Wise Genius

Mimi nilianza kumfahamu Wise Genius baada ya kununua mradi wa Pizzo Madawa, Panga Mbili. Hapa ndipo niliposkia kwa mara ya kwanza midundo inayotoka kwa producer huyu ambayo ilinivutia sana.

Baada ya kuskiza kazi zake toka kwa ma emcee wengine niliona ni vyema nimtafute niongee nae ili mimi na watu wengine waweze kumtambua Wise Genius kama namna moja ya kuonesha upendo kwa kazi nzuri na za hali ya juu anazotupatia sisi mashabiki wa underground Hip Hop.

Karibuni sana ili muweze kujifunza kitu kutoka kwa producer Wise Genius MD.

Wise Geniuz ni nani, kazaliwa wapi na anatokea/kupatikana wapi?

Wise Geniuz ni kijana mtanzania mwenye asili ya Mbeya nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Alizaliwa Jijini Arusha ambako familia anayotoka ilikuwa ikiishi na baadae kuhamia Mbeya ambako alipata kuwepo hadi wakati huu, kwa sasa anapatikana Jijini Mbeya.

Unaitwa nani rasmi?

Majina rasmi ya Wise Geniuz ni Nicholaus William Mwakalukwa

Kwa nini wajiita au waitwa Wise Genius? Jina lilikujaje? Na MD je lina maana gani?

Jina la Wise Geniuz nilipewa na watu wangu wa karibu niliokuwa nikishinda nao kipindi cha nyuma.

Lilianza jina Wise ambalo waanzilishi wa jina hilo ni watu wawili ambao ni Daniel Magehema pamoja na kaka yake Jeseph Magehema ambao nilikuwa karibu nao sana kwa wakati huo. Baadae liliongezeka Geniuz ambalo liliongezwa na rafiki mwingine anaeitwa Daniel Mbisse. Hivyo ndivyo lilivyo kamilika na kuwa Wise Geniuz

Kuhusu MD ni abbreviation ya Messiah Disciple. Sababu ya kuwa na hilo jina ni kwamba mimi ni mtu ambae najali sana hali ya kiroho (spirituality) na nakubaliana na Messiah katika perspective ya mtu na utu wake na ninaujenga utu wangu kwa mafundisho ya Messiah ambayo kubwa zaidi ni upendo.

Wise Genius unajishughulisha na nini kimaisha na kimziki?

Kimaisha na muziki ninajishughulisha na utayarishaji wa muziki hasa wa hip hop, katika studio za AMG jijini Mbeya.

Historia yako ki mziki ipoje? Ulianzaje shughuli ya u producer na ni kipi kilicho kupatia motisha kubaki hapo?

Historia yangu kimuziki: nimeanza kuwa karibu na muziki kwa kuanza kuusikiliza tangu utotoni, kwa asilimia kubwa nilikuwa nikisikiliza muziki wa hip hop, baadae nikaanza kuwa mdadisi sana kuhusiana na mziki kutaka kujua jinsi inavyotokea tokea mpaka wimbo unapatikana, early 2010's nikiwa na rafiki yangu Benedicto a.k.a Boika tulianza kujifunza utayarishaji wa muziki, nadharia ya mziki(music theory) na matumizi ya Digital Audio workstations zinazotumika kuandaa midundo ya muziki, uchakataji wa sauti za muziki na mengineyo.

Wakati huo tulikuwa tukijifunza kwa kupenda tu sio kwa lengo la kujihusisha kama wanamuziki. Wakati nikiendelea na mchakato huo na nikiwa naunda midundo watu niliokuwa nao karibu walitokea kupenda sana nilichokuwa nafanya na wakanipa msukumo wa kuanza kutekeleza rasmi shughuli za utayarishaji muziki.

Watu wenye mchango mkubwa kutoa msukumo huo ni Joseph Magehema, Daniel Magehema pamoja Emannuel ( Mwanakondoo) huyu ni Emcee pia.   Hawa walinishawishi nikanunua baadhi ya vifaa vya awali katika kurekodi muziki na tukaanza kuvitumia na mwamko ukawa mkubwa katika jamii yangu niliyokuwa nayo karibu nikajikuta nna deni la kutoa service ya namna hii.

Tueleze kidogo kuhusu mchango wako kwenye Hip Hop game ya bongo maana nimeona umekua kwenye hili game mda mrefu na umehusika kwenye miradi kibao?

Kuhusu mchango wangu kwenye game ya Hip Hop ya bongo ni kwamba najitahidi kuweka tone flani ya muziki iwe kati ya zilizopo ila wale wanaoshiriki muziki wangu na wanaouangazia na kuguswa nao ndio wanaweza wakawa na maelezo zaidi kulingana na wanavyoguswa na ninachokifanya katika Hip Hop ya bongo

Tueleze kidogo kuhusu production. Hua unapenda kutumia vifaa gani na software zipi ili kufanikisha kazi zako za production?

Katika production natumia sana keyboard kwa kupiga ala za muziki pamoja na ku manipulate sampuli mbali mbali ili kuunda midundo na software hua natumia Fruity Loops na Cubase.

Waeza niorodheshea baadhi ya Albums, Mixtapes, Eps ulizoziunda au zilikua chini ya usimamizi wako?

Orodha ya baadhi ya miradi niliyofanya (albums, mixtape na eps) ni Siku Njema album-Yunani Empire, Loyal To The Truth album-SAWINA, Njia Sahihi Ep-Nala Mzalendo, Utu Na Watu Ep -Mentality, Mionzi album- X-Ray Vina, Panga Mbili- Pizo Madawa, Penda Unachofanya- Sajo MC, Gang Kubwa-Maujanja Sapplayaz, Akili Kichwani Ep, Trickson Knowledge x Nala mzalendo, Dreams- Lugombo MaKaNTa ( washiriki wengine wa hii ni Hayati Burn Bob [R.I.P], 10th Wonder, Old Paper na Dabo.)

Je kando na kuwa sound engineer una uwezo wa kupiga vifaa gani vya mziki?

Kifaa ninachokipiga kwa kiasi kikubwa ni keyboard/kinanda.

Tueleze kidogo kuhusu AMG records? AMG inamaanisha nini na ilianzaje? Nini kilichofanya mfanikiwe? Je kando na WG kuna ma producer wengine wanaofanya chini ya usimamizi wa studio za AMG?

AMG ni recording studio ambayo tuliiasisi mimi na Benedicto (Boika) ambaye ndiye aliipa hilo jina. Boika pia ni producer ila kwa sasa amejikita katika video productions (kumbuka huyu ndiye nilianza naye maswala ya muziki kabla hatujafika hapa tulipo.

Kilichofanya tufanikiwe ni kuheshimiana katika teamwork, kukiheshimu tunachokifanya, kupendana na uwajibikaji katika majukumu ya kila siku ya muziki na tabia endelevu ya kutafuta maarifa kuhusiana na uboreshaji wa tunachokifanya katika shughuli za muziki.

Je unatengeneza aina gani ya miziki?

Aina za muziki ninazotengeneza hasa ni Hip Hop/Rap na R&B na miziki ya aina hiyo.

Kazi ya sound engineer ni nini na kuna utofauti gani kati ya producer ambae amesomea Sound Engineering/Uhandisi Wa Sauti na yule ambaye hajasomea? Wewe umeisomea kazi hii?

Kazi ya sound engineer katika muziki ni kuwa na / au kuandaa sound plan ya wimbo kabla ya kuanza utayarishaji na kuwezesha mazingira sahihi ya ubora wa wimbo kabla ya uundaji, wakati wa uundaji na baada ya uundaji, kwa kuzingatia mazingira ya uundwaji wa wimbo, vifaa na software vyenye/zenye ubora sahihi, ubora wa vyanzo vya sauti ikiwa ni pamoja na vyombo vya muziki na sauti za wanamuziki, mchakato na mpangilio wa kurekodi na uchakataji baada ya kurekodi hadi wimbo unakamilika tayari kwa kusikilizwa.

Tofauti kati ya producer aliye na maarifa ya sound engineering na asiyenayo ni kutofautiana viwango vya nyimbo kwa kuzingatia wajibu wa sound engineer nilioutaja hapo juu.

Kuhusu mimi kusomea au kutosomea sound engineering ni kwamba nimejifunza nje ya taasisi za elimu kwa sababu naamini maarifa yoyote unayoyataka katika shughuli zako unaweza kuyapata hata bila kupitia taasisi za elimu swala uwe unajua ni nini unataka na wapi utapata na uthabiti wa nia ya kujifunza. Ilipo nia na njia ipo hapo hapo.

Je wewe pia ni emcee na una miradi yako binafsi?

Mimi pia ni emcee na nina mradi wa album mmoja ambao nilishirikiana na Nala mzalendo na Sajo MC, unaitwa Loyal To The Truth ila sijajikita sana huko nimejikita katika utayarishaji, u emcee unanisaidia katika kuboresha kazi za ma emcee wengine (hasa wanaokua) ninaofanya nao kazi.

Ilikuchukua mda gani hadi Wise Genius aanze kusikika ?

Kuanza kusikika haikunichukua muda mrefu kwa sababu hata kabla ya kuanza kuwa producer nilikuwa karibu na jamii ya muziki tangu ukuaji wangu kwa hiyo ilikuwa ni kama maisha yetu ya kila siku yamehamia ngazi nyingine. Tulianza kushirikiana sisi kwa sisi na miongoni mwetu walikuwepo waliokuwa wakifahamiana na jamii zingine za mbali na sisi ila kikubwa ni wengi hasa wa karibu yangu walipenda ninachokifanya kwa muda mfupi sana.

Style ya kazi zako mimi binafsi nikiskia ngoma yako bila kujua nani alieunda mdundo mara nyingi naweza kisia umehusika na nikawa sahihi? Hii style yako ya kuunda midundo aina hii unaizungumziaje?

Utofauti wa style yangu ya kuunda midundo imetokana na imani yangu kuwa kila binadamu ana kitu chake kizuri ambacho hakifanani na mtu anachotakiwa kufanya ni kutojifananisha na wengine na kuwa mbunifu yeye kama yeye. Hata sura tukijitazama binadamu hazijafanana kikamilifu ila zote ni za binadamu kwa hiyo hata shughuli zetu zinaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu ila zote zikawa nzuri na bora. Tujifunze kubuni vyetu na kuheshimu vya wengine kwa kiwango chake.

Mwaka huu umekua busy sana, nimeona umehusika kwenye miradi sio chini ya mi nne? Tueleze kidogo kuhusu work ethic yako? Pia niorodheshee projects ulizohusika mwaka huu wa 2021

Work ethics zinazotumika katka ufanyaji kazi wa kila siku ni uwajibikaji kwa wakati kwa kila namna inayolazimu kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ubora.

List ya miradi ya mwaka huu iliyokwisha kutoka ni Gang Kubwa album - Maujanja Sapplayaz, Mionzi- X Ray Vina, Akili Kichwani- Trickson Knowledge x Nala Mzalendo, Penda Unachofanya - Sajo MC, Dreams the album-Lugombo MaKaNTa hii imehusisha na producers wengine pia kama nilivyowataja awali.

Kwa maoni yangu naona pia unafanya kazi kibao na ma emcee chipukizi, unalizungumziaje swala hili?

Ni kweli nafanya kazi sana na ma emcee chipukizi kwa sababu naamini katika kukuza vinavyokuwa ili vije kuwa vikubwa baadae. Na hii pia ni hatua muhimu ya ukuaji wa vipaji napenda niwe mmoja kati ya wanaovizingatia hivyo vipaji angalau kwa kutoa service kwa nafasi yangu.

Je unaelezeaje mtindo wako wa kufanya kazi na msanii ?

Mtindo wangu wa kufanya kazi na msanii ni wa muundo wa uwajibikaji wa kila mhusika katika nafasi yake ukihusisha kusikilizana na kuheshimiana na kupeana nafasi ya kutosha katika utekelezaji wa majukumu ndani ya muda mahususi wa kufanya kazi husika ili kutimiza lengo lililopo.

Ni wimbo gani au mradi gani unaoupenda sana ambao uliufanyia kazi?

Wimbo au mradi ninaoupenda kati ya yote niliyofanya ni mingi ila siwezi kutaja hapa ili kuepusha misconceptions katika watu kwa kuzingatia nafasi yangu katika ninachokifanya.

Gharama zako kwa kazi hii ni kiasi gani?

Gharama ya kazi yangu inategemeana na mambo mengi yanayohusika katika mradi, inahusisha makubaliano ya aina tofauti tofauti.

Je ni jambo gani moja kila wimbo lazima uwe nalo ili uwe thabiti?

Katika kila wimbo nazingatia ubunifu na utofauti.

Je mziki hususan Hip Hop unalipa? Je unaweza kusema kwa asilimia 100 kua mziki wa Hip Hop unakuwekea chakula mezani? Je unaweza kuwaambia watu kwa ujasiri kua mziki wa Hip Hop ni ajira tosha?

Kuhusu kulipa au kutolipa inategemeana na lengo kuu la mtu husika na tafsiri ya faida kwake katika anachokifanya na mfumo wake wa kuwekeza na kuvuna kinachotokana na alichopanda na anavyotumia muziki wake katika shughuli zingine ambazo zinapata content kutoka katika Hip Hop music.

Kwangu mimi naona unalipa kwa sababu mbali na uuzaji wa miradi ya nyimbo kuna bidhaa nyingine za kiutamaduni wa Hip hop zinazaliwa na hizi zinauzwa zinaingiza pesa. Mfano Mradi wa Gang Kubwa una mavazi pia ya Gang Kubwa ambayo yanauzwa  na watu wanazichanga.

Kuhusu kuwa ajira au kutokuwa ajira tosha inategemeana na ni skills gani na ni strategies zipi unazitumia kwa lengo lipi! Kwa hiyo kila mtu ajitathmini yupoje katika hayo yote. Hiyo ni katika kila jambo la kiuwekezaji.

Nje ya muziki Wise Genius hujishughulisha na nini?

Nje ya music Wise G hujihusisha na ujasiriamali.

Unazungumziaje game ya hip hop underground/handakini toka Tanzania na Africa Mashariki?

Game ya Hip hop underground toka Tanzania na Africa Mashariki ipo na miradi ipo na inaendelea kufanywa kutoka maeneo tofauti tofauti kwahiyo watu waongeze tu mbinu na ubunifu katika maeneo yote yanayoihusu underground hip hop.

Kama ni changamoto katika kila jambo hazikosekani, kisichokuua kitakukomaza kiaskari twenzetu mbele tuache lawama tujitegemee, nguvu ya kulaumu ihamie kwenye kutatua changamoto.

Kwa maoni yako ni nini kinacho mtofautisha emcee mwenye uwezo na whack emcee?

Katika Hip Hop, emcee mwenye uwezo ni muwasilishaji ambaye anawasilisha maudhui yenye uhalisia either aliyo/anayoyaishi ama yanayomzunguka kutoka katika jamii aliyopo akiwa na lengo la kuelimisha au kuburudisha ama vyote kwa pamoja. Whack emcee anawasilisha maudhui ambayo ni illusion na havina uhusiano na uhalisia.

Tutegemee nini toka kwa Wise Genius hivi karibuni na baadae?

Kuna miradi ipo inaandaliwa itatoka muda uliopangwa, ni ya emcee's wapya zaidi wakali na wengine wanaofahamika. Imepikwa kiustadi wadau wakae mkao wa kula.

Changamoto unazokabiliana nazo ukiwa kazini au kwenye hii fani yako ni zipi?

Changamoto zipo za kawaida ambazo nazitumia kama ngazi ya kujiboresha zaidi ninapopambana nazo sizichukulii kama kitu kibaya. Nafsi ya mtu inakua kwa kasi ikipata changamoto endapo utakaa nafasi sahihi katika hali husika. Na haya yote tunayofanya chanzo chake ni nafsi.

Ni nini cha mwisho unachoweza kutuambia ki ujumla ambacho sijakuuliza?

Kitu cha mwisho ninachoweza kuwaambia ni kuwa nipo grateful kwa wote mnaounga mkono harakati zetu kwa namna moja au nyingine wadau wote, wateja wa miradi yetu wasambazaji wa taarifa za harakati zetu.

Shukran kwa Micshariki Afrika. Niwaambie tu mtavuna mnachopanda kwa wakati. Blessings sana.

Shukran sana pia kaka Wise Genius.

Wasiliana na Wise Geniuz kupitia mitandao ya kijamii;

Facebook: Wise Geniuz WG (MD)
Instagram: Wise_Geniuz_WG