
Ukaguzi wa Albam: Maktaba Ya Mitaa (Street Library)
Msanii: Vioxii Dede
Tarehe iliyotoka: June 2018
Nyimbo: 18
Ma Producer/Wapiga midundo: Suspect Zero, Duboiz, Llyod Marcos, Fifth Letter
Mchanganyaji sauti na midundo: Duboiz
Studio: Duboiz Studio
Maktaba zipo nyingi duniani na zote zina nia sawa zinapojengwa; kuhifadhi kumbukumbu za historia, kuelimisha pamoja na kutoa fursa za utafiti. Maktaba zimekuwepo toka binadamu alipo gundua mbinu ya kuandika na walitumia njia tofauti kama vile kuandika kwenye kuta za mapango, kuchora na pia kuandika kwenye mafunjo.
Maktaba zimezidi kuboreshwa kutoka enzi zile kule Timbuktu, Mali walipokuwa na maktaba moja wapo kubwa barani Africa kama si duniani hadi sasa ambapo zipo viganjani mwetu kwa njia ya playlist. Na kwenye playlist yetu leo tupo na mhadhiri toka chuo kikuu cha mtaa Vioxii Dedee akituletea Maktaba Ya Mitaa (Street Library) ambayo ni albam yake ya pili kuachia tangu ajitose kwenye ulingo wa mziki.
Vioxii Dede ambaye alizaliwa kule Kericho, Kenya kabla ya kuanza kuishi mji wa rap kule Nairobi yaani Dandora Hip Hop City akiwa na umri mdogo wa miaka minne. Alizaliwa Victor Otieno Dede na alijikuta akipenda mziki baada ya mamake mpendwa kuanza kununua cassettes za mziki.
Aliweza kuingia studio 2006 baada ya kuanza kuandika mashairi yake mwenyewe na kwenye mazingira haya uandishi wake ulianza kuegemea sana mtindo wa Hip Hop baada ya miziki ya akina DMX, Common, Coolio, Tupac Shakur, Poxi Presha na Cool James Mtoto Wa Dandu kufika maskioni mwake.
Aliweza kuangusha mradi wake kwa kwanza kwa jina Huru Kwa Minyororo kabla ya kuachia albam yake ya pili Maktaba Ya Mitaa 2018. Maktaba Ya Mitaa kama jina linavyo jieleza ni albam ambayo nia yake inashahabiana na malengo ya maktaba. Mradi huu uliundwa kwa nia ya kuhifadhi matukio mbali mbali kwa njia ya audio na kwenye albam hii hususan yale aliyoyaona Vioxi na kuyapitia.
Mradi huu wa Maktaba Ya Mitaa pia ulikua na ma emcee waalikwa kama vile Kitu Sewer, Zakah Wenyeji, Nikki Mbishi(Tz), Nash MC(TZ), Nafsi Huru, P The Mc(Tz), Romi Swahili, Trabolee, Tonicah Wenzo (Denmark) Eskr One(Canada) Lafam, Dynamizoh, Ndocha Ziki safi,Labalaa, Ordinareh Bingwa, Ketina pamoja na Gsp Conscious (Tz).
Vioxii ambaye jina lake lina maanisha V-irtuous I –nspirational, O-ptimistic, X-extreme I-nfuence anaanza kuonesha uwezo wake pindi albam inapoanza kwa njia ya story telling kwenye kama vile Natoka Jela, Nisamehe Mama pamoja na Rafiki. Kwenye Natoka Jela Dede anatusimulia story ya jamaa mmoja anaetoka jela baada ya kukaa jela miaka mikumi. Vioxi anaongea na mwanae kwenye mdundo mzuka sana ambao kuna violin wazimu sana inayomsaidia Vioxi kufungua hisia zake. Madini kibao yanapatikana kwenye wimbo huu kama vile kwenye wimbo ya Nisamehe Mama.
Mapenzi, mahusiano na changamoto zake, mimba za utotoni, uavyaji wa mimba, maamuzi na ushauri mbaya maishani pamoja na maswala ya msongo wa mawazo pamoja na maswala ya kujiua yanapata fursa kuzungumziwa kwenye wimbo wa Maria. Hapa ndipo unaonekana uwezo wa Vioxi kutumia njia ya hadithi kutufunza vingi ndani ya beti moja.
Kwenye wimbo wa 5 Star General Vioxi kama ilivyo kawaida ya emcee anachukua mda kidogo kujigamba kuhusu uwezo wake na pia anatupatia historia ya maisha yake japo kwa uchache.
Uwezo wa Vioxi kupaa na mdundo wowote pia unaonekana dhahiri pale anapochana kwenye midundo ya mziki wa Reggae na Ragga kwenye nyimbo kama Ghetto Youth, Gazeti Ya Mitaa pamoja na Maombi.
Kwenye Ghetto Youth akiwa na Dynamizoh na Sabrina d’Avirro Vioxi anachukua mda ili aweze kuongea na yanki wa Africa akiwaambia;
“Dear toto wa Africa asikuambie mtu hauwezi/
Ndoto zako zitatimika, you can be what you wanna be kama Nyong’o Lupita/
Tia bidii kuwa persistent siku moja utafika/
Chuki, roho mbaya tunazika futi sita/
Uhalifu na ma dree kila siku piga vita/
Marafiki wabaya kaa mbali nao maelfu mita/
Haijalishi wapi unapotoka positivity wakilisha/
G.O.D. ako nawe ana tizama struggle yako/
No matter what you going through utafunguliwa mlango/
Fanya vitu taratibu kila siku kuwa na mpango/
And sure naku assure wee ndio Tarzan kwa hii jungle/”
Wimbo mzuka sana kwani hata kiitikio kinakuwacha na positive vibes sana. Moja ya wimbo niliopenda toka kwa mradi huu.
Kifo ni mada iliyogusiwa kwenye nyimbo mbili; Kifo ambao unapigwa kwenye mdundo bouncy sana na gita kama za ki South America huku Vioxii akiongelea vile kifo kiligusa familia yao walipo mpoteza dada yake mkubwa na kuwaacha na majonzi.
Pia na kwenye wimbo wa Isiwe Leo ambao unamkuta Vioxii akiomba kikombe cha mauti kiahirishwe toka kwake na kije tu pale atakapo fanikisha malengo na ndoto.
Umuhimu wa waandishi na mwandishi umegusiwa kwenye nyimbo kadhaa ambazo pia zinagusia maswala ya historia ya mtu mweusi na mwafrika pia kwenye Maandishi Kwenye Ukuta, Historia Nyeusi, Ukombozi Wa Africa na Gazeti Ya Mtaa. Vioxii, Trabolee pamoja na Romi Swahili wanashirikiana vyema kwenye wimbo Maandishi Kwenye Ukuta watukumbusha kuwa lazima tujue kusoma ishara za nyakati.
Mradi huu ni kumbukumbu nzuri kwenye tasnia ya Kenya sio tu Kenya bali hata Mashariki Afrika au kokote kule Kiswahili kinapo ongelewa. Mada na hoja zilizo guswa hapo ndani ni mada nzito zinazoonesha uhalisia wa maisha si tu ya Vioxii bali yetu pia. Mda ukiwadia na tukaamua kuunda maktaba ya audio mradi huu lazma utakuwa mmoja wa miradi tutakayoihifadhi kwenye Maktaba Ya Mitaa.
Kupata nakala yako ya albam gusa link hii:
HustleSasaShop: VioxiiDede
Au wasiliana na Vioxii moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii:
WhatsApp: +254714883998
Facebook: Vioxii Dede
Instagram: vioxiidede
Twitter: vioxii dede