Msanii: Watunza Misingi
Album: Afrika (Alkebulan)
Tarehe iliyotoka: 15.12.2018
Nyimbo: 18
Producers: JEgalla, 10th Wonder, Abby MP, Blackfire, Dela P, Issam, Troo Frunk, Momoko, Bin Laden
Ma emcee walioshiriki: Dela P, Albeez, Ze Pipo, Ras Muhemusi, Eddy MC, Vak Mtatu, Lugombo Makanta, Levis Makanta, Jadah Makanta, Siga Nyox, Sarafu(coin X), Kiraka Tosh, Kaa Feel, Kella B, Adam Shule Kongwe, Javan, MaJaNTA, Ndevu emcee, Mad Kachaa, Jedikouga, Ramoo, ABC, Lady Yoo, Gome Jero, Pop Dyz, Funda Ndaga, Sekesi, Kay Maujanja, Adamoe MaKaNTa

Toka enzi za jadi historia ya muafrika na Afrika kwa ujumla imekuwa ikitunzwa na kuhifadhiwa kwa ajlli ya vizazi vijavyo kupitia njia tofauti tofauti zikiwemo; uchoraji, vinyago, mashairi, upigaji ngoma, misitu walipoabudia mababu zetu kuhifadhiwa na nyimbo. Kupitia nyimbo walizotufunza wazazi wetu waafrika waliweza kuhifadhi historia yao kwa kuimba ili vizazi vijavyo viweze kujua vilipotokea.
Watunza Misingi pia nao wameamua kuendeleza utamaduni huu wa kutunza kumbukumbu ya historia ya Afrika kwa kupitia nyimbo, hususan aina ya Hip Hop, kwani walisema wazee wetu kuwa, “Muacha mila ni mtumwa”.

Watunza Misingi ni vijana walioamua kutafuta ukweli na huru ya mtu mweusi (muafrika) kiuchumi, kiimani, kiutamaduni kwa kuitazama Afrika ya kale. Vijana hawa kipindi cha 2013 walikuwa wanatumia jukwaa liitwalo Rebels For Revolution pale Facebook hadi hapo 2016 wakiwa kwenye vikao vyao walipo afikiana kufanya mradi utakaoshirikisha makundi yote chanya katika kuleta mapinduzi ya kijamii na ndipo hapo Watunza Misingi ilipo ota mizizi yake. Mwaka huo pia ndio Watunza Misingi waliweza kurekodi wimbo wao wa kwanza kule Mbeya uitwao Watunza Misingi Part 1. Kwenye kundi hili Watunza Misingi wote wanatambuana kama “Generals” na waliohusika kwa vitendo kwa namna yeyote wanatambulika kama “Frontline Generals”.

Je mtunza misingi ni nani? Mtunza misingi ni mtu yoyote anaesimamia ukweli katika Hip Hop, ni mtu anayetafuta aufrika wake wa asili popote alipo pale duniani.

Mnamo mwaka 2018 Watunza Misingi waliamua kuachia mradi wao wa kwanza ikiwa ni albam iliyokwenda kwa jina la Afrika (Alkebulan).Mimi binafsi japokuwa nimependa historia sikuwahi jua kuwa Afrika hapo awali ilikuwa inaitwa Alkebulan. Album hii ya Afrika (Alkebulan) ilisisitiza nia ya ma emcee hawa ya kuenzi Afrika yetu ya awali zikiwemo mila zetu, tamaduni zetu na njia zetu asilia.

Jalada la Afrika (Alkebulan) ni zuri sana linalong’aa kwa rangi ya dhahabu kama ishara kuwa tulipotoka na tulipo ni pahala pa thamani kubwa sana na ndipo wanajaribu kutushawishi Watunza Misingi turudie Afrika yetu ya zamani. Pia Jalada la albam linaashiria kuwa tutakachokipata ndani ya albam hii ni cha thamani; madini ya kupanua mawazo ki historia na kimaisha.

Albam hii inaanza na utangulizi mzuri uitwao “Bara Langu Pt 1” toka kwa Ras Muhemusi anayetupa historia fupi kwa mtindo wake wa uchanaji-mashairi huku maneno yakisindikizwa na kinanda na Zeze kwa nyuma.

Wimbo wa kwanza ambao ni moja ya nyimbo ninazozipenda toka album hii, “Nakupigania (Afrika)” ulio pikwa vizuri na Abby MP ndio unatufungulia albam pamoja na emcee Adam Shule Kongwe. Adam anaonesha vile anavyoithamini Afrika kwa kusema,

“Ninakupa, na Nitakupa Sifa Mara Zote/
Ya Kwamba Umebarikiwa Kupita Mabara Yote/
Hebu Tafuta Kwa Kutazama/
Sidhani Kama Utakuta, Hakuna wa Kufanana/
Historia Yako Naijua Ni Kubwa Sana/
Tatizo Walioandika Wanazusha Wanatuchanganya/”

Kisha wanafuatia akina Javan, Eddy Mc, Majanta na Dambwe wakipigana vita “Dhidi ya Dhuluma” kabla ya Lugombo kufungua vesi ya kwanza kwenye wimbo unao sisitiza umoja kwenye kundi lao, “Watunza Misingi Part 1” akiwa na ma emcee kibao akisema, “Hatuendi na Wakati, Tunaenda na misingi”.

Producer Troo Funk kisha anachukua doria kwenye wimbo “Amsha, Unganisha, Tekeleza” kabla ya Popdyz Mc na Gome Jero ku “Sambaza Upendo” wakisema,

“Usijivunie mali na pesa ulizonazo/
Ujue maisha ni safari utawachana nazo”

Kwenye wimbo wa “Jeshi La Mungu” anapatikana emcee Lady Yoo na katikati la kundi la Watunza Misingi wakiume anaachia mistari mikali akisema,

“Kama kijana nikiwaza ni shule na kazi pia/
Malengo juhudi, nakaza naweka nia/
Kipi cha kwanza kujenga na familia/
Tafakari sana ujana kwa kutulia/”

Kwenye wimbo huu pia yupo first lady wa Watunza Misingi Jadah MaKaNTa.

“Bara Langu Pt 2” ni wimbo unaowakutanisha ma emcee KaaFeel, Gome Jero, Adam Shule Kongwe na Kiraka Tosh (From Kwembe). Hii chemistry ya KaaFeel na Kiraka Tosh inaonekana kwenye wimbo mzuri aliouunda tena Abby MP (Multi-Purpose) uitwao “Sauti ya Mamlaka” ambao una sauti za Saxophone kwa nyuma na wote wanaunga kwa sauti moja wakisema,

“Hii ni nguvu ya akili iliyoambatana na sauti/
Utakufa mwili sauti itashinda mauti/
Mtabaki mnaijadili hii sauti hamuifuti/
Hii Sauti ya Mamlaka Kiwashe Acha Kunyuti”

“Siku ya Mapinduzi” ni wimbo unaoongelea siku ya ukombozi wa Afrika yetu na unapigwa juu ya kinanda cha ISSAM.

Dela P na Al beez wanaunga kwenye wimbo “Afrika damuni” akisema Dela P,

“Afrika ni vazi wameshalitia doa/
Hawajui Afrika yai na kesho litatotoa/
Lengo la Babylon tayari nishagundua/
Ni kummaliza mtoto wa Afrika kabla hajakua/
Kwa vidonge anavyomezeshwa mama wakati wa mimba/
Sindano wanazowachoma watoto ni kama mwiba/”

Gita la Dela P linapita taratibu juu ya biti lililokwenda shule.
“Rejea Asili” ukuwashirikisha Wanaboma ni wimbo ambao sauti ya kwaya inaskika na kutoa masikitiko na pia msukumo kuwa lazma turudie vitu vyetu vya awali. Kella B hapa anasema,

“Kutoufahamu utamaduni wako ni kama mti uliokosa mizizi/
Kweli ipo kazi/ Hivi watoto wanapatikana wapi? Tuliwauliza wazazi/
Mtoto wa miaka miwili wa siku hizi utamwambia nini? Mambo yako wazi”

Kaa Feel na dada Jadah MaKaNTa wanakutana tena kwenye “Mtaji wa Mapinduzi” ili kuenzi mchango wa wanawake kwenye mapinduzi ya maisha yetu. Jadah analainisha sauti ngumu ya mistari ya Kaa Feel kwa sauti yake nyororo kwenye kiitikio.

KaaFeel na “Pacha” wake ki mistari Kiraka Tosh wanaungana tena wakiwa na muimbaji Koku kwenye wimbo “Ujamaa” kabla ya “Mapacha” hawa kuungana tena wakiwa na Popdyz kwenye “Wapo Uchi”. Chemistry ya KaaFeel na Kiraka Tosh ni kama ile ya Redman na Methodman au "Mkoloni' na "Dr John" wa kundi la Wagosi wa Kaya. Hata single ya kwanza ya albam hii iitwayo “Rejea Alkebulan” inaonyesha maelewano mazuri ya wawili hawa.
Troo Funk anatuachia dude flani la ki Funk hivi zuri lenye vinanda noma sana kwenye “Ninachokijua”, na ni nani wengine walilitendea haki kama sii KaaFeel na Kiraka Tosh wakiwa na Ramoo. Ramoo anang’aa hapa na haachwi nyuma kimistari akisema,

“Ajira hakuna na pesa hakuna/
Hali sio shwari home, jiko limenuna/
Mvua zimebuma na shambani sijavuna/
Natafakari shida zangu nauchuna/
Mi ninachofanya ni kuvumilia mengi/
Hata ka sipendi, kuiba siwezi/
Siwazi ma Benzi, siwazi mapenzi/
Mtoto sipendezi ndio maana hawaniiti bebi”

Album inamalizia na wimbo uitwao “Watunza Misingi Pt2” ambapo wanatufungia mradi akina Adam Shule Kongwe, Levis MakaNTa, Mad Kachaa, Javan na Ze Pipo. Hii ndio single pekee ambapo emcee anadondosha vesi kwa lugha ya ung’eng’e.

Album hii ni kozi fulu kuhusu historia ya Afrika na waafrika na inatuhimiza kujipenda, kujithamini na kujiinua. Kama album za akina 2Pac, Rapsody, Jay Z na Kanye West pamoja na Kendrik Lamar zinafunzwa vyuo vikuu huko America huku Tanzania pamoja na Afrika kiujumla pengine Afrika (Alkebulan) ingepaswa kufunzwa vyuo vyetu vikuu na kwa lugha yetu tunayoienzi ya Kiswahili na mtu akahitimu na shahada.