Albam: Nondo
Msanii: Watema Nondo
Tarehe iliyotoka: 09.08.2020
Nyimbo: 12
Ma Producer na waunda midundo: Sigger, Freddy Saganda, Bano Stylez
Studio: Paradise Apple
Watema Nondo ni familia inayo undwa na wachanaji tofauti tofauti toka Tanzania wakiwemo; Songa, Ado Tembo, Nick Maujanja, Sosa, Kay Wa Mapacha, Kugu, Freddy Saganda, De La P, Mau Kolimba,Magazi Juto, WyName, Pochaz,Black Wa Uswazi pamoja na ma producer Saint Pio, Bano Stylez na Sigger.
Mwaka jana kundi hili liliacha mradi wao unaokwenda kwa jina Nondo uliotolewa rasmi na studio za Paradise Apple.
Nondo kitaalum zinaitwa bars, steel bars au hata reinforcing bars (Rebar) na hutumika kuongeza nguvu kwenye ujenzi kwa mfano misingi ya nyumba. Pia kwenye mziki wa Hip Hop, bars lina maanisha “verse”, vesi au beti. Hivyo ni kusema toka kwenye maana hizi mbili Watema Nondo wametoa album iitwayo Nondo yaani mradi ulio na mashairi yenye nguvu na uimara.
Nondo zinazo tengeneza mradi huu ni za uhakika zikiwepo nondo zinazo ongelea imani zetu kwa mfano kwenye nyimbo iitwayo Asante Mungu inayo tufungulia mradi baada ya utangulizi. De La P anasema, “I’m closer to nature/ That’s why I’m closer to the creator.” kuonyesha mahusiano yake na muumba wake yapoje. Mada hii ya imani inaongelewa tena kwa undani na Sosa kwenye ndimbo iitwayo Uhuru Wa Manyani ambapo emcee huyu anahoji kwa undani swala la imani. Sigger anaunda mdundo wenye sauti za mzuka au mizimu. Sosa anahoji hivi,
“Mungu ni nani? Au nakufuru kiimani niache? /
Mungu ni nini? Ni mtego kichwani ulio pahala pake/
Kuhusu kumjua Mungu, nadharia chungu za wachache/
Mungu mwenye hekima, binadamu wote si wa kwake/
Unaumizwa unasamehe kisha unamuachia Mungu/
Unajiumizi aliye kuumiza mzee amuogopi Mungu/
Mafungu ya adui yana windana kama Chui na Nyumbu/
Visasi mpaka siku ya kiama mpaka roho ina ukungu/
Kuamini Mungu hayupo kiini cha kukata tamaa/
Haujapata unacho kiomba, labda unateswa na njaa/
Unacho kiona watu wanamtumia Mungu kukuhada/
Au rizki kwa mafungu tu Mungu huziandaa/”
Maadui Zetu ni nyimbo ya pili kwenye mradi huu na mdundo wake umeundwa ki West Coast kule America ambapo Kay Wa Mapacha pamoja na Kugu wanaungana kutuwachia mambo yakutafakari.. Mashairi ya Kugu yamesimama sana kwenye mdundo huu akionyesha kua si kila mtu anakuombea mema kwenye maisha yako. Anasema,
“Hao, hawapendi tuzunguke/
Mioyoni mwao nia yao wazee game tuisuse/
Kwenye kwa mafanikio, kamwe tusiguse/
Zaidi na zaidi wanaomba sisi tufe/”
“Uanaume sio kichwa kama usmamii shows” ndio mistari unayo fungua nyimbo ya tatu iitwayo Being a Man. Ni nyimbo inayo hamasisha wanaume kuwajibika maishani mwao. Nyimbo hii murua inampa motisha mwanamme yoyote kuwajibika vilivyo kupitia madini kibao wanayo wachia ma emcee Ado Tembo, Magazijuto na Songa. Gita za producer Freddy Saganda ni tamu sana kwenye mdundo huu na Songa anazidi kusisitiza kua,
“Uanaume sio kuwavua chupi ma binti/
Tafuta mkwanja ka’ vile unasotea madini/
Au Moran kama una Ng’ombe kapotea zizini/
Na sio ukiziotea tuu, unangojea kuzini/
Wakikwambia una mimba yako unapotea jijini/
Jali family, uwe maskini au uwe tajiri/
Uskimbie majukumu, chamuhimu ni kuyakabili/”
“Being a man ni ku hussle/ Being a man ni ku struggle” dada anaye imba kiitikio anatusisitizia.
Album hii pia inatupa mtazamo kuhusu maisha ya ma emcee waliopo handakini na wale ambao wanaonekana ma superstar na pia umuhimu wa kuangalia mistari ya ma emcee tunao wasifia na kama wanaisha maisha ya kweli au unafiki. Nyimbo 4 kwenye mradi huu zilizo ongelea mada hii ni Mainstream ikichanwa na Nick Maujanja, Tofauti Kidogo ikiwashirikisha ma emcee Ado Tembo, Songa, Kay Wa Mapacha pamoja na Sosa. Vile vile nyimbo zinazo beba jina la albam Tema Nondo na Nondo na Uisogelee Mic ni nondo tupu! Kwenye Mainstream Nick Maujanja kwa ucheshi anarusha madongo kwa ma emcee kanjanja akisema,
“Mikataba yote ya kipuzi/
Ndio maana hata nyi wenye ni wapuuzi/
Alipwe mtu wa kati, amlipe mtu wa kati, ndio aje akulipe laki ni ushuzi/”
Pia anawakejeli ma emcee kwa kuishi maisha fake anapo hoji,
“Baada ya video una rudi home na Uber/
Fake it till you make it, msongo wa mawazo huja/”
Nyimbo hii imejaa wosia na tahadhari kua maisha tunayo sifia ya ma star wengi ni fake. Vile vile Tofauti Kidogo inaendeleza mada hii kwa kuonyesha vile emcee wa kweli yupo tofauti sana na ma rapper wako wa kawaida. Ado Tembo anasema,
“Vilinge vingi ukuda huja kwenye cash na who’s the best/
Tapes nyingi, cover kubwa ndani ni poor deliverance/
Ukileta njaa utakula bench/
Hii ligi ni handaki hutaki ligi uza mech/”
Kay Wa Mapacha nae anakuonyesha utofauti wake na ma emcee gushi anaposema,
“Mi ni legendary kama Dikembe Mutombo/
Mashairi yana wanasa kama ngada za Colombo/”
Pia anaonyesha vile yee ni wakitambo sana akitukumbushia enzi za floppy disc akisema,
“Enzi na enzi hadi leo na trendy/
Toka enzi zile floppy disc Transcendi/”
Kwenye vesi la mwisho Sosa anatufunza kuhusu vigezo vya underground emcee ni vipi akisema,
“Kua underground emcee ni kua na jamii/
Elimisha uburudishe ni kazi ya emcee/
Acha kutisha watu mang’aa haujui hataa fasihi/
Kujivisha ukuu sio maisha ya ulimbukeni ya msanii/”
Kila emcee kwenye nyimbo zilizotajwa hapo juu amesimama kwa zamu yake kimashairi.
Mradi huu ni moto mwanzo mwisho na nyimbo kama Let It Be ni nondo tupu,
“Ku rap nako wito/
Ni kama doctor, mi ni doctor wa Kigambonito”, anasema Jos Mitambo ambae pia ana mistari ya uchesi anaposema “Ukimfumania mkeo usiue, jiue/Hapo ndipo kifo kimewatenganisha, ujue”
Naiogopa Kesho inampata emcee Pochaz akiongelee kuhusu kifo kwenye biti ambalo ni gita tu ikisindikizwa na sauti nyororo ya binti Miss Geez. Pochaz anajaribu kupeleka mda mbele kama alivyo fanya Kinya Mistari kwenye Mda na kutuwaisha kufa akisema,
“Nikiwa hai ni mwanadamu ila nikifa ni maiti/
Sifai kitandani, sebuleni, sifai kwa kiti/
Siwezi ita, sisikiki sisikii na siitiki/
Mwili hauko nami nguo gani itanifiti/
Kiroho nafsi itaishi/
Mwili utazikwa nanyi wanadamu wazandiki/
Kila mwanaharamu atapitia kisanga hiki/
Huwezi rudi mwili uko chini 6 feet/”
De La P, Mau Kolimba na Saint Pio wanaungana kwenye nyimbo iitwayo Maradhi ambayo mistari ni tiba toka kwa ma emcee hawa. Maneno mazuri ya ukweli ni dawa na sauti murua ya dada Mau Kolimba inaishusha taratibu kooni mwetu.
Mradi huu umejaa nondo zitakazo muwezesha yoyote anae penda mashairi yaliyo enda shule kuukubali. Kama vile kupiga nondo ni muhimu kwa afya yako kwa mujibu wa ma bwana afya, Nondo ya Watema Nondo ni muhimu kwa shabiki yoyote anae kusanya albam za Hip Hop. Wacha nipige Nondo.
Nondo album yote (Audio) - https://mdundo.com/a/148820
Tema Nondo (Video) – https://www.youtube.com/watch?v=bHkNZDpFoGM
Tofauti kidogo (Video) - https://www.youtube.com/watch?v=SQ_RRdSBUm4
