Uchambuzi Wa Album: Mionzi The Album
Emcee: X-Ray Vina
Tarehe iliyotoka: 14.05.2021
Nyimbo: 18
Mtayarishaji, Mtayarishaji Mtendaji, Mixing & Mastering: Wise Geniuz
Studio: AMG Records

Nyimbo Nilizozipenda: Inaonekana, Mionzi, Mionzi 2, Kimachale, Kivuli, Wito, Usichojua, Naigusa, Mwisho, Classmate, Baba Mwenye Nyumba, Msomi, Punde, Mpo Karibu, Usingizi Vitani

X Ray Vina

Baada ya rafiki yake kuona uwezo wa Omary Seif Dihile wa kutazama mambo kwa undani aliamua kumbatiza jina ambalo ndilo tunalomfahamu nalo ki usanii, X- Ray Vina. Mashine ya X-Ray hutumia Mionzi ili kuweza kupenya kwenye vitu na kuweza kutuonesha uhalisia wa kitu kiundani.

X –Ray Vina mwaka jana alifanikiwa kuachia album yake ya kwanza Mionzi ambayo kwa kutumia uwezo alionao wa kuona kiundani aliyopewa na muumba wake anaweza kuangalia kiundani na sio tu kubaini matatizo bali hata kutoa ushauri ya nini kifanyike ili kuweza kutatua matatitzo hayo.

Kazi hii ambayo imesimamiwa kwa asilimia mia na Wise Genius wa AMG Records inaanza na Intro akisema kuwa, “Mionzi, tiba kwa yaliokusibu” na hili unaliona tu kila mahali kwenye mradi huu.

Uzuri wa mradi huu ni kuwa emcee huyu amesimama mwenyewe kwa asilimia kubwa tofauti na kwenye kazi kadhaa alipowashirikisha wasanii wengine kama vile Nala Mzalendo kwenye Inaonekana ambao pamoja na kwenye Kimachale ambapo anamshirikisha Sammy ambayo pia ilikuwa singo ya kwanza kuachia toka kwa mradi huu. Sammy alishirikishwa tena kwenye Hitaji.

Pia wasanii wengine walioshirikishwa kwenye mradi huu ni Trickson Knowledge na Nala Mzalendo kwenye Wito ambayo ndiyo ilikuwa “singo” ya pili rasmi kutoka kwenye kazi hii. Wengine walioshirikishwa ni Mbanga na mtayarishajii Wise Genius kwenye Kimya, Frege kwenye Punde. Mwishoni mwa mwaka jana emcee huyu pia aliangusha singo ya tatu toka kwa mradi huu akiwashirikisha ma emcee Shaulin Seneta na Kondoo kwenye Usingizi Vitani.

Inapokuja kwenye upande kuhadithia emcee huyu anatuonesha uwezo wake kwenye nyimbo kadhaa kama vile Classmate ambao anamkumbuka rafiki yake ambaye walisoma nae shule, hii true story naona. Rafiki huyu baadae alibahatika kupata kazi jeshini ila kwa bahati mbaya alifariki akiwa vitani, “RIP hustler/ Wilson Kimaro Mungu akulaze pema peponi kaka/”. Wise Genius anampa mdundo mzuka sana wa kumuenzi mwana.

Story nyingine ambayo wakati huu ni ya kubuni ni Baba Mwenye nyumba ambapo emcee huyu anaongelea vile alikuwa na pupa ya kujitegemea akaamua kuhama toka nyumbani na kupanga kwa Mzee Mwandulela. Kwa ucheshi anatuambia vituko alivyopitia toka kwa Father House akisema,

“Miezi ikapita mambo yakabadilika/
Nikaanza kuona mambo yaliyojificha/
Ana masharti kama mganga/
Cha kwanza hakuna kula mpaka yeye ashibe kwanza/
Asiskie unapika wali nyama/
Kwenye nyumba yake ukithubutu tu umehama/
Sio siri ana vituko vya kukera leo kapewa kodi kesho anakukopa hela/”

Hadithi nyingine anayoiwakilisha vizuri ni Msomi ambayo inaongelea changamoto wanazopitia wasomi wengi ambao baada ya kuhitimu elimu hii haiwaletei manufaa waliyoyatarajia. Kwenye wimbo wenye beti moto emcee anaweka bayana kinachowaponza wasomi akisema,

“Msomi chenga,
Ameenda shule sawa ila cha ajabu anakosa dira/
Hana elimu ya ugunduzi ndio maana anawaza ajira/
Ya serikali haitaki kumuajiri/
Na ikiajiri ni kisanga mshahara kitendawili/
Yuko freshi kwenye theory praci anayumba/
Kala jumba chini Moca na kingeli cha kuzuga/
Msomi wa kibongo longo longo kibao/
Ana ndoto ya kujenga akishapata mafao/
Ya kustaafu maana anaongoza kwa madeni/
Nyie acheni hali ngumu ashakopea hadi pensheni/
Hana ishu amebakia na mdomo wa kujisifu/
“Nimesoma, nimesoma”, na mfukoni hana kitu/
Analalama jamii haimthamini/
Matusi anatukana “Sa’ nimesoma kwa nini ?”/
Hawezi kujiongeza kwenye mishe ndogo ndogo/
Za ukulima na biashara ila kaongeza nyumba ndogo/
Amesoma na hajaelimika/
Anashindwa kuja msibani kisa hajapewa taarifa/
Kuzika, sifa ndio zinamponza/
Anachagua kazi, “Mi’ siwezi kuwa konda!”/….”

Ngoma hii ni noma sana, mionzi imepenya hadi sekta yetu ya elimu na kuhoji kama wasomi wanaotoka shule kila kukicha wana vigezo vya kujisimamia sio tu kwenye ajira bali hata pale wanapojiajiri.

Kupitia Mionzi ya mtu mashine X –Ray Vina tunaweza kuona kwa kina mtazamo kuhusu maisha yetu ya kila siku; changamoto, mahusiano, matumaini na vituko vya uswahili kwenye maisha yetu ya kila siku. Shabiki yoyote wa Hip Hop lazima aende apigwe X- Ray na Dr. Vina kwa kutumia Mionzi yake.

Kupata nakala yako ya album hii kwa Tshs 10,000.00 (Kes 500.00) wasiliana na X-ray Vina kupitia;

Facebook: X-ray Vina
Instagram: x_ray_vina
WhatsApp: +255654054352