wanaweza kujitegemea wenyewe kuuza miziki yao kwani ni rahisi na hakuna dalali atakayehusika kwa hili.

Wapi inapatikana albam yangu? Inapatikana kwenye tovuti yangu www.verylmkaliwao.com

Unapata wapi motisha ya kuandika mashairi yako? Nini hukugusa na kukuskuma kuandika mashairi yako?

Mimi huandika mziki wangu kutokana na vitu ninavyopitia mimi binafsi au mtu wangu wa karibu ila anaenipa motisha ya kuandika sana ambae ni muhimu sana kwangu ni mwanangu.

Siku hizi kuna kila aina ya midundo, Shrap, Drill, na kadhalika. Unaliongeleaje hili kwani mimi nimekuskia sana kwenye midundo ya Boombap.

Kila msanii ana aina yake ya mziki anaoupenda na mashabiki wake. Kwa hiyo mashabiki wakikubali unachowapatia nenda nayo…Mimi binafsi napenda Boombap kwa sababu najiskia raha sana kuchana kwenye midundo ya Boombap kwani inaniwezesha kujieleza vizuri wakati nikitoa mashairi yangu.

Malengo yako baada ya kuachia albam ya Shadow Of Death ni yapi na sisi kama mashabiki zako tutarajie nini toka kwako?

Lengo langu la kuachia albam lilikua kuonesha watu kinachofanyika nyuma ya pazia kwenye ulingo wa hip hop sio kitanda cha maua ya waridi. Hivyo sote tunapaswa kua na ngozi ngumu ili kuweza kufika ngazi za juu.

Nini utarajie toka kwangu? Ni mradi baada ya mradi, hakuna kulala. Nipo hapa kudumu.

Ni ma emcee gani toka Africa Mashariki unawakubali na ungependa kupiga kazi nao?

Emcee ninaye mkubali Africa Mashariki ni Rosa Ree (toka Tanzania). Napenda sana kazi zake na mtazamo alionao ni wa ajabu sana.

Changamoto za Uviko 19 zilidhuru vipi kazi zako ka mchanaji?

Changamoto mojawapo ilikua kupata matamasha ya mziki ila kwangu ilinisaidia sana kwa sababu niliweza kukaa na kuunda na kumaliza albam yangu. Hili ndio jambo moja lililokua chanya sana wakati wa janga la Uviko 19.

Kwa akina dada ambao wangependa kuchana ungewashauri nini?

Ningependa kuwaambia waje kwenye mziki wakiwa na akili timamu na tayari kwa lolote kwani tasnia ya Hip Hop ina ugumu na hakuna atakayekubembeleza, ni aidha uchane au uchanwe na uende nyumbani!

Kipi cha mwisho ambacho sijakuuliza ungependa kutuambia?

Kuwa na tim nzuri inayokuamini sana ni muhimu kwa msanii kwa sababu kuskuma kazi ukiwa peke yako unaweza pata msongo wa mawazo sana. Kwa hiyo kufanya kazi ki timu ndio mpango mzima. Sio lazima timu yako iwe na fedha, bora iwe na nidhamu na nyote muwe na lengo moja.

Ningependa kuwashukuru sana ma producer wangu toka 1183; Level Next na Edd The Beatsmith.

Shukrani sana kwa kukubali mwaliko wetu wakuhojiwa. Naomba tumalizie kwa kutupatia anwani zako za mitandao ya kijamii unapopatikana

Facebook: Veryl Mkali Wao
Instagram: Veryl Mkali Wao
YouTube: Veryl Mkali Wao
Twitter: Veryl Mkali Wao
Tovuti: www.verylmkaliwao.com

Shukran sana Micshariki Africa.