White Mkatili nilianza kumskia na kumfuatilia baada ya emcee mwenzake Fivara (Nyati) kumpa shavu kwa ku promote mradi wake Walimwengu kwenye mtandao wa kijamii Facebook. Moja kwa moja nilizama kule Boomplay alipotupia huo mradi wake na kuanza kuskiliza kazi zake. Pia nilienda YouTube ili kucheki vichupa vyake kwani nilichokiskia pale Boomplay kilinivutia.
Baada ya kumskia kwa mda nikaona ni vyema nimtafute tuyajenge na tufanye mahojiano nae. Cha kwanza nilichotaka kujua na nilichokua nakiwaza sana ni kujua kwa nini kaamua kujiita Mkatili kwani maana ya moja kwa moja ni mtu mwenye unyama ndani yake.
Swali hili na mengine mengi yalijibiwa nilipofanya mahojiano nae. Karibu sana msomaji ili nawe pia upate kujifunza kama mimi nilivyojifunza toka kwa White Mkatili.
Karibuni sana!
Karibu sana Micshariki Africa kaka White Mkatili. Kwanza tuanze kwa kukufahamu jina ni nani na unatokea wapi?
Jina langu naitwa Hemedi Adam Waziri nimezaliwa Dodoma mwaka 1994 Tarehe 2 mwezi wa 12.
Mwaka 1999 wazazi wangu walihamia Dar Es Salaam.
White Mkatili ni jina la utata sasa? Jina hili ulilitoa wapi na we ni mkatili kweli?
White mkatili walinipa washikaji zangu. Nilipokua nikichana walikua wananiambia, “Wewe white (mweupe) halafu mkatili!” ndio nikawa White Mkatili. Baada ya hapo nikaona nitumie jina hilo japokua hapo mwanzoni nilikuwa najulikana kama Dizzo.
Ahahaha mimi ni mkatili kwenye michano yangu lakini kwenye maisha yangu halisi ni mtu wa amani tu.
Ukisikiliza album zangu utaelewa mimi napenda sana kuzungumzia maisha halisi ya mtanzania sana sana sisi wa hali ya chini na jamii yote kiujumla. Pia napenda kuelimisha jamii kupitia sanaa yangu.
Nipe Historia yako ya mziki,ulianzaje hadi kufikia ulipo kwa sasa? Hadi sasa una miradi mingapi, inaitwaje na ilitoka lini?
Mziki nimeanza kufanya rasmi mwaka 2005 na mwaka 2008 nikaingia studio nikiwa na kundi langu mbalo linajulikana kama Wawega. Tulifanya kazi mpaka mwaka 2014 likavunjika nikaanza kufanya kazi mwenyewe.
Mwaka huo 2014 nikaingia studio na kufanya wimbo nikiwa peke yangu niliouita Tafuta utapata na kisha baada ya hapo nikaandaa album yangu ya kwanza ambayo inaitwa Jamii Ya Malalamiko nikaitoa mwaka 2019 yenye nyimbo 8.
Baada ya hapo mwishoni wa mwaka 2019 nikatoa tena album yangu nyingine inayoitwa Nguvu nikiwa nimeshirikiana na Rasta Michael yenye nyimbo 11.
Baada ya hapo nikakaa mwaka mzima sikutoa album mpaka 2021 nikatoa album nyingine inayoitwa Walimwengu na sikukaa sana ndio nikaachia Ep yangu yenye nyimbo 5 inayoitwa Mudricky. Ep hii pia nimeitoa mwaka huu 2021.




White Mkatili mashairi yako hua yana malengo gani na yanamlenga nani?
Mashairi yangu huwa yanamlenga mtu yoyote sababu nyimbo zangu huwa naongelea vitu tofauti vinavyolenga jamii sana sana kwenye uelemishaji
Ni kipi kinachomtofautisha emcee wa handakini na rapper yoyote yule? Ni kipi wafanye ma emcee wa handakini ili waweze kupanua soko lao?
Msanii wa handaki kwanza huwa hapangiwi cha kuimba na msanii wa handaki siku zote huwa ni msema ukweli na sio waigiza maisha yani huwa wanaishi maisha yao halisi. Wasanii wengi watumwa kwa kutaka umaarufu au pesa za haraka na ndio maana wengi wao wanaandika nyimbo ambazo hazina elimu yoyote zaidi ya kushawishi ngono, kutokuwa wamoja na kujiona mimi bora wakati hakuna unachofanya kwenye jamii zaidi ya kupotosha.
Bro Kefa nataka nikuambie kitu kimoja, ma bro wengi ambao wanajifanya wana misingi kiundani maisha yao daaaaah tofauti kabisa na wanachokiimba kwenye ngoma zao. Ma brother waliotutangulia ndio hawana support kabisa kwa sisi ambao tunakuja na unakuta hao wasanii wadogo wana support kazi za wakubwa lakini wakubwa kutu support sisi ni adimu sana.
Kwanza wanataka utubu ndio wakukubali wanaleta mambo yale yale ya kitumwa bro, mambo ya makundi makundi, ya kinafiki ndio yanaua game ya Hip Hop. Kwenye media hatusikii Hip Hop yenyewe ya kuelimisha
Kwa upande wa kupenya sokoni huwa unatumia mbinu gani kuuza mziki wako?
Mimi mziki wangu nauza kwa njia tofauti kwenye platform (za streaming kama vile Boomplay), pia kwa kuuza nakala kwa njia ya CD au pia mtu akitaka namtumia kwenye WhatsApp au email (barua pepe) kwa wepesi zaidi.
White Mkatili kando na mziki unajishughulisha na kitu gani kingine ili kuweza kujikimu kimaisha?
Kwa sasa sina kazi nyingine zaidi ya mziki ila pia mimi ni fundi wa A/C za magari.
Unapotaka kuchagua muunda mdundo au producer, emcee au hata mwanamziki wa kufanya naye kazi huwa unaangalia vigezo vipi kama njia ya kujiridhisha kuwa utakayemchukua atakufaa?
Naangalia producer mwenye uwezo wa kutengeneza beat. Sauti naweza kuingiza popote pale kikubwa mdundo kwanza. Kama msanii wa kuimba huwa naangalia uwezo wake na je kama atakaa kwenye wimbo ninaotaka kumshirikisha basi tunapiga kazi.
We huandika mashairi kabla ya kuchagua mdundo au huwa unapata mdundo kisha unapata mada ya kuandika?
Mimi huwa naandika kama nikikutana na beat liko poa nafanya. Pia ikitokea kuna mdundo basi nauchorea. Mimi huwa sina ratiba maalum, ki vyovyote naweza kuandaa wimbo.
Kitu nimeona na wewe ni kuwa umefanikiwa kuachia vichupa kadhaa kwa ajili ya ngoma zako? Umewezaje kufanikisha hili kwani nadhani kutengeneza video za mziki ni zina gharama kubwa? Je kuwa na video kumeongeza thamani gani kwenye mziki wako?
Tunajichanga kinachopatikana tunawekeza kwenye mziki na support kubwa inatoka kwa bro wangu Pablo Zungu kwani mara nyingi yeye ndiye ananisupport kwenye harakati zangu hata kwenda studio na mambo mengine zaidi.
Kufanya video kumeongeza mashabiki wengi kwenye mziki wangu kiukweli.
Wakati mwingine ma yanki kibao wangependa kuwa waimbaji, wachoraji au hata chochote kile kando na matarajio ya wazazi wao. Hili unalizungumziaje?
Kama wanaamua kufanya wafanye ila wasiache kufanya walichokuwa wanafanya wakataka kuingia kichwa kichwa tu kwani huku kunahitaji uvumilivu. Kuna mengi yanaendelea ukiwa nje ya mchezo huwezi kuyajua
Mbona video za ma emcee wa handakini huwa ngumu kuona zikichezwa kwenye station za tv? Changamoto nini? Nini kifanyike ili wao pia wapate nafasi kule au kuna mbadala wa hili?
Mara nyingi kukosekana kwa ubora wa video lakini hata video nyingine nzuri hawawezi kucheza hata ikichezwa week tu inatupwa mbali kama uliwapa elf 50 yako ndio imeisha hiyo. Hao wachezaji hizo video kwenye media waache kusikiliza wake zao kuwa wanataka nini waangalie jamii yote kiujumla sio mapenzi yao tu wenyewe.
Ndio maana leo underground kutoboa pasipo kubebwa na msanii mkubwa hapa bongo inakuwa ndoto. Yote ni utumwa tu na hao ma bro wanataka wawe wao tu kwenye game hawataki kuona vijana wanakuja kuwapita.
We angalia tu marapa wao wa sasa wanaotamba utasikia yupo na flani so ndio hivyo ubinafsi tu unafanya handakini kufikia malengo unakuwa kazi sana
Vijana wengi waliosoma wanapata changamoto za ajira ilhali wana karama walizopewa. Ungewaambia nini vijana hawa kwani matumaini yao yote kwa white collar jobs (kazi za kuajiriwa)?
Mimi nawaambia kusoma sio kufanikiwa bali ni ufunguo wa maisha so wasitegemee kuajiriwa tu hata kujiajiri inawezakana kufikia ndoto zao.
Shukrani sana White Mkatili kwa kukubali wito wetu. Neno lipi la mwisho ungependa kutuachia tukifika tamati ya gumzo letu
Kikubwa naweza kusema kwa wasanii wa Hip Hop ni tupendane haswa sisi wa handakini
Pia watu ambao watahitaji miradi yangu wanicheke
WhatsApp: +255687725761
Facebook: Whitemkatili Tz
Twitter: White mkatili
Instagram: white_mkatili