X-Ray Vina

X-Ray Vina sikuwa namfahamu kivile. Mwaka jana niliona wana wakinadi album yake Mionzi nikaamua kumcheki nipate nakala yangu ili niskie alichonacho huyu jamaa.  Kazi yake niliipenda nikaona ni vyema sio tu kuichambua bali kumtafuta na kupiga nae story ili mimi na wasomaji tuweze kumfahamu fresh emcee huyu.

  • MkoKeNya

Karibu sana Micshariki Africa kaka X-ray Vina. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu, unaitwaje rasmi, unatokea wapi na unajihusisha na nini?

Kwa majina naitwa Omary Seif Dihile, natokea Mbeya na najihusisha utamaduni wa Hip Hop (mchanaji).

X-ray Vina, mbona ukaamua kujipa jina hili? Jina lilikujaje na linamaanisha nini?

Jina la X-ray nilipatiwa na rafiki yangu mmoja baada ya kuhisi na kuona uwezo wangu wa kutazama mambo kwa undani zaidi ndipo akahusianisha hiyo hali na X-ray Machine

Tueleze kidogo kuhusu historia yako ya nyuma ya maisha na muziki. Umezaliwa wapi, umesomea shule gani na umefikia wapi kimasomo? Je mziki ulianzaje?

X-ray nimezaliwa mkoa wa Dar es salaam ,na nimepata elimu ya msingi katika shule ya Kimara B na elimu secondary (O level) katika shule ya Anne Marie Academy na kisha kuendelea na advance (form 5&6) Mbezi High School  na mpaka sasa nina Shahada Ya Elimu katika Masomo Ya Sanaa(Bachelor Of Arts) niliyoipata katika chuo cha Teofilo Kisanji (TEKU).

Muziki nimeanza baada ya kupata hamasa kutoka kwa familia yangu ikiwemo kaka zangu ambao walikuwa wanachana kipindi hicho na kuanza kufanya taratibu vitu kama mitindo huru mpaka leo nilipofikia hapa.

Mpaka sasa umeachia miradi mingapi, inaitwaje, imetoka lini na inapatikana wapi ?

Mpaka sasa nimeachia mradi mmoja tu ambao ni Mionzi album inayopatikana kwa soft copy ambayo nimeiachia mwaka 2021.

Tueleze kidogo kuhusu mradi wako Mionzi? Kwa nini Mionzi maana mionzi niijuayo si kitu cha kuchezea.. Mradi huu ulisimamiwa na nani na maudhui yake ni yapi ?

Mradi wa Mionzi umesimamiwa na AMG studios chini ya Wise Geniuz. Mradi niliuita Mionzi kwa maana kuu ya tiba na maudhui yake ni kuamsha jamii kifikra kuhusu masuala mbalimbali katika mtazamo chanya kupitia ukali wangu (kwa maana mionzi ni mikali).

Ni ngoma gani ulizozipenda ndani ya album hii? Hebu tueleze kuhusu wimbo unaopatikana kwenye album hii Usingizi Vitani? Nani kalala vitani na ni vita gani unavyoviongelea, au Ukraine na Russia?

Ngoma karibu zote nazipenda kwa sababu nyimbo nyingi ni hisia za ukweli kabisa.

Usingizi Vitani ni wimbo wa kuwashtua watu kifikra kwamba wasijisahau na dhana ya usingizi ni kuridhika na vitani maana yake matatizo mbalimbali kwa hiyo lengo ni kuamsha watu wasihisi hakuna shida kwa furaha ya muda mfupi bali ni kupambana kitu muhimu sana.

X-Ray gharama za uandaaji wa miradi kama huu wako zikoje? Kwa emcee chipukizi mwenye ndoto za kuangusha album unamshaurije?

Gharama siwezi nikasema moja kwa moja kwa kuwa huu mradi ulikuwa chini ya usimamizi wa AMG Studios, na album ni kitu kizuri na kikubwa katika maisha ya mchanaji yeyote au msanii lakini hupaswi kukurupuka kufanya kwa sababu album inahitaji muwala wa nyimbo na mawazo toka Intro mpaka mwisho. Kwa hiyo ni lazima upate utulivu wa akili íli kutoa kitu kizuri na kuweka kumbukumbu katika maisha ya sanaa. Huo ndio ushauri wangu.

X Ray kando na uchanaji, je una vipaji gani vingine?

Ukiachana na uchanaji X-ray ni mchezaji mpira wa miguu. Uchezaji mpira wa miguu ni kipaji changu pia ambacho niko nacho.

Ni nini kinachomfanya mtu azidi kuwa emcee bora na sio bora emcee?

Kinachomfanya emcee kuwa bora ni kuishi katika uhalisia na sio hisia mfano kupenda kujifunza ,kuijua hadhira yako na jamii kwa ujumla. Hii humsaidia emcee kuwa na utunzi wa mashairi yenye mguso kwa jamii

Tutarajie nini toka kwako hivi karibuni?

Hivi karibuni natarajia kuachia wimbo wangu mpya kabisa ndani ya mwezi wa nne.

Kipi cha mwisho ungependa kutuambia ambacho sijakuuliza

Cha mwisho ni shukrani nyingi kwa Micshariki Afrika kwa kunipatia fursa na wasaa wa kuelezea kwa ufupi kuhusiana na mradi wa Mionzi.

Kikubwa wadau na mashabiki nawakaribisha kujipatia nakala halisi ya Mionzi kwa gharama ya elfu kumi(Tshs 10,000.00) pekee íli kuweza kupata elimu na maarifa. Asanteni sana. Upendo Utuongoze.

Shukran sana kaka X-ray Vina kwa muda wako.

Shukran sana kaka!

Mfuatilie X-Ray Vina ili kusapoti kazi na harakati zake kupitia mitandao ya kijamii;

Facebook: X-Ray Vina
Instagram: x_ray_vina