Ukaguzi Wa Albam: Walimwengu
Msanii: White Mkatili
Tarehe iliyotoka: 22/04/2021
Nyimbo: 10
Ma Producer na Wapiga Midundo: G Kifaa, Pinna, Turenga,
Mchanganya Sauti na Midudo: Pinna
Studio: Project Records, KB Records
Waswahili hawakukosea waliposema, “Asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu” ila hapo hapo emcee Adam Shule Kongwe kwenye wimbo wake Walimwengu toka kwa debut albam yake ANKO alitukumbushia kwamba, “Walimwengu na mambo yao, walimwengu noma sana mwanangu!”
White Mkatili aliamua kuingia booth mwaka huu kutupatia mradi wake wa tatu uendao kwa jina walimwengu ili kutuelewesha walimwenguni ni akina nani na wakoje na juhudi zake zikatupa mradi aliouita Walimwengu.
Mradi huu ambao umeundwa studio za Project records na KB records, unaanza na wimbo mzuka sana unaobeba jina la albam Walimwengu. Wimbo unaanza na gita likipiga taratibu kabla ya mdundo kuingia pamoja na kinanda mdogo mdogo. Walimwengu ni nani? White anaanza kwa kutueleza hili akisema,
“Ulimwengu ndani ya ulimwengu na walimwengu wenzangu/
Ndio sisi walimwengu tunamkufuru Mungu/”
Hivyo basi White anasema kuwa walimwengu ni yeye mimi na wewe hivyo mradi huu unatuhusu sisi sote. Kupitia wimbo huu White anatuonesha vile walimwengu wapo tofauti, wengine watakupenda, wengine watakuchukia, wengine watakua wanafiki, wengine watakua marafiki, wengine watakua maadui, wengine watakupotosha na hivyo basi kwenye kiitikio White anatupa tahadhari akisema,
“Asiyefunzwa na mamaye/ (Atafunzwa na ulimwengu mwili umetaka kwa shida aisee tukomae)
Ukiiba wakikukamata walimwengu/ (Ni mkong’oto na baada ya hapo kifuatacho ni moto)”
Wimbo wa pili kwenye albam hii Haile pia inaendelea na mada hii ya ulimwengu na walimwengu wake.
Changamoto za walimwengu zinaendelea kuongelewa kwenye nyimbo mbili tofauti ambapo White anaonyesha ukatili uliopo duniani kwa njia ya mashairi ya hadithi kwenye nyimbo mbili Hukumu Yangu akiwa na Nyuzi na Mariamu akiwa na Rasta Michael. Kwenye Mariamu White Mkatili anaonesha unyama uliojaa duniani pale binti kwa jina hilo anapopitia magumu kwenye ndoa yake kwa sababu ya kushindwa kupata mtoto. Changamoto zinazidi na anakimbia nyumbani na kubahatika kupata chaka la nyumbani kwa pastor flani ambaye pia anageuka mnyama na kumtaka ki mapenzi japokua kaoa na ana watoto watatu. Mariamu anaamua kukimbia usiku wa manane na kwa bahati mbaya ananajisiwa na kitendo hichi ndio kinampa mimba. Masaibu yaliyoje haya!
Kwenye Hukumu Yangu White Mkatili anatupa stori vile maisha yalimbadilikia ujanani alipokua mhuni flani na maisha yake mabaya yake kumpelekea kufungwa “nyundo tisa” au miaka 45! Maisha yalimfunza hadi alianza kujutia maisha yake ya awali kwani hata alihisi amemkosea mamake sana. Kwa kweli asiyefunzwa na mamae hufunzwa na walimwengu. Story hii inapigwa kwenye mdundo mzuka sana wenye vinanda na bass gita safi sana.
Kifo ni moja ya ishu ambazo walimwengu tunazijua na zinatuathiri. Emcee huyu pia alichukua kalamu na kuandika mashairi ya kuenzi watu wake wa karibu waliomtangulia mbele za haki na pia ma emcee wabongo walioaga dunia kama vile Andre K na Mac 2 Be. Kwenye mdundo ambao waeza dhania umeundwa na Pharell Williams wa The Neptunes White Mkatili anaomba tuweke Bendera Nusu Mlingoti kama njia ya kuwakumbuka waliotuacha.
Ulimwengu huu bila mziki ingekuaje? Je bila mziki wa Hip Hop je si ndio ingekua umepoa sana? Hivyo basi emcee huu kwenye mradi huu kwa kuliona hili na kujua kuwa walimwengu pia wanapatikana kwenye mziki wa Hip Hop basi hasiti kugusa palipo karibu na moyo wake. Kwenye nyimbo nne White anaongea na wana Hip Hop; Underground ulioundwa na Turenga ambao unaomkuta akiapa kuwa handakini ndipo alipoanzia, alipo kwa sasa na atakapokuwepo mpaka Yesu arudi kwenye mdundo mzuka sana. Pia anaendelea mada hii kwenye wimbo wa Msafara akiwa na Fivara pamoja na Nubi, Tour Za Mikoa akiwa na Gwanta na mwisho Hii Ni Hip Hop.
Msafara ni wimbo mzuka sana ambao ma emcee wote wanatema madini wakielezea mtazamo wa maisha ya wana Hip Hop, historia yake na wapi walipo wakongwe waliolianzisha game hili hapa bongo.
“Kwenye msafara na wengi walikuepo/
Ulipo change upepo wakapotea leo hawapo/
Nyingi changamoto/
Mafanikio ni siri nidhamu itakutoa ulipo/
R.I.P Mabovu wape mashavu wana Mchomvu/
Nusu kukata tamaa ile ni roho ya kiushujaa inaniambia tunasonga/
Kwa nguvu za Jah hakuna kulega tupa kule acha uwoga/
Tumepoteza marapa kibao/
Kwa powder bob nakaza msuli hii safari isiniache njia panda no ku surrender/
Halafu naipenda/
Naona makundi yanavunjika/
Sijui ni kwanini alafu mengine yanaunganika/”
Kwenye kiitikio Fivara anatupatia muhtasari mzuri wa maudhui ya wimbo huu akisema,
“Msafara wa hii sanaa/
Bado ngumu usiwaze kua kinara/
Ndugu waza majukumu/
Tutafika tu haijalishi kuna jambo/
Tutaskika tu kwani kinacho matter nidhamu/”
Pinna anashika doria kwenye mdundo wa singo ya mwisho One Day Yes wakati emcee White akituhakikishia kua tukifanya kitu cha maana na mda wetu na maisha yetu kila siku basi mafanikio lazma yatakuja.
Mradi huu ni mzuri sana ila kusema kweli mimi kuna maneno mengine kulingana na delivery ya uchanaji au pengine lafudhi ya emcee huyu yalikua yananipita ila sidhani kama ni mapungufu ya White bali ni mapungufu yangu na inanihamasisha kurudi na kuskia mradi huu tena na tena kwa umakini ili niweze kumuelewa na kuelewa mashairi yake vizuri zaidi. Mimi, wewe na White Mkatili ni Walimwengu.