Msanii: Wabeti
EP: Ukubwa
Tarehe iliyotoka: 11.02.2021
Nyimbo: 6
Wapiga midundo na ma producer: Young Ghost Kifaa, 10th Wonder, Ebube, Jerry Mtata
Studio: Action Records

Ukubwa, dawa! Wahenga hawakukosea waliponena maneno haya. Hivyo Basi, kuonesha kua wameshakua, vijana wawili toka Kahama waliungana na kuunda timu ya waandika mashairi ili kututengenezea dawa.

Dawa yenyewe waliiunda kwa mfumo wa kuandika mashairi, kwa mfumo wa kuweka mashairi kwenye midundo na mwisho kwa kutumia kinasa ili kuhakikisha kuwa tunawasikia vizuri popote pale tulipo ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

“Wabeti” kama wanavyojiita vijana hawa wawili ni “Papaa Frege” (Freddy Fabian) na “Bad Ngundo” (Salum Said Hamad) na kilichowaleta ni upendo wao wa kuandika beti za mashairi hivyo basi wakajiita Wabeti yaani waandishi wa beti. Japokuwa EP hii iliandikwa pakubwa na ma emcee hawa wawili, pia waliwashirikisha Adam Shule Kongwe ambaye alionesha umakini wake kiuandishi kwenye track iitwayo “Ukweli” ilhali Bless P naye alitupia ma vocal kwenye mdundo uliobeba jina la album Ukubwa. Wote hawa walizingatia vigezo na masharti ya EP hii kwa kuhakikisha kuwa walichokileta kwa mradi ni cha hali ya juu.

Ukubwa ambayo imebeba jina la mradi ndio single iinayotufungulia mradi huu. Kwenye mdundo wa Jerry Mtata, Bad anatufungulia na vesi ya kwanza akisema,

“Ukubwa sio kufoka kwa madogo/
Ukubwa ni kusota kama dojo/
Sio ndevu sio mwili jumba/
Mtu mzima ni mwerevu hii siri tunza/
Mtu mzima anatambua baada ya maisha ni kifo/
Na hapo ndipo anagundua ibada nzito/
Itamfaa, itampeleka pema/
Hana maneno ya kinyaa anabagua cha kusema/
Haongei kufurahisha genge/
Akiongea ni busara hana visa, mbwembwe,
Mkubwa hana wenge/”

Kiitikio toka kwa Bless P pia ni cha kiwango na unajua kuwa ujio wake kwa mradi huu pia ulikua wa maana.
Kwenye vesi ya pili ya single hii Papaa Frege naye pia anatupa mtazamo wake kuhusu Ukubwa akisema,

“Ukubwa jina kataa/
Aliye gizani we mpe nuru sio unazima na taa/
Na pia shukuru ukipewa sio unavimbaa kitaa/
Waombee dua, sio kuwacheka wanaoshinda na njaa/
Na ukishajua kua umekua jua kifua/
Kina beba siri nzito sio popote unatua/
Hata ukutane na magumu ndio ujue tayari ushakua/
Hakuna gumu linalo dumu ni kusali na dua/”

Ghost Kifaa na Ebube wanashika doria na kutupa mdundo murua wenye “Ukweli” mtupu na hapa emcee pekee aliyealikwa kuchana kwenye mradi huu, Shule Kongwe naye haachwi nyuma akisisitiza kuwa atasimama kidete na Ukweli akisema,

“Japo ni mchungu na unauma/
Siachi kuusema ili udumu kila muda/
Isitoshe si wengine hatuna pesa wala nguvu/
Nini kingine kitakacho tuweka huru/
Ukweli ndio silaha na bakabaka zangu/
Ninapopigana vita kwenye tabaka langu/
Ndio maana nikishika Mic sikwepeshi mambo/
Sijing’ati kiboya wala sipepesi macho/”
Nakupa, nagawa, sina paukwa pakawa/
Umeniathiri kama unga na nauvuta kama dawa/
Kisha nautumia kunyosha vilivyo bend/
Kutukuza vitu vya kishujaa visivyo trend/
Nausambaza na unatapakaa kote/
Zilipo jaa blunder na blah blah zote/
Onyo kwa waongo wote Ile siku inakuja/
ya Ukweli kutawala na uongo kuanguka/
Shule!”

“Msichoke” ndio track ya tatu kwenye EP ambayo inatutia moyo hata tunapopitia magumu kwenye mdundo ambapo gita kutoka Mali aina ya Ngoni linasikika vizuri wawili hawa wanapo tutia moyo.
“Kesho” inafuata kwenye mdundo wa Ghost Kifaa na Mr. Boombap mwenyewe 10th Wonder wanapo tupa tahadhari kuhusu kufanya mipango kwa kusema, “Inshallah/ tuiwazapo kesho” kwa lolote lile tunalo lipanga. Wachukua mikopo wanapewa onyo kwenye wimbo huu akisema Bad,

“Ikiwa kama una deni usiseme kesho nitalipa, Sema nikijaliwa uhai /
Kama nikifanikiwa, kesho nitarejesha utapokuja kudai”

Nae Papaa Frege anatupa mtazamo wake akisema,

“Nipo leo, nashkuru nimevuka jana/
Sitakufuru wapo walioitaka ikashindikana/
Wapo walioitaka nuru, wakaomba na haikuwezekana/
Lakini haimaanishi kwamba Mungu hakuwatazama!”

Mradi unamalizika na single ya “Sio Hip Hop” ikifuatiwa na “Orijino Gemu” ambapo umahiri wa muunda mdundo Ghost Kifaa unazidi kuonekana. Sio Hip Hop inatupa tahadhari kuhusu maisha ambayo watu wanadhania mwana hip hop anapaswa kuishi ili aitwe mwana hip hop kama vile kutumia madawa ya kulevya na ganja. Orijino Gemu inatuhimiza turudi kwenye uhalisia wa hip hop kwa kuwainua wana hip hop bila shuruti kama wewe ni shabiki au presenter wa redio.

Papaa Frege anawapa onyo akisema,

“Sicheki na presenter anayezingua/
hutaki cheza kazi yangu acha tu wahuni wataisakua/
Popote wataitafuta wataipakua/
Na bado kiharakati ki itikadi mtaani napata tour/
Yee najua unawaza pesa mzee/
Huwezi piga zangu ukaacha za Vanesa Mdee/
Nakupa kazi na unauliza maswali ya kiwaki/
“Frege umejipangaje?”, “Nimepanga mitaa ya kati!” /

Anavyomjibu presenter kimkato lazma utakubali kuwa Wabeti ni wacheshi.

Ukubwa EP ni mradi uliokamilika, kila wimbo uliopo ndani ya mradi huu umeandikwa kwa dhamira na lengo na wabeti wote wanapoangusha mistari yao wanahakikisha wanachochana kimeshiba. Kila wimbo uliopo hapa ni mkubwa ki ujumbe na ki mdundo. Hakuna ngoma ya kuruka hapa na msikilizaji lazma ataguswa na Ukubwa wa EP hii.