Black Ninjah

Kwa kawaida mtu anaposikia neno Black Ninja picha inayokuja fasta akilini mwake ni ya mtu aliyevaa nguo nyeusi mwili mzima na pia kuziba uso wake wote isipokuwa macho yake ili kuzuia watu wasimuone sura na kumfahamu. Pia mtu huyu mara nyingi hubeba upanga mgongoni ambao ni silaha yake kuu anayoitumia kujilinda na kulinda jamii yake.

Kwenye ulimwengu wa Hip Hop,Tanzania kuna Black Ninja ambaye yupo tofauti kidogo. Kitu ambacho ni cheusi pekee mwilini mwake ni ndevu zake zinazong’aa kwenye kichwa ambacho mara nyingi kanyoa upara. Silaha yake kuu ni kinanda, kinasa, kipaza na studio inayomuwezesha yeye kufanya kazi ya kusaidia wana Hip Hop kuunda miradi yao. Black Ninja huyu ni producer toka  studio za Boombap Clinic (B.B.C) Dar Es Salaam.

[Updated 2025]

Leo tumepata fursa ya kufanya mahojiano na Dr. Black Ninja, karibu umfahamu...

Black Ninjah ni nani, kazaliwa wapi na anatokea/kupatikana wapi? We ni muunda midundo tu/beat maker au producer?

Black Ninjah ni Mtozi au (Producer) wa muziki wa kufoka(rap), DJ, pamoja na mwalimu wa muziki na Utamaduni wa Hip Hop Tanzania.

Nimezaliwa Mbeya mjini, mtaa wa Ilolo. Baba yangu ni Mmbunga kutoka Ifakara -Morogoro ila Mama ni Mnyakyusa. Kiasili mimi ni mtu wa Ifakara, ila kiuzalendo mimi ni mtu wa Mbeya.

Mimi ni Producer, napiga midundo na kuchakata sauti.

Jina lako la kwenye kitambulisho ni nani?

Kwa majina kamili naitwa Shukuru Matonga.

Kwanini unajiita au unaitwa Black Ninja? Jina lilikujaje na linamaanisha nini?

Jina la Black Ninjah nilipewa na marehemu mama angu mzazi Bi Sophia Adamson Mwambuta. Mama alikuwa anapenda sana Movies za ngumi. Tulikuwa tunaenda pamoja kwenye mabanda umiza kipindi hicho miaka ya 2000 pale Ilolo na Mafyati, kuna Movie ilikuwa inaitwa American Ninja na hii mama alikuwa anaipenda sana yani alipo kuwa akirudi kutoka kwenye pombe zake amelewa basi alikuwa akiniita “Ninjaaah Ninjaah wangu!” na ndie alikuwa anapenda rap music kwenye banda lake la pombe alikuwa na kanda nyingi sana za muziki wa rap ziikiwemo za Mr II aka Sugu, Professor Jay, Solo Thang na wengine wengi. Hapo ndio historia ya hili jina likazaliwa kwenye maisha yanga.

Kwanini wajiita Doctor Black Ninjah, ulihitimu na Phd?

Hii ni heshima nayo kuwa napewa na watu wanaokubali uwezo wangu. Mimi nina Degree ya Music pia nilipo namalizia degree yangu ya pili ya mambo ya music naelekea huko kwenye Phd Insha’Allah baada ya miaka 4 ijayo nitakuwa Professor wa muziki.

Tueleze historia yako kwenye matumizi ya Native instrument (Maschine Mk3)?

Nilianza kutumia Akai MPC 500 miaka 8 iliyopita ila baade nikafanikiwa kupata Mk3 nilijikuta navutiwa sana na Maschine kwakuwa kwangu ilinipa wepesi wa kuweza kupiga beat kwa haraka na kufanya mambo mengi na mtu alienivutia zaidi ni kuweza kupenda na kutumia mtambo huu ni mtayarishaji Nottz kutoka Marekani. Kwangu mimi Maschine Mk3 ni moyo wangu japo pia naunda beat pia kupitia Akai Mpc 5000  mfano beat kama “999” ya Nikki Mbishi, “Futi Sita” ya P Mawenge na zingine nyingi.

Mimi situmii software kuunda beats -napenda kutumia analog equipments kwakuwa nafurahia.

Unawezaje kufanya live beat making na Maschine MK3?

Mimi najifunza kila siku na pia nafanya sana mazoezi. Hii inapelekea Maschine niweze kuichezea navyo taka mimi. Maschine ni nzuri sana na ninyepesi sana tofauti na Mpc. Mara nyingi napokuwa na tukio la kufanya show ya kupiga beat mbele ya hadhira huwa na beba Maschine kwakuwa inafanya naunda beat chap chap ,japokua Mpc 5000 pia ni nyepesi sana ila ndio kuna sequence zake zinachukua muda kuweza kwenda sawa inapokuja maswala ya timings.

Maschine beast shows kati ya Black Ninjah na Cjamoker (South Side Brothers), nani alitoa hili wazo na kwanini mliamua kwenda wawili mikoani kufanya shows zenu za kupiga beats live?

Nilikaa kuwaza nani atafaa kufanya live beat making show kwa kutumia kifaa na sio software katika kutafuta nikaona anaweza Cjamoker kwakuwa huwa anajua kutumia Maschine pia na hizo softwares kuunda dundo.

Pia ana Maschine MK 2 Ko nika check nae na akakubali. Basi tuka match, lengo ni kuhamasisha beat makers kutumia vifaa na pia kutengeneza nafasi kwa makampuni ya vifaa vya muziki kutoa nafasi kwa ma producers wetu wa Tanzania. Mimi naona tunapoishia kwenye ma software wote inakuwa sio njema sana japo sio dhambi.

Ulianzaje shughuli ya u producer na ni kipi kilichokupatia motisha kubaki hapo?

Daaah aiseeh nilianza kama DJ ambae nilikuwa natumia deki za CD kipindi hicho Ifakara - Nilikuwa naishi kwa kakangu na kuna siku kaka alileta deki mbili nyumbani za CD. Ile siku nilibahitika kubakizwa mwenyewe ndani katika utundu utundu nilijikuta nimeweka CD kwenye deki zote nikasema nitafanyaje zote zitoe sauti! Kwa hivyo katika kuwaza nikagundua kuna waya mweupe wa sauti na mwekundu ambao unatoa sauti kwa mbali sana. Kwahiyo nilipo toa waya mweupe kwenye deki (A) sauti ikawa Chini nilipo chomeka deki (B) sauti ikawa juu na zote zilikuwa zipiga miziki tofauti kwenye Spika moja …..

Nikapata bahati ya kuwa nashinda kwenye maeneo ya sherehe na kuna bro akaniamini akawa anasema niwe nabadilisha CD muziki ukiisha, nikawa sasa naleta ule utundu wangu mwisho akanikubali na nikawa nawapigia wasanii wengi kwenye mashow yao pale Ifakara akiwemo Ferooz, Mr Blue, Juma Nature, Professor Jay na wengine wengi.

Utamu wa muziki ukanikolea sana nilipo badili makao na kwenda Bukoba - ndipo nikakutana na jamaa yangu anaitwa Jevs Jasper huyu ndie akanifunza kutumia Computer na alikuwa anapenda kurap na kuimba akafanya mpango tukapata Fl studio 9 hapo ni mwaka 2011 tupo kidato cha kwanza pale Lakeview, na Cubase H2O znzi hizo. Yeye aliniambia hivi, “Ninjah jitahidi wewe uwe producer na mimi nitakuwa msanii wako, kwa hiyo wewe pambana kujua beats mimi nipambanie miistari…”

Tulikuwa tukijiiba na kwenda kwenye mastudio ya watu na kutazama alafu nakwenda kufanya nilicho kuwa nimekiona. Ilinichukua wiki kadhaa nikawa napiga beats ila zilikuwa bado hadi nikaja kulink na Kibabu Wapoten kule Facebook akaanza kunitumia video na maelekezo ya namna ya ku-sample beats hadi nikawa master.

Motisha wa kubaki hapa ulitokana na kutokuwa na ishu nyingine pia kwenda chuo kikuu kusoma muziki ikanifanya hii kitu kuipa nafasi kubwa sana katika maisha yangu.

Je unatengeneza aina gani ya miziki?

Natengeneza mziki wa rap na RnB tu!

Ulishawahi kuwa na shaka kuwa utafanikiwa kwenye hili?

Sijawahi kuwa na shaka juu ya hili kwakuwa nimechagua mimi mwenyewe kufanya hiki kitu.

Ni kipi kilichokusukuma usiache fani hii?

Sina kitu kingine nacho weza fanya zaidi ya muziki na ndio msingi wangu unao fanya naendesha familia yangu nina mtoto wa kike anaitwa Nina a.k.a Soul sister 2 (na jina lake nimetoa kwa Nina Simone hahah) mama shujaa wa muziki wa Jazz Duniani. Anapata kila kitu kupitia hii fani pia nina jukumu la kuijenga jamii kifikra na kuikomboa kupitia utamaduni wa Hip Hop.

Ilikuchukua muda gani hadi kuanza kusikika na kutambulika kama producer?

Ilinichukua miezi mitatu kuwa producer mkali na yote ni kwa sababu ya shida nilipo rudi Dar baada ya kumaliza form 6 nilikuwa sina ishu yoyote ya kufanya nikasema sasa nakomaa na muziki nijue kila kitu ili niweze kuutegemea na kujisomesha chuo kikuu kwahiyo nikakaza buti nikakesha sana kwenye PC na mwisho ndio mambo yakawa poa.

We hupata vipi wateja wako?

Kupitia kupost sana beats na kufanya kazi na wasanii wengi zaidi wanao chipukia na wakongwe ila kubwa zaidi kuweka ukaribu mzuri na wasanii wote kwa nafasi zao hiyo ndio nyenzo bora.

Ungetoa ushauri gani kwa yoyote anayependa kufuata nyayo zako?

Asiwe mvivu. Inatakiwa apambane sana katika kujifunza kila siku. Mimi kila siku najifunza kitu kipya kwenye muziki, nasikiliza sana kazi za ma-producers’ bora wa rap duniani ndani na nje ya nchi. Pia kujiamini muhimu kwani mimi inapofika kwenye kitu hiki cha Boom bap najiamini sana kwakuwa najua ninachokifanya.

Ushawahi kupata kazi kutoka wasanii wa nchi za nje?

Yeah nimefanya kazi na wasanii kama Essence kutoka North Carolina, RapOet kutoka New york, Dhemi kutoka LA, na Laobma kutoka Paris France. Pia tupo kwenye mpango kazi na legendary emcee Edo G kutoka Boston. Kazi zitatoka na kusikika Insha’Allah. Kwa upande wa nchi za Afrika mashariki kama Kenya nimefanya na Kaa La Moto, Kayvo K force, Oksyde, Igee Africa na wengine wengi.

Umeshafanya kazi na ma emcee gani na kwa miradi gani?

Nimefanya kazi na Kalapina, Saigon, Nikki Mbishi, ConBoi, P Mawenge, Songa, Maalim Nash, Jcb, One The Incredible, Nyenza Emcee, Cado Kitengo, Ghetto Ambassador, Rabi James, Boshoo Ninja, Wagosi Wakaya, Kay la Mapacha, ChindoMan, Wakazi, Mex Cortez, Young Killer, Mchizi Moxie, Stereo Singa Singa, KadGo, Azma Mponda, Izzo Business, wasanii wengi sana na miradi ni mingi sana pia.

We upo chini ya umiliki wa studio ya mtu au unamiliki studio yako mwenyewe? Tueleze kuhusu B.B.C, historia yake kidogo?

Niko chini ya ofisi yangu mwenyewe. BoomBap Clinic (B.B.C) ilianza 2015 nikiwa na mwanangu John Paul Kirenga - Bukoba alikuwa ni mmoja kati ya watu walio saidia kupatikana kwa jina la Boom  Bap clinic  ila kwa sasa mimi mwenyewe ndio naongoza Boom Bap Clinic  (B.B.C) nikiwa chini ya taasisi mbili (Hakuna Matata 101 na The (TZ ) Connection ) awa ndio walezi wakuu wa Black Ninjah na BBC yake  bila kusahau idara nzima ya BBC management ikiwa chini ya Wakili Octavian John Kamugisha na mameneja wanne. Hadi sasa BBC inasimamia msanii mmoja tu wakike anaitwa Tabby.

Ile sign tune yako ya “BBC once again!” ilikujaje?

Ile ilikuwa 2017 pale Sinza – Mori, nilikuwa nafanya kazi kwenye studio ya Success Music chini ya Chief Elia. Ilikuwa weekend niko na mdogo wangu Phina The Truth studio tuna record ngoma fulani inaitwa “Mbibi” alipoingia booth nikamwambia ok twende anzisha akaipiga hiyo.

Mwanzo siku zingatia ila nilipo kuwa na mix sauti akili ikaanza kuelewa hicho kitu hapo nilikuwa nataka nipate kitu tofauti niache kutumia Black Ninjah Sasa nikaona wacha niende nayo hii “B.B.C once again” tamu sana!.

Boom Bap Clinic (B.B.C)

Je unaelezeaje mtindo wako wa kufanya kazi na msanii?

Napenda kuunda beats nikiwa na msanii ili niweze kufanya matching nzuri, huwa nafurahi kwakuwa napata kitu nacho kitaka.

Je wewe ni mdonoaji? Udonoaji na ubamizaji ni nini?

Udonyoaji unatokana na utumizi wa bifaa hivi-Maschine Mk3, Mpc 5000.

Mimi natumia kifaa kinaitwa Maschine Mk3 na MPC 5000 kutengeneza midundo yote hiyo. Kwenye utumiaji hivi vifaa nakuwa nabonyeza pad kwa kidole kimoja kimoja sasa hii namna ndio inapelekea fasili ya udonyoaji.

Ni wimbo gani au mradi gani unaoupenda sana ambao uliufanyia kazi?

Kazi zangu zote nazipenda sana kuzidi kitu chochote kwa kuwa nafurahia ninacho kifanya.

Gharama zako kwa kazi hii ni kiasi gani?

Gharama zangu uwa nazitoa kuangalia uchumi wa msanii.

Umekuwa ukiskiliza mziki wa aina hivi karibuni?

 Ndio uwa naskiliza miziki mingi kupata sampuli—inaweza isiwe pendwa kwangu ila uwa naangalia vijengo vyake wenda vikawa muhimu kwangu kuundia Boom Bap beat.

Je ni jambo gani moja ambalo kila wimbo lazima uwe nalo ili uwe thabiti?

Uwasilishaji bora na mada thabiti.

Ni nani mtayarishaji bora wa muziki anayefanya kazi katika tasnia hii leo unaye mkubali?

Wote wanao piga Boombap beats nawakubali sana.

Nje ya muziki Black Ninja hujishughulisha na nini?

Biashara na ufugaji.

Ni watayarishaji gani, waimbaji au wasaniii waliokupa motisha yako ya msingi?

Nottz, Jay Dilla, Diamond D, Pete Rock, Kev Brown, Dj Premier, Erick sermon ,45 King, Madlib, Black Milk na wengine kibao/

Unazungumziaje game ya underground Hip Hop /handakini toka Tanzania na Africa Mashariki?

Game ya underground hapa kwetu tuko vizuri japo bado changamoto ipo kwetu wenyewe ni lazima tufike muda tupambanie mazingira yetu ya kiburudani yawe na burudani sahili na tufike hatua kubwa ila wadau wapo kama wameridhika na wakifanya vitu vinakuwa kama utani fulani yani mazingira fulani ya kwenda kupotezea muda.

Mfano Mimi nimeweza kuja na TuKuSa cyphers zimekutanisha wasanii kibao ambao wenda wasinge kutana pia nikawaza zaidi Nimekuja na TuKuSa, festival hii ndio festival ya kwanza Tz ya Underground Hip Hop sahili achana na hizo zingine ndani yake zina michanganyiko kibao, yote ni kupambania hii kitu ndani na nje Tanzania.

Kwa hiyo lazima tufike pahala tukubali tunahitaji kurekebisha namna yetu ya ufanyaji hii kitu.

Je ni masomo gani muhimu ambayo umejifunza juu ya kutengeneza midundo ambayo ma producer pamoja na wasanii chipukizi wanaweza kujifunza?

Music theory, piano instructions, selection of instrument.

Mimi nime specialize kwenye Native instrument-Maschine Mk3 kama chombo changu cha kuundia beats sipendelei, software kupigia beats mimi napenda kutumia Maschine micro mk3 na Mk3 pamoja na Mpc 5000.

Una miradi yako binafsi iwe ni EP, mixtape and albam ambayo ulishawahi iachia sokoni?

Nina albums “4 “Ilolo confirmed 1,2,3 pamoja na Bumunda, Ep zipo 3, Beat tapes zipo 13.

Zote zipo kwenye digital platforms zote.

Niliona mna mpango wa kufanya kazi na Tenth Wonder, hili unalizungumziaje?

Ni producer aliye Boombap Clinic (B.B.C) anaendeleza harakati zake vyema zaidi.

Black Ninjah na Tenth Wonder

Tutegemee nini toka kwa Black Ninja na team yote ya B.B.C hivi karibuni na baadaye?

Tuna TuKuSa (Tunajua Kuchana Sana) cyphers ambazo zinaunda TuKuSa Clan - na chambers 36 na sasa tumemaliza chamber 2 tupo kwenye TuKuSa Festival tukimaliza hapo tunaanza tena chamber 3 na 4 tunapozi tena na festival.

Lengo kuu ni kuendeleza hisia za underground Hip Hop music katika jamii pia. TuKuSa festival kimataifa zaidi hapo baadae kuweza kuwakutanisha legendaries wote wa Hip Hop kutoka USA na emcee wetu wa Tz

Ni nini cha mwisho unachoweza kutuambia ki ujumla ambacho sijakuuliza?

Nina Academy ya kufundisha Boom Bap na Hip Hop culture inaitwa -Boom Bap academy (BBA) kwa wadau wanaopenda kuwa professional katika beats karibuni sana tunatoa elimu ya mambo haya.

: - Maschine course 1 and 2

: - Fl studio course

: - Cubase, Studio One, Logic, Pro-Tool course

: - Akai Mpc 500 course

Wasiliana na Black Ninja kupitia mitandaoa ya kijamii:

Facebook: Blaq Ninjh(Black Ninja)
Instagram: black_ninjaah
Boombap Clinic(B.B.C) - boombapclinic

Wasiliana nasi kupitia :- +255689091511